Safari ya Olimpiki Tokyo sio mchezo, tujipange

Muktasari:

Kwa mfano iliyopita ya Rio De Jeneiro iliyofanyika Brazili mwaka jana jumla ya nchi 205 zilishiriki na kuhusisha wanamichezo 11,544 katika michezo mbalimbali. Pia, katika michezo hiyo ya mwaka 2016 kulikuwa na jumla ya michezo 28 na matukio 306 na yote yalifanyika ndani ya siku16 za mashindano hayo, jambo linalofanya michuano hiyo iwasisimue wengi.

MICHEZO ya Majira ya Joto ya Olimpiki ndio mashindano makubwa zaidi duniani kuliko mengine kutokana na nchi zinazoshiriki, idadi ya michezo inayoshindaniwa na hata idadi ya wanamichezo wenyewe.

Kwa mfano iliyopita ya Rio De Jeneiro iliyofanyika Brazili mwaka jana jumla ya nchi 205 zilishiriki na kuhusisha wanamichezo 11,544 katika michezo mbalimbali. Pia, katika michezo hiyo ya mwaka 2016 kulikuwa na jumla ya michezo 28 na matukio 306 na yote yalifanyika ndani ya siku16 za mashindano hayo, jambo linalofanya michuano hiyo iwasisimue wengi.

Katika michezo hiyo ya Olimpiki kuna ratiba ambayo hupelekea kila siku kuwe na michezo kwa takriban muda wote.

Michuano hii inayosimamiwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (OIC) imekuwa ni moja kati ya chombo kikubwa kilichosaidia nchi nyingi kupiga hatua ya maendeleo katika michezo mbalimbali kulingana na vipaumbele. Zipo nchi vipaumbele vyake ni riadha, kama ilivyo Kenya au Ethiopia na zipo nyingine vipaumbele vyake huwa ngumi, miereka, kuogelea, mpira wa vinyoya na nyingine huwa na kipaumbele cha mchezo wa soka.

Zipo nchi zilizoitumia Olimpiki kama nyenzo ya kukuza mchezo kipaumbele kwao na nyingine zilizoitumia michezo hiyo kukuza michezo mbalimbali kwa pamoja, ingawa nyingi ni zile ziliozendelea kama vile Marekani au Australia. Kwa mfano kwa mchezo wa soka kuna baadhi ya nchi ambazo zimewahi kuandaa programu za soka la vijana kupitia mashindano ya Olimpiki na kufanikiwa kuwa na timu imara za soka za taifa siku za mbele kwa kuwa soka katika michuano ya Olimpiki huchezwa na vijana wenye umri chini ya maika 23. Kila timu ikipewa nafasi tatu za kuongeza wachezaji waliozidi umri huo ili kuwapa uzoefu vijana hao. Ghana Iliwahi kuandaa timu ya vijana kwa ajili ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 1992 iliyofanyika jijini Barcelona nchini Hispania, timu hiyo iliandaliwa kwa miaka mitatu na ilichukua vijana wengi wakiwemo akina Yew Achempong, Sammy Adjei, Frank Amankwa, Odatey Nii Lamptey, Mohamed Gargo, Samuel Osei Kuffor na wengine wengi. Timu hiyo haikufanikiwa kutwaa medali ya dhahabu, lakini ilitwaa medali ya shaba baada ya kuwa washindi watatu katika michezo hiyo ya Olimpiki. Mafanikio ya timu hiyo hayakuishia hapo kwani baada ya mashindano hayo karibu wachezaji wote waliocheza katika kikosi hicho walipata timu za kulipwa barani Ulaya na wengi wao waliendelea na kuwa wachezaji wakubwa kama vile kina Kuffor aliyekipiga katika timu ya Bayern Munich ya Ujerumani.

Nchi ya Cameroon pia imewahi kunufaika na programu za soka la vijana kwa ajili ya michezo ya Olimpiki ambapo mwaka 2000 ilitwaa medali ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki ya Sydney, Australia. Kwenye timu yao ya Olimpiki ya wakati huo walikuwepo chipukizi kama kina Samuel Eto’o, Patrick Mboma, Pierre Wome na wengine wengi ambao baadaye baada ya kutwaa medali ya dhahabu mwaka huo, walisambaa katika timu mbalimbali za Ulaya.

Baadaye wakawa wachezaji wakubwa kwenye ligi za Ulaya, kwa mfano wa nchi za Amerika ya Kusini ni Argentina iliyoshiriki na kutwaa medali ya dhahabu mwaka 2008 katika Olimpiki ya Beijing, China ambayo ilikuwa na vijana wengi kama vile akina Pablo Zabaleta, Fernando Gago, Juan Roman Riquelme, Angel Di Maria, Sergio Aguero, Lionel Messi, Javier Mascherano ambao wote baadaye wamekuja kuwa wachezaji wakubwa nchini mwao na duniani kwa jumla.

Bahati mbaya nafasi zilizopo kwa nchi za Afrika huwa ni tatu katika timu 16 zinazotakiwa kushiriki katika michezo hiyo ya Olimpiki, hivyo uchache huo husababisha nchi nyingi za Afrika kuona mashindano ya soka katika Olimpiki ni migumu, hivyo kuamua kutoshiriki katika hatua ya awali.

Miongoni mwa nchi hizo ni pamoja na Tanzania ambao kwa miaka yote tumekuwa tukishiriki mashindano ya Olimpiki katika michezo mingine tu kama vile riadha, kuogelea, judo na kadhalika, huku soka tukilitupa mkono.

Ingawa tumewahi kupata medali za dhahabu katika michezo ya Olimpiki miaka ya nyuma, lakini kwa miaka ya hivi karibuni hata katika michezo hiyo pia tumekuwa tukishiriki bila tija na mara ya mwisho ni mwaka jana 2016 katika Olimpiki ya Rio ambapo pia wanamichezo wetu waliondoka bila medali yoyote.

Uamuzi wa kuandaa timu ya soka kwa ajili ya kusaka nafasi ya kushiriki katika michezo ya Olimipiki ya mwaka 2020 ni uamuzi mzuri na unaotakiwa kuungwa mkono na wadau wote hasa serikali.

Kwa sababu licha ya kuongeza kwa idadi ya michezo ambayo tutashiriki mpango kama huu umekuwa unatumiwa na mataifa mengi ya Afrika Magharibi na kufanikiwa kusogeza mbele maendeleo ya mchezo wa soka na kuuza wachezaji wengi nje ya nchi. Kwa leo naomba kuishia hapo huku nikisubiri mrejesho kutoka kwenu!