TFF iachane na usiri ratiba ya Kombe la FA

Muktasari:

  • Hakuna anayejua imekuwaje kwa Shirikisho la Soka nchini (TFF) kutoa ratiba ghafla namna hiyo kabla ya timu kushuka uwanjani, wakati tayari walikuwa wakifahamu wiki ya kuanzia Januari 20-25 kutakuwa na mechi za michuano hiyo.

RAUNDI ya tano ya michuano ya Kombe la FA, inaendelea ambapo hatua hiyo itakamilisha mechi zao keshokutwa Jumatano.

Mechi hizo za raundi hiyo ambayo imezishirikisha timu za Ligi Kuu Bara na zile zilizopenya kwenye raundi ya nne, zilianza Jumatano.

Ratiba ya mechi hizo ilitolewa Alhamisi iliyopita, siku moja tu kabla ya kuanza kwake, kitu ambacho sio tu kimeshangaza wengi, lakini kimezipa mtihani mkubwa timu za madaraja ya chini zilizopangwa kuumana na timu za Ligi Kuu.

Hakuna anayejua imekuwaje kwa Shirikisho la Soka nchini (TFF) kutoa ratiba ghafla namna hiyo kabla ya timu kushuka uwanjani, wakati tayari walikuwa wakifahamu wiki ya kuanzia Januari 20-25 kutakuwa na mechi za michuano hiyo.

Halafu, Kombe la FA ni michuano mikubwa kwa sasa ikiwa ndio inayotoa moja ya wawakilishi wa michuano ya kimataifa kutoka Tanzania, hivyo ni lazima ichezwe kulingana na hadhi yake na hata bingwa akipatikana kusiwepo na manung’uniko.

Wakati uendeshaji wa kubabaishaji ulivyofanyika katika michuano ya msimu uliopita hasa kwa ratiba za kushtukia na kuzibeba timu fulani kucheza  mechi mfululizo nyumbani, tuliamini ni sababu ya ugeni wa michuano hiyo iliyofufuliwa upya.

Kombe la FA lilizimika kwa miaka zaidi ya 10 tangu ilipochezwa kwa mara ya mwisho mwaka 2002, hivyo msimu uliopita iliporejeshwa tena, tulijua TFF ilikuwa haijajipanga vema ndio maana ilikuwa ikifanya mambo yake kwa kulipua.

Hata hivyo, msimu huu ni wa pili na kila mdau wa soka alikuwa akifahamu kuwa michuano hiyo ipo na itaendeshwa kulingana na hadhi yake, lakini hali sivyo ilivyo, TFF bado inaishi katika utamaduni iliyozoea kwa kukurupuka kila mara.

Haiwezekani ratiba ya mechi itolewa Alhamisi mechi zianze kuchezwa Jumamosi timu zinapata muda gani wa kujiandaa dhidi ya wapinzani wao kama sio kuweka mazingira mazuri kwa timu za Ligi Kuu kuendelea kutawala michuano hiyo.

Haikushangaza sana kuona Ashanti United ambayo kwa kawaida huisumbua Yanga, ikikubali kipigo cha mabao 4-1, huku Alliance FC ikitota kwa Mbao FC, ni kwa sababu hata akili za wachezaji wa timu hizo hazikuwa zimeandaliwa kuvaana na wachezaji wa timu za Ligi Kuu.

Ndiyo maana tunasema wazi kuwa, TFF inapaswa kubadilika na kuandaa ratiba ya uwazi na inayotoa muda timu kufanya maandalizi ya kukabiliana na wapinzani wao katika michuano hiyo badala ya kuzishtukiza timu kama michuano imezuka.

Kwa mfano tayari timu zilizosonga mbele zimeanza kufahamika, inapaswa TFF mara ya kukamilishwa kwa mechi za raundi hiyo ya tano, iitishe droo ya wazi kisha kufahamika nani anacheza na nani kwa mechi zitakazofuata ambazo kwa mujibu wa kalenda inavyoonyesha ni kwamba zitachezwa tena Februari 25-26.

Kutolewa mapema kwa ratiba kwa timu kufahamu wapinzani wao, hutoa fursa kwa timu na wachezaji kuandaliwa kiakili kwa vile michuano hii inahusisha timu za madaraja tofauti, inashtusha kwa mchezaji wa timu ya Ligi ya Mabingwa RCL kupangwa na timu ya Ligi Kuu ndani ya siku moja ama mbili kisha ikapata matokeo mazuri. Ni ngumu na ndiyo maana inazifanya timu za Ligi Kuu kuonekana wababe kwa washiriki wengine, wakati michuano ya Kombe la FA kwa miaka ya nyuma hata timu ya mchangani isiyocheza ligi yoyote ilikuwa na uwezo wa kuisimamisha timu ya Ligi Kuu. TFF kama inapenda kuiga mambo ya Ligi Kuu za Ulaya, vipi inashindwa kuiga ratiba na uendeshaji wa soka kisasa?