NINACHOKIAMINI : Simba, Yanga, Azam bado safari ndefu kimataifa

Muktasari:

Kuna mjadala gani utapita usisikie maoni ya Watanzania au kuna jambo gani litatokea usisikie maoni ya Wabongo. Wanazugumza sana utadhani wanajua, kumbe wengi wanababaisha tu, hakuna kitu.

WATANZANIA wanajua kila kitu, wanaweza kujadili kila kitu. Wanazungumza sana kuliko kutenda, wanaamini wanajua, lakini katika vitendo huwezi kuwaona, hubaki nyuma wakishangaa.

Kuna mjadala gani utapita usisikie maoni ya Watanzania au kuna jambo gani litatokea usisikie maoni ya Wabongo. Wanazugumza sana utadhani wanajua, kumbe wengi wanababaisha tu, hakuna kitu.

Mtanzania anaweza kukupa habari za Jiji la New York ukadhani amewahi kufika, kumbe hajawahi hata kufikiria kufika huko, lakini jinsi anavyokusimulia utadhani ni mzaliwa wa huko.

Ukitokea mjadala wa siasa, utasikia jinsi watu wanavyojadili kwa kuponda upande fulani na kusifu upande mwingine na usipokuwa makini unaweza kuamini wanachozungumza. Kuwa makini sana.

Ikifika katika muziki, utasikia wanavyozungumza. Utadhani kila Mtanzania amewahi kwenda chuo cha muziki, utasikia fulani anajua kuimba kuliko mwingine. Halafu atatoa sababu anazozijua kutetea hoja yake nyepesi.

Ukitaka ujue kuwa Watanzania wanajua kila kitu ifike mjadala wa mambo ya soka, utawapenda. Utawapenda kwa sababu wanajua mpira wa miguu kuliko makocha wa klabu husika. Wanajua kuuelezea mpira kuliko Sir Alex Ferguson au Arsene Wenger. Utashangaa wanavyopiga kelele wakati Marouane Fellaini anapasha misuli akijiandaa kuingia kuchukua nafasi ya Michael Carrick.

Watapiga kelele na matusi yote yataenda kwa Kocha Jose Mourinho kwa kufanya mabadiliko hayo.

Watanzania bila kujali timu wanayoishangilia, wanadhani wanamjua Fellaini kuliko Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho. Hawamtaki Fellaini apangwe mechi yoyote.

Mashabiki wa Arsenal, Chelsea na Liverpool watashangilia mabadiliko hayo kwa sababu wanaamini kuwa mchezaji anayeingia ni mzigo. Kwa jumla hata mashabiki hawa wanadhani wanamjua mchezaji huyo kuliko Mourinho.

Mashabiki wa soka hasa Watanzania wanashindwa kujua kuwa Kocha Mourinho anawajua vizuri wachezaji wake kuliko mtu mwingine yeyote duniani.

Mourinho anakuwa nao muda mwingi wachezaji hao, anakuwa nao asubuhi na jioni mazoezini, anakuwa nayo wakati wa chakula cha mchana na wakati mwingine.

Mourinho anawajua wachezaji wake, umuhimu wa kila mmoja, udhaifu wa kila mmoja, hivyo anavyopanga kikosi chake huwa anazingatia mambo mengi, lakini mashabiki huwa hawataki kuheshimu kazi ya kocha, wanadhani anapanga tu kikosi ilimradi, wanasahau kuwa yeye ni mtaalamu aliyesomea ukocha.

Lakini mashabiki hawataki kukubali hilo, wanataka wao ndio wapange kikosi, wafanye mabadiliko ya kikosi na kama hilo linashindikana, huwa wanashinikiza kocha afukuzwe.

Makocha wetu wa ndani ndio kabisa wamekosa kuheshimiwa, wanafanya kazi katika presha kubwa, hawana uhuru. Wanafanya kazi kwa presha kutoka kwa mashabiki na mbaya zaidi kwao presha za viongozi wa klabu.

Tunaweza kuwa tunawalaumu makocha, lakini viwango vya wachezaji vipo chini, bado hawajitambui.

Nilikuwa natazama michuano ya Kombe la Mapinduzi, nikafanya suluhisho kuwa bado klabu zetu haziwezi kupambana mechi kubwa za kimataifa.

Nimeiangalia Simba nikawa najiuliza hivi wachezaji wanafanya mazoezi ya kupiga mashuti langoni? Nikashindwa kupata majibu kwa sababu wachezaji wao hawawezi kupiga mashuti ya maana langoni mwa adui yao.

Licha ya kupiga vijishuti vya mtoto mchanga, wachezaji wa Simba walikuwa wakianguka hovyo kana kwamba walikuwa wanaingia uwanjani wakiwa na njaa.

Wachezaji wa Yanga licha ya kuwa na uzoefu wa mechi za Caf wameshindwa kuonyesha hilo katika michuano ya Mapinduzi.

Utawapenda wakicheza na timu ndogo, lakini wanapokutana na klabu kubwa utashangaa jinsi wanavyobabaika na kucheza kwa hofu kana kwamba hawana uzoefu wowote.

Azam FC licha ya uwezekaji mkubwa bado ni timu ya kawaida. Angalau wachezaji wao wanaonekana kujitambua na mashuti yao ya mbali wanaonyesha wanayafanyia mazoezi.

Wanatambua kuwa la muhimu kwao ni ushindi na ndio maana wanatafuta mabao kwa njia yoyote.

Nzuri zaidi kwao wanabadilika kutokana na mchezo wanaocheza. Walivyocheza na Yanga ni tofauti na walivyocheza na Simba.

Hata hivyo, ukiangalia kiwango cha timu hizo tatu kubwa nchini, bado napata wasiwasi kama tunaweza kuwa na wawakilishi wazuri kwenye mashindano ya Caf. Bado wachezaji hawajajitambua na kuweza kutoa ushindani. Siamini kama tunaweza.