STRAIKA WA MWANASPOTI : Ryan Giggs kaacha simanzi Man United

Muktasari:

Kuondoka kwake kumetokana na ujio wa Kocha Jose Mourinho ndani ya klabu hiyo ambaye binafsi hamkubali asilan.

HATIMAYE mkongwe wa Manchester United, Ryan Giggs ameamua kundoka klabuni hapo.

Kuondoka kwake kumetokana na ujio wa Kocha Jose Mourinho ndani ya klabu hiyo ambaye binafsi hamkubali asilan.

Kuna sababu nyingi ambazo zinamfanya aondoke, ila kwangu sababu kubwa naiona ni kwa vile hakukabidhiwa mikoba ya klabu hiyo baada ya Kocha Luis Van Gaal kutimuliwa klabuni hapo kutokana na matokeo mabaya ya msimu uliopita.

Kumbuka Giggs kipindi Sir Alex Ferguson akiondoka alikuwa tayari ashaanza ukocha. David Moyes alipokuja klabuni hapo Giggs alikuwa msaidizi wake. Baadaye nye aliondokana nafsi yake kuchukuliwa na Van Gaal aliyembakisha kama msaidizi wake.

Hivyo kwa misimu minne tangu Ferguson aondoke Giggs amekuwa msaidizi wa makocha wote wanaoingia na kutoka Old Trafford. Safari hii aliona ni vigumu kwake kuweza kuendelea kufanya kazi kama kocha msaidizi chini ya Jose Mourinho.

Giggs alijiunga na Manchester United akiwa kinda kabisa. Tangu muda huo hajawahi kucheza klabu nyingine yoyote ile duniani.

Maisha yake yote yalikuwa katika klabu hiyo tu. Giggs mwenye umri ya miaka 42 amekuwa Man United kwa zaidi ya misimu 29. Ni uchungu kuondoka kwake lakini ninachofahamu maamuzi yake yanatokana na ujio wa Mourinho.

Jose Mourinho ninavyomfahamu ni kocha ambaye anapoteuliwa katika klabu yoyote ile hutua na kikosi chake cha kufanya kazi kuanzia kwa madaktari hadi wasaidizi wake.

Kwa hivyo itakuwa ni vigumu mno kwa Ryan Giggs kubakia katika klabu hiyo. Kwake Mourinho anaona kutakuwa na kutoelewana na Giggs kikazi ndipo akaona kuondoka kwa Giggs kutampa ama kutaifanya kazi yake kuwa rahisi zaidi. Ishu ya kulaumiana haitakuwepo iwapo atakuja na kikosi chake. Ni kawaida kote duniani makocha wanaoteuliwa katika klabu kubwa kila kocha kuja na kikosi chake cha makocha wasaidizi.

Kila kocha huja na anabadilisha benchi lake la ufundi. Upande wa Ryan Giggs anaona muda umewadia wa yeye angalau kutafuta klabu ambayo itampa nafasi ya kuwa Kocha Mkuu.

Kwangu ni vyema aondoke akapate ujuzi kwingine na iwapo atafaulu kule ataenda basi sina budi akirudi Old Trafford kama kocha mkuu na sio msaidizi tena.

Kazi ambayo ameifanyia Man United tangu utotoni ni kubwa, hakuna taji hii dunia hajawahi kulishinda akiwa ndani ya kikosi cha timu hiyo.

Ameshinda kila taji. Kwangu namtakia kila la kheri katika maamuzi yake ya kuondoka Man United wakati huo huo namtakia Jose Mourinho The Special One, kila la heri atakapoanza kazi ya kukinoa kikosi cha timu hiyo.

Wakati huo huo Zlatan Ibrahomivic ashaatua Manchester United. Zlatan aliyekuwa akikipiga Paris Saint German Ufaransa alikamilisha uhamisho wake juzi punde tuu baada ya kikosi chake cha Sweden kubanduliwa katika michuano ya Euro 2016 inayoendelea Ufaransa.

Ujio wake utakuwa wa muhimu sana kwa vijana wachanga Martial na Rashford. Hao ni washambuliaji chipukizi wa Manchester United na wanahitaji mtu wa kuwapa muongozo ili waweze kujiendeleza kisoka.

Zlatan ni mshambuliaji anayeheshimika duniani. Muda wake pale Manchester Utd utasaidia kukuza vipaji vya hawa washambuliaji wachanga wa kikosi hicho.

Eric Bailly kutoka Ivory Coast anayecheza katika safu ya ulinzi ndiye aliyekuwa wa kwanza kusajiliwa na kocha Mourinho. Zlatan amekuwa wa pili na Man United inatarajia kumalizana na Henrikh Mkhitaryan kiungo kutoka Armenia. Wakati huo huo kuna tetesi za hapa na pale kuhusu kurejea kwa Paul Pogba katika klabu hiyo ya Manchester Utd. Jose Mourinho anajulikana kwa kutengeneza kikosi cha kushinda mataji. Kwa hivyo shughuli zake za kuimarisha klabu ya Man Utd imeanza.

Hata hivyo swali langu ni je? Ataweza kubakisha kiungo Juan Mata katika kikosi hicho? Kumbuka ni Mourinho aliye muuza Mata wakati akiwa Chelsea.

Aliona Mata ni mzigo kwake katika klabu hiyo. Hata hivyo Mata alitua Man Utd na kutamba vyema katika kikosi hicho cha Mashetani Wekundu.

Swali langu kwa sasa ni je? Ataweza kufanya naye kazi katika kikosi hicho? Hayo yanabakia kuonekana ndani ya huu mwezi ujao kisa na maana wachezaji wataoondoka ni lazima wajulikane kabla ya mwisho wa mwezihuu kwani ligi kuu England inaanza Agosti 14.

Kwa hakika itakuwa ligi tamu kwa vile Pep Guardiola amejiunga na mahasimu wa Man Utd, Manchester City.

Ikumbukwe wakati wakiwa Hispania walikuwa mahasimu wakati huo Pep akikinoa Barcelona na Jose akiwa Real Madrid. Uhasama huo wa makocha hatari duniani unashuka katika Ligi Kuu ya England.

Huku kando yao kuna Mfaransa Arsene Wenger ikiwa klabu ya Arsenal. Je? Msimu ujao? Ni Mourinho, Wenger ama Pep atalibeba taji? Kila shabiki anavuta upande wake. Tusubiri.