NINACHOKIAMINI : Simba ya URA ndio yenyewe, ile ya AFC ilitudanganya

Muktasari:

Ukizunguka katika kila kijiji, bila shaka utakutana na watu wanaoheshimiwa kwa sababu ya mali na utajiri wao.

UNAWEZA kudhani una mafanikio makubwa katika jamii inayokuzunguka, lakini jamii hiyo ikawa inakudanganya.

Ukizunguka katika kila kijiji, bila shaka utakutana na watu wanaoheshimiwa kwa sababu ya mali na utajiri wao.

Imekuwa kama fasheni, kila kijiji huwa kina mtu au watu wanaoheshimika kwa sababu ya mali na utajiri walionao.

Lakini matajiri hao wa vijijini ukiwaleta Dar es Salaam, wanaweza kuwa watu wa kawaida sana. Wanaweza kuonekana hawana kitu kabisa.

Ni hivyohivyo hata katika shule mbalimbali, kila darasa huwa na mwanafunzi anayeonekana kuwa na akili kuliko wengine. Kila mtihani huwa anaongoza kwa kuwa wa kwanza.

Lakini ukifanyika mtihani wa wilaya, utashangaa kuona mwanafunzi huyo amekamata nafasi ya 50 kwa sababu amekutana na wenye akili zaidi yake.

Hapo ndipo tunapaswa tupafikie katika maisha ya kila siku. Hupaswi kujipima kwa kuangalia mazingira yanayokuzunguka tu, kufanya hivyo ni kujidanganya na unaweza usifikie malengo makubwa.

Ukitaka kufanikiwa siku zote ujipime kwa kuangalia picha kubwa zaidi, ujipime kwa kuitazama jamii kubwa zaidi kuliko kuangalia watu wachache wanaokuzunguka.

Hata katika soka letu ni hivyohivyo, klabu zetu zinatakiwa kufanya mambo makubwa zaidi katika soka kwa kuangalia mbali ili kuweza kuweza kujenga timu.

Uliona jinsi Simba walivyotaka kujidanganya kwa AFC Leopards ya Kenya katika mechi ya Simba Day iliyochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam Agosti 8, mwaka huu.

Katika mchezo huo ambao Simba ilishinda mabao 4-0, ungedhani vijana wa Msimbazi wangetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa asilimia 100.

Kama uliufuatilia mchezo huo, Simba ilikuwa nzuri kila idara, wachezaji walicheza kwa kuelewana vizuri, walikuwa na nguvu, kasi, mnyumbuliko na timu ilicheza kwa pamoja zaidi. Ilikuwa timu zaidi.

Ungeweza kutoa majibu ya haraka haraka kuwa safari hii, Simba ina uhakika wa kutwaa ubingwa wa Bara bila kipingamizi.

Hilo lingeweza kuwa kosa kubwa kudhani hivyo, kwa sababu Simba halisi tuliiona katika mechi dhidi ya URA juzi Jumapili iliyopita.

Katika mechi hiyo ya sare ya 1-1, URA ilionekana timu ya Ligi Kuu wakati Simba ilionekana kama timu ambayo bado inaundwa na haijui inachokifanya. Na huo ndio ukweli wenyewe hata kama baadhi ya watu wataukataa.

Nilitamani URA wageuzwe wawe Simba na Simba wawe URA lakini haiwezekani kwa sababu watoza ushuru hao wa Uganda wanatakiwa kurudi kwao Kampala kuendelea na maandalizi ya mechi za Ligi Kuu Uganda.

Ili mashabiki wa Simba wasije kupata magonjwa ya moyo, presha na msongo wa mawazo, wanapaswa kujua kuwa Simba halisi ni ile iliyocheza na URA na si ile ambayo ilicheza na AFC Leopards. Ile haikuwa timu halisi kwa kuwa ilikuwa imecheza na timu unayoweza kusema kwamba haipo hata katika ligi daraja la kwanza.

Bado kuna mambo mengi ambayo benchi la ufundi la Simba linabidi kuyafanyia kazi, mojawapo likiwa ni kuwapa mazoezi ya stamina wachezaji wao, lakini pia kuwaongezea maarifa ya mchezo.Tatizo kubwa ambalo nimeliona ni nidhamu, haiwezekani wachezaji waruhusiwe kwenda majumbani kwao kwa muda wa wiki moja tu, wamebadilika na kuwa wachezaji wa mchangani kwa sababu tu walijiachia na kusahau kufanya mazoezi ya kujiweka fiti.

Pamoja na kwamba katika mchezo huo, Simba ilisawazisha bao la URA lakini utofauti ulionekana kulikuwa na timu na nyingine ilikuwa ni mfano wa timu. Mabeki wa URA walionekana kujua kazi yao tofauti na wale wa AFC Leopards kwa kuweza kuwadhibiti vilivyo washambuliaji walionekana kuwa hatari wiki moja kabla ya mchezo huo. Hakukuwa na Laudit Mavugo, Shiza Kichuya, Ibrahim Ajib wala Muivorycoast, Blagnon Frederic walioweza kufurukuta.