TFF wanafikiria kwa akili ya jana, badala ya akili ya kesho

Muktasari:

Safari hii akaunti maalumu ya Tegeta Escrow imedhihirika kuwa fedha Sh321 bilioni zimechotwa zikiwa ni mali ya Tanesco. Jambo hilo limezua mjadala mkubwa bungeni.

NCHI hii hakuna siku inayopita bila kuacha vituko. Baada ya Bunge la Katiba ambalo lilijaa vijembe na kupitisha katiba kiasi cha wabunge kusakata rhumba bungeni, kuna kituko kingine kimeibuka.

Safari hii akaunti maalumu ya Tegeta Escrow imedhihirika kuwa fedha Sh321 bilioni zimechotwa zikiwa ni mali ya Tanesco. Jambo hilo limezua mjadala mkubwa bungeni.

Kama jinsi katiba ilivyopitishwa kitata, hata suala hilo linataka lisijadiliwe kwa madai kuwa kuna kesi mahakamani, hivyo haitakiwi mihimili miwili kujadili suala mmoja kwani huenda kukawa na mgongano katika maamuzi.

Unapoyaona majina yaliyotolewa kwenye mitandao ya kijamii, unashangaa na kujiuliza hivi nani anastahili kuitwa msafi katika nchi hii, kwa sababu wengine waliotajwa usingetarajia.

Unapata hasira, unaamua kufungua kurasa za michezo, unapata kizunguzungu zaidi na unajisemea moyoni ni nani ambaye aliwaroga viongozi wa nchi hii?

Ni wapi umeona Ligi Kuu imechezwa raundi saba tu, halafu inasimama kwa zaidi ya miezi miwili kupisha vitu ambavyo havipo, na wakuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wapo na hawaelewi kinachoendelea. Hawana uhakika kinachoendelea.

Ukizungumza na wakuu wa TFF wanasema walitarajia michuano ya Kombe la Chalenji ingefanyika ndio maana wakapanga ratiba iwe hivyo, lakini baada ya michuano hiyo kuwa shakani au kuota mbawa, wamekosa kuwa na mpango wa pili.

Ni jambo ambalo linafahamika kuwa michuano ya Chalenji hufanyika kimkandamkanda kutegemeana na kuwepo kwa wafadhili, hivyo jambo hili TFF walipaswa kulijua.

Na kama walipaswa kujua ina maana walitakiwa kuwa na ratiba mbili za Ligi Kuu; ya kwanza ingeonyesha iwapo kutakuwa na michuano ya Chalenji na nyingine ingekuwa iwapo michuano hiyo isingefanyika.

Sasa wameibuka na hoja mpya kuwa wanataka kuipisha michuano ya Uhai, ambayo hushirikisha timu za vijana.

Miaka yote michuano hii hufanyika bila kusimamisha ligi, lakini sababu ya pili ni kuwa michuano hii hushirikisha timu za vijana, hivyo ni timu chache ambazo zingeathirika na bado ratiba ingeweza kuendelea.

TFF walitakiwa kufikiria kidogo tu na kufanya Ligi Kuu Bara angalau imalize mzunguko wa kwanza kuliko kufanya kama walivyofanya kwa kuruhusu kila timu kucheza mechi saba tu.

Wakati dunia ikiwa inabadilika kwa kasi kiasi kwamba kila kitu kinakwenda kiteknolojia zaidi, inashangaza kuona TFF bado wanafikiria katika enzi za mawe.

Ligi ndio ilikuwa imeanza kuchanganya iwe kishabiki au kwa wachezaji uwanjani, hivyo kuikatisha njiani ni kuipotezea ladha yake na hasa ikizingatiwa kuwa ikianza tena itahitaji angalau mechi tatu au nne kwa kila timu kuwa fiti.

TFF walihitaji kufikiria hili, kwa sababu halihitaji elimu ya darasa la saba kulijua ila ni ‘common sense’ tu ambayo ingeweza kuchukua nafasi yake kwa wakuu hawa wa shirikisho la soka.

Kinachoonekena sasa ni kama TFF imekata tamaa, haielewi inafanya nini, inafikiria jinsi watu wengine walivyofikiria miaka 100 iliyopita, hawafikirii kwa akili ya kesho, bado wanafikiria kwa akili ya jana.

Ukiona binadamu anafikiria jinsi alivyofikiria jana, ujue kabisa kuwa ana matatizo makubwa na hawezi kupiga hatua yoyote katika maendeleo.

TFF wanapaswa kufikiria kwa akili ya mbele zaidi ili kuwapo katika dunia hii ya mashindano, vinginevyo tutaendelea kutoa sare na Swaziland kwa miaka mingi ijayo.