Stars inacheza, wala hakuna anayejali

Muktasari:

Stars kwa sasa haina mvuto, licha ya mazoezi wiki nzima hakuna aliyetaka kuifuatilia sana. Hata Wanahabari wengi wanaokwenda mazoezini wanamfuata Mbwana Samatta tu.

TAIFA Stars leo Jumamosi itacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Botswana pale kwa Mchina, yaani Uwanja wa Taifa, hakuna anayejali.

Stars kwa sasa haina mvuto, licha ya mazoezi wiki nzima hakuna aliyetaka kuifuatilia sana. Hata Wanahabari wengi wanaokwenda mazoezini wanamfuata Mbwana Samatta tu.

Stars imekuwa kama yatima kwa kipindi cha miaka hii miwili iliyopita kwani hata wachezaji wanaoitwa, wanaona ni kawaida tu.

Miaka minne iliyopita, Stars ilipendwa asikwambie mtu. Ilipocheza wengi walijitokeza kuipa sapoti.

Kumbuka michezo dhidi ya Morocco na Ivory Coast mwaka 2013, Taifa palitapika. Karibu kila mdau wa soka nchini alitamani kuiona. Lakini sasa mambo yamebadilika.

Kuna tatizo limetokea mahali. Haiwezekani, kuna mtu amekosea mahali. Watu wamekosea mahali.

Tatizo la kwanza la Stars ni Jamal Malinzi. Kigogo huyu tangu achukue madaraka katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mwaka 2013 mambo yamekuwa ndivyo sivyo. Malinzi ameiua Stars, haina mashiko tena.

Alianza kwa kumfukuza kocha, Kim Paulsen. Akamleta Mart Noij ambaye hata hivyo hakuwa mtu anayejali sana.

Stars yake haikuitwa kutokana na ushindani wa wachezaji. Aliowaita mara ya kwanza ndiyo hao hao waliopata nafasi mara ya pili na ya tatu. Wachezaji wakaanza kuona hakuna ufahari tena wa kucheza Stars kama anayekaa benchi msimu mzima bado anaitwa. Ajabu.

Stars ikaanza kufungwa. Ilifungwa na Zimbabwe, Uganda, Lesotho, Swaziland, Madagascar na timu nyingine za ajabu. Noij hakujali. Malinzi hakujali pia.

Matokeo yake basi la wachezaji wa Stars likaanza kupigwa mawe. Malinzi aliendelea kumkumbatia Noij mpaka Wanzanzibari walipomkomalia baada ya kufungwa na Uganda 3-0 pale Amaan, Zanzibar.

Ikaendelea kupoteza mvuto kwa kufungwa 7-0 na Algeria. Haikuwahi kutokea kufungwa mabao mengi kiasi hicho. Hata hivyo haya yote yalichagizwa na uwajibikaji mbovu wa Malinzi pale TFF.

Mwisho wa siku Stars leo ipo chini ya kocha ambaye hajawahi kushinda ubingwa wowote wa maana katika soka la Tanzania. Mafanikio makubwa ya Salum Mayanga ni kuziwezesha timu kumaliza nafasi ya nne na ya tatu Ligi Kuu. Huyu ndiye kocha wa Taifa sasa. Inachekesha sana.

Matokeo yake Stars inacheza na hakuna anayejali.