TFF isifanye mchezo na uhai wa wachezaji

Tuesday December 20 2016Kipa wa Lyon Youthe Rostand

Kipa wa Lyon Youthe Rostand 

UPO msemo wa Kiswahili unaosema mtu hujifunza kutokana na makosa, lakini ni kama vile Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wala halitaki kujifunza kwa makosa ya zamani.

Zimepita takriban wiki mbili na ushei sasa tangu mchezaji chipukizi wa Mbao FC, Ismail Khalfan Mrisho apoteze uhai wake kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kwenye mechi za michuano ya Ligi ya Vijana U20.

Mchezaji huyo alianguka uwanjani baada ya kugongana na mchezaji wa Mwadui, lakini juhudi za kuokoa maisha yake zilishindikana kutokana na uwanjani hapo kukosekana kwa gari maalumu la wagonjwa (Ambulance).

Chipukizi huyo alibebwa na gari la zimamoto kuwahishwa hospitalini kabla ya kubainika kwamba alipoteza uhai wake akiwa njiani.

Wengi walifikiria TFF imejifunza kwa uzembe iliyofanya kwa kuchezesha mechi za ligi ya kitaifa bila kuwapo kwa huduma ya gari la wagonjwa, hivyo kuanzia wakati huo viwanja vingekuwa na huduma hizo kwa ukaribu.

Kuwapo kwa huduma hiyo siyo tu inarahisisha kutoa huduma kwa wachezaji na watu wengine viwanjani, pia linasaidia kuepusha vifo vya kizembe hata kama ni kweli kifo ni mipango ya Mungu na hakuna wa kuizuia.

Hata hivyo, juzi Jumapili kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Azam FC na African Lyon iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam janga jingine lilikaribia kutokea uwanjani hapo.

Kipa wa Lyon Youthe Rostand aliumizwa uwanjani katika harakati za kuokoa mkwaju wa Yahya Mohammed wa Azam na kutibiwa kwa muda mrefu bila mafanikio, huku uwanjani hapo kukiwa hakuna gari maalumu la wagonjwa.

Mwanaspoti lililokuwa uwanjani hapo, lilishuhudia kipa huyo akihudumiwa na watoa huduma ya kwanza kwa muda wa dakika karibu 10 kabla ya kubebwa mzegamzega kutolewa nje ili kuwahishwa Hospitalini.

Ilichukua tena kama dakika 3-5 kabla ya gari la wagonjwa kuletwa na kumbeba mchezaji huyo kumkimbiza hospitalini kwa matibabu zaidi.

Kama lolote baya ambalo lingempata kipa huyo, TFF ilikuwa ikiingia tena lawamani kwa uzembe wa kushindwa kuharakisha matibabu ya Rostand hospitalini, kwa sababu ilichukua muda mrefu kutibiwa na bado hakukuwa na gari karibu ili kumbeba.

Ilishawahi kutokea pia tukio kama hilo misimu michache iliyopita kwenye Uwanja wa Chamazi, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu, ambapo aliyekuwa kipa wa JKT Ruvu, Jackson Chove nusura apoteze maisha baada ya kukosekana kwa gari la kubebea wagonjwa na badala yake kubebwa kwenye gari aina ya Noah kuwahishwa hospitalini.

Haya ni matukio yanayojitokeza mara kwa mara viwanjani, lakini wasimamizi wa soka ni kama hawashtuki, hawajali wala kuthamini usalama wa wachezaji na mashabiki wanaoliingizia fedha shirikisho hilo kwa kwenda viwanjani kutazama mechi.

Imefika wakati wa viongozi wa shirikisho hilo na hata wamiliki wa viwanja hivyo kujaribu kutengeneza mazingira mazuri ya kulinda usalama wa wachezaji na wadau wengine wanaokwenda viwanjani kwa kuwepo kwa huduma muhimu za kiafya sambamba na gari maalumu la wagonjwa.

Tusisubiri yatokee maafa kama yaliyomkuta Ismail kule Kaitaba, hata kama wakati mwingine ni gharama kubwa kuweka huduma hiyo, lakini kupi bora kati ya kufanya ubahili na kulitia aibu soka letu kwa mambo yanayoepukika.

Wachezaji na mashabiki wanaokwenda uwanjani ndio wanaolifanya soka letu kuwa lilipo, kama wanakosekana watu hao, hakutakuwa na TFF, ndiyo maana tunalikumbusha shirikisho hilo liwe makini katika suala hilo la msingi.

Ni aibu uwanja mkubwa kama wa Uhuru unashindwa kuwa na gari la wagonjwa ndani ya uwanja ili ikitokea dharura lisaidie kwa haraka, badala ya kuruhusu mchezaji abebwe kwa machela kwa umbali wa zaidi ya mita 50 kulifuata gari nje ya uwanja katika hali ya maumivu ya majeraha ya uwanjani.

Imefika wakati viongozi wa soka na hata wamiliki wa viwanja kujifunza kutokana na makosa, pia kuiga namna wenzao wa mataifa ya nje walivyo makini katika suala zima la usalama wa wachezaji na watazamaji viwanjani.

Hata kama ni kweli kifo hakizuiliki, lakini maafa ya kizembe yanazuilika kwa kuwepo kwa umakini katika suala zima la kuchukuliwa tahadhari viwanjani kabla ya kutoa maafa.