NJIA NYEUPE : Simba iamue kumpa MO timu, la imshawishi kuidhamini

Muktasari:

Manji licha ya kuwa ni Mwenyekiti wa klabu hiyo, lakini sasa kampuni yake ya Quality Group ndio mdhamini mkuu wa Yanga baada ya kuiondoa kwenye nafasi hiyo Kampuni ya Bia ya Tanzania (TBL) iliyokuwa inadhamini klabu hiyo kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro.

YANGA ya Dar es Salaam licha ya kufanya vizuri kwenye michuano mbalimbali inayoshiriki msimu huu, lakini imeamua kumkabidhi timu yao mfanyabiashara maarufu nchini, Yussuf Manji.

Manji licha ya kuwa ni Mwenyekiti wa klabu hiyo, lakini sasa kampuni yake ya Quality Group ndio mdhamini mkuu wa Yanga baada ya kuiondoa kwenye nafasi hiyo Kampuni ya Bia ya Tanzania (TBL) iliyokuwa inadhamini klabu hiyo kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro.

Hatua hiyo inaiweka Simba ya Dar es Salaam katika njia panda kwani, huenda TBL ikakataa kuwa mdhamini mwenza wa Yanga na pia ikakataa kuendelea kuidhamini Simba kwa sababu ya maslahi ya kibiashara.

TBL kupitia bia ya Kilimanjaro ilikuwa inazidhamini klabu zote hizo mbili zenye utani wa jadi kwa miaka mingi na maskani yake Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Kujitoa kwenye udhamini wa TBL kwa Yanga kunaipa mtihani Simba kuwa na kazi ya kutafuta mdhamini mpya kwani, kuna uwezekano mkubwa TBL ikaacha kuzidhamini timu zote mbili.

Katika mazingira hayo Simba itakuwa na nafasi ya kumrudia mdhamini wake wa miaka ya nyuma Kampuni ya Mohammed Enterprises [MeTL] inayomilikiwa na bilionea kijana, Mohammed Dewji [MO].

Simba watakuwa katika mtihani wa kuamua iwapo wampe MO moja kwa moja timu yao au wampe kwa njia ya udhamini kupitia moja ya bidhaa zake anazozalisha nchini.

Iwapo watakuwa na uamuzi wa kumpa timu moja kwa moja mkutano mkuu wa wanachama uliopangwa kufanyika Julai 10, mwaka huu, utakuwa na nafasi nzuri ya kuamua suala hilo ambalo kwa sasa ni nyeti katika klabu ya Simba.

Kwa sasa wanachama wa Simba wamegawanyika makundi, wapo ambao wanaunga mkono klabu yao ichukuliwe na MO na kuna wale wanaopinga na kutaka mfumo wa sasa wa kuwa chini ya wanachama uendelee.

Lakini kwa vyovyote vile Simba italazimika kuchukua moja ya hatua hizo ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuiendesha klabu hiyo ambayo gharama za kuiendesha timu ya mpira zinazidi kupanda siku hadi siku kulingana na mahitaji.

Vinginevyo uongozi wa Simba utalazimika kujipanga na kutafuta wadhamini wengine kazi ambayo inaweza kuwa ngumu zaidi kuliko kumshawishi MO kudhamini timu yao.

MO, ambaye ni mwanasimba yuko katika nafasi nzuri na inaelekea ana utashi wa kuichukua Simba moja kwa moja au kuidhamini kwani, ameshawahi kufanya hivyo miaka ya nyuma na kulikuwa na mafanikio makubwa.

Ikiwa chini ya udhamini wa MO mwaka 2003 Simba ilifanya vizuri katika michuano ya kimataifa na kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika historia yake na kuwa klabu ya pili nchini kufanya hivyo baada ya Yanga kuingia hatua hiyo mwaka 1998.

Jitihada za Simba inayoendelea kukisuka kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao kwa kupata Katibu Mkuu mpya wa klabu, Patrick Kahamele na kocha mpya, Joseph Omog kutoka Cameroon aliyekuwa anainoa Azam FC hazitazaa matunda iwapo hawatakuwa na udhamini wa uhakika.

Itakuwa vigumu kuendesha timu kwa mafanikio kwa kutegemea udhamini wa Vodacom inayodhamini Ligi Kuu Bara na Azam TV inayodhamini kupitia haki za matangazo ya ligi hiyo.

Udhamini wa makampuni hayo mawili unasaidia, lakini hautoshelezi kukabiliana na gharama ya kuendesha timu ambazo mbali na mishahara ya timu, kuna kambi na za kukodi viwanja vya mazoezi kuna gharama nyingine kadhaa.

Kwa hiyo Simba hata kama itafanikiwa kukisuka vizuri kiasi gani kikosi chake kwa kufanya usajili wa maana kwa kuleta wachezaji hodari, lakini kama haitakuwa na fedha ya kuihudumia vizuri timu yake itakuwa kazi bure.

Huu ni wakati muafaka kwa Simba kumkabidhi MO timu yake au kumpa udhamini ili Simba ipate fedha ambazo zitasaidia kuitoa timu hiyo mchangani.

Uongozi unapaswa kulifikiria hilo kwa umakini na kufanya uamuzi sahihi kabla ya kuanza kwa msimu mpya ili kuponya maumivu ya wanachama wake wanaosubiri matokeo mazuri ikiwa ubingwa kwa miaka zaidi ya mitatu sasa.

Masoud Sanani ni Mwandishi wa Habari Mwandamizi amewahi kufanya kazi Televisheni Zanzibar,Uhuru na Mzalendo,Bussiness Times[Mhariri mwanzilishi wa Spoti Starehe] na Mwananchi.

Alikuwa Mkurugenzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania [TEF].Anapatikana kwa email [email protected] simu 0712-020020