Serikali ikiamua upangaji matokeo utaisha

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba wakati akikabidhi tuzo mbalimbali za Ligi Kuu ya Vodacom Bara (VPL) msimu wa 2015/16

KAMA kuna tatizo linalotajwa kuwa sababu ya Tanzania kutopiga hatua katika soka basi tatizo hilo ni upangaji matokeo.

Ni kweli yapo matatizo mengi lakini hili la kupanga matokeo kamwe haliwezi kupuuzwa, ni tatizo ambalo limekuwa likizungumzwa mara kwa mara. Hata hivyo bado nia thabiti ya kukabiliana na tatizo hili haipo, ni watu wachache mno ambao japo wamekuwa mstari wa mbele katika kulikomesha lakini juhudi za watu hao zimeshindwa kuzaa matunda.

Tatizo limeendelea kukuwa na hakuna mdau wa soka anayeweza kusimama na kusema kwamba Tanzania haina tatizo la upangaji matokeo.

Kwetu hii tunaiona ni hatua nzuri, ni aina mojawapo ya kulikubali tatizo kwani hata wale waliokuwa wakipinga siku za nyuma kwa sasa hawawezi kusimama na kupinga kuwapo kwa jambo hilo.

Ni hivi karibuni tu tumeshuhudia timu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zikifungana mabao 8-0 na 7-0 matokeo yaliyotoa dalili za kuwapo mchezo mchafu na jambo jingine la kufurahisha ni kwamba hatua zikachukuliwa kwa wahusika.

Katika hatua hizo zipo timu zilizoshushwa daraja na baadhi ya viongozi kufungiwa kujihusisha na soka wakiwamo waliofungiwa kwa vipindi virefu hadi baadhi ya wadau wakaanza kulalamikia adhabu kuwa kali. Juzi Jumapili Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba wakati akikabidhi tuzo mbalimbali za Ligi Kuu ya Vodacom Bara (VPL) msimu wa 2015/16 alizungumzia tatizo la upangaji matokeo.

Katika hotuba yake waziri huyo alikiri kwamba tatizo hilo ni kikwazo cha maendeleo ya soka na kusisitiza kwamba halipaswi kuvumiliwa hata kidogo.

Tungependa kuunga mkono kauli hiyo ya waziri lakini pia kuungana naye katika kukubali tatizo, kwani kauli aliyoitoa waziri inamaanisha kukubali kwamba tatizo la upangaji matokeo lipo katika soka la Tanzania.

Tunachosubiri sasa ni kuona namna waziri au serikali itakavyosimama kidete kukabiliana na tatizo hilo kwani tayari amekubali lipo na linakwamisha maendeleo ya soka.

Imani yetu ni kwamba kama serikali itakuwa na dhamira ya dhati ya kukomesha madudu haya kwenye soka ni lazima mafanikio yataonekana mara moja.Tumewahi kulizungumzia jambo hili na kubainisha kwamba kuna mtandao mpana unaosimamia matukio ya upangaji matokeo, mtandao ambao unawahusisha watu wenye fedha na ambao hutumia fedha zao kuhonga wachezaji au waamuzi.

Serikali inachotakiwa kufanya kwanza ni kuhakikisha mtandao huu unavunjwa haraka iwezekanavyo, kuuvunja mtandao huu itakuwa hatua nzuri ya kumaliza tatizo la upangaji matokeo.

Tunafahamu ukweli kwamba ushahidi wa matukio haya ni mgumu na upo uwezekano mkubwa wa kuwanasa wahusika wadogo wakati wakubwa wanaotoa fedha zao wakasalimika.

Kufanya hivyo kamwe hakuwezi kumaliza tatizo, ni lazima serikali idhamirie kuwanasa mapapa wanaotumia utajiri wao kukwamisha maendeleo ya soka vinginevyo itakuwa kazi bure.

Hata katika hili tukio la timu za FDL zilizofungana mabao 7-0 na 8-0 lazima kuna mkono wa watu wenye fedha ambao umefanya kazi, hao ndio watu wa kushughulikiwa.