TFF, Bodi ya Ligi ikomalie waamuzi waharibifu

Muktasari:

  • Simba ipo kileleni mpaka sasa ikiongoza na pointi zao 20, ikifuatiwa kwa karibuni na Stand United yenye pointi 19, huku Kagera Sugar ikikamata nafasi ya tatu mbele ya Yanga na Mtibwa Sugar.

LIGI Kuu Bara inashika kasi na kunoga kwelikweli ikiwafanya mashabiki wa soka kuifuatilia kwa makini kutokana na ushindani uliopo. Ikiwa imeingia raundi ya tisa, ushindani wa ligi hiyo umekuwa ukiongezeka kila uchao, huku ikiwapa ugumu mashabiki kutabiri matokeo. Hakuna timu yenye uhakika wa matokeo mpaka pale dakika 90 kinapolia kipyenga cha kumaliza pambano.

Utamu wa ligi hiyo umeongezeka maradufu kutokana na namna baadhi ya klabu zilivyojipanga na kufanya maajabu tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita ama ligi ilipoanza Agosti 20 mwaka huu. Simba ipo kileleni mpaka sasa ikiongoza na pointi zao 20, ikifuatiwa kwa karibuni na Stand United yenye pointi 19, huku Kagera Sugar ikikamata nafasi ya tatu mbele ya Yanga na Mtibwa Sugar.Kagera inafahamika msimu uliopita ilivyoponea chupuchupu kushuka daraja, lakini msimu huu wamekuja kivingine na kufanya iwe tishio.

Mbao walioanza kinyonge ligi na kutabiriwa ingekuwa miongoni mwa klabu tatu za kushuka daraja, imeanza makeke, huku Chama la Wana, Stand United ikiwaduwaza wengi kwa kufanya vizuri licha ya kukimbiwa na wadhamini. Azam na Prisons zilizofanya vema msimu uliopita safari hii zinayumba na kuacha maswali mengi juu ya mustakabali wao mwishoni mwa msimu, japo muda bado upo wa klabu hizo na nyingine kurekebisha mambo yao. Kifupi ni kwamba ligi ya msimu huu imekuwa tamu na kufuatiliwa kwa karibu na mashabiki tofauti hata na msimu uliopita, ukitaka kujua ukweli wa jambo hili sikiliza mazungumzo na mijadala vijiweni katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam. Ukiwa ndani ya daladala stori ni hizo hizo za ligi kuu na namna baadhi ya nyota wa klabu kubwa wanavyofanya yao na utani wa Simba na Yanga ni kama umefufuliwa upya. Mashabiki wanatania mitaani na kutambia nyota wao, kitu ambacho kinaongeza msisimko wa ligi hiyo. Kizuri zaidi ni kwamba mechi nyingi za ligi msimu huu zimekuwa zikirushwa mubashara na kituo cha Azam na kufanya hata wasioenda uwanjani kupata burudani na cha kuzungumza kwenye vijiwe mitaani.

Hata hivyo wakati ligi ikishika kasi na kuzidi kuwa na msisimko, tayari kumekuwa na malalamiko ya kila mara dhidi ya waamuzi wanaochezesha ligi hiyo wakidaiwa kuvurunda na kusababisha matokeo kuwa sivyo ndivyo.

Malalamiko hayo yamekuwa yakiongezeka kadri ligi inavyosonga mbele kitu ambacho Mwanaspoti kinadhani kuna haja ya wasimamizi wa ligi hiyo kwa maana ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB) kutoziba masikio na badala ya kufanyia kazi kelele hizo ili kurekebisha tatizo.

Mwanaspoti linafahamu kuwa TFF na TPLB inayasikia malalamiko hayo na baadhi imeanza kuyachukulia hatua kama Kamati ya Saa 72 ilipokutana na kutoa maamuzi kwa baadhi ya mambo ikiwamo pambano la watani Simba na Yanga, lakini hiyo haitoshi. Kunahitajika juhudi zaidi kufanyika katika kuhakikisha waamuzi wanaolalamikiwa wanafuatiliwa kwa kina kisha kuchukuliwa hatua ili kusaidia kuwafanya wengine kuogopa kutuharibia ligi yetu. Ni kweli yapo makosa mengine yanayofanywa na waamuzi hutokea kibinadamu, lakini bado inahitajika kuyadhibiti yasijirejee mara kwa mara kwani yanaharibu msisimko wa ligi.Mwanaspoti halina ni ya kumnyooshea mtu kidole ama kuwa na ushahidi juu ya madudu yanayofanywa na waamuzi, lakini kwa kuwa wanaopiga kelele ni klabu na kila mmoja anazisikia ni wajibu wa kusikilizwa. Hata kama kelele nyingine zinazopigwa na klabu kupitia makocha na mabosi wa ni njia za kujihami na kuficha udhaifu wa timu zao nyuma ya migongo ya waamuzi, lakini kuna makosa yanayoonekana wazi na mashabiki. Hivyo ni wajibu kwa mamlaka hizo zikishirikiana na Kamati ya Waamuzi kuhakikisha marefa wanaovurunda wanaondolewa mapema ili nafasi zao kubebwa na waamuzi makini watakaoinogesha zaidi ligi hiyo. Kama kuna la kujifunza kwa mamlaka hizo ni makosa machache yaliyofanywa na waamuzi wa mechi ya Simba na Yanga na jinsi vurugu zilizotokea.