Ranieri hakustahili kabisa kufukuzwa kazi

Muktasari:

Leo hii Leicester City imeshika nafasi ya 18 huku timu hiyo ikiwa katika nafasi ya kushika mkia.

SOKA ni mchezo wenye vitu vinavyobadilika haraka. Wakati huu msimu uliopita Leicester City iliongoza Ligi Kuu ya England.

Leo hii Leicester City imeshika nafasi ya 18 huku timu hiyo ikiwa katika nafasi ya kushika mkia.

Ni hali hii ambayo imeisababisha Bodi ya Leicester kumfukuza kazi Kocha Claudio Ranieri.

Kocha ambaye miezi mitatu iliyopita alipewa tuzo ya Kocha Bora wa Dunia kwa mwaka 2016.

Kocha ambaye aliwapa Leicester taji la Ligi Kuu kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo.

Dunia ya soka imeshangaa kuona jinsi Leicester imeshindwa kupata matokeo mazuri msimu huu. Lakini, mashabiki wengi wa soka pia wameshangaa sana kwamba Kocha Ranieri amefukuzwa kazi.

Bila shaka, Leicester ipo katika hatari ya kushuka daraja. Ipo katika hali mbaya sana kisoka huku wachezaji tegemeo kama Riyaz Mahrez na Jamie Vardy hawapo kileleni kama msimu uliopita.

Bodi ya Leicester inaamini kwamba Kocha Ranieri hana uwezo wa kuhakikisha Leicester mkataba mpya katika Ligi Kuu.

Na ukweli ni kwamba klabu nyingi zilivyo katika hatari ya kushuka daraja zinafanya vizuri zaidi zinapopata kocha mpya.

Kisaikolojia wachezaji wengi wanaona uteuzi wa kocha mpya kama mwanzo mpya wa timu yao na hivyo wanajituma zaidi.

Msimu huu tumeshaona klabu kama Crystal Palace, Hull City na Swansea City wakifukuza makocha wao, huku wakiamini kwamba kocha mpya ataweza kurudisha timu zao katika hali nzuri kimpira.

Hakika Swansea imeanza kucheza vizuri zaidi chini ya kocha wake mpya, Paul Clement na Hull City imekuwa katika hali nzuri zaidi tangu Marco Silva alipopewa kibarua na klabu hiyo.

Lakini, kwa mtazamo wangu Kocha Ranieri hakustahili kufukuzwa kazi hata kama dalili nyingi zinaonyesha kwamba kocha mpya anaweza kuipa Leicester nguvu mpya.

Ni kwa kuwa kocha huyu ameshaonyesha kwamba ana uwezo mkubwa sana. Na shida za Leicester msimu huu kwa mtazamo wangu sio tu za Ranieri bali wachezaji wengi wa timu hiyo wamekosa njaa ya kupata mafanikio.

Ukimuondoa N’Golo Kante, kikosi cha Leicester msimu huu ni kilekile kilichoshinda Ligi Kuu ya England msimu uliopita. Lakini, wachezaji wengi katika kikosi hicho wamekuwa kivuli tu cha wachezaji ambao walishinda Ligi Kuu ya England msimu uliopita.

Kutokana na historia ambayo Ranieri ametengeneza na timu hii ya Leicester, naamini kwamba kocha huyu alistahili angalau kumaliza msimu na timu hiyo ya hata kama ipo katika hatari ya kushuka daraja.

Klabu ya Leicester iliundwa mwaka 1884 na ilichukua miaka 142 kwa timu hiyo kushinda Ligi Kuu ya England.

Huenda itachukua miaka 100 tena kwa Leicester kushinda Ligi Kuu na ndio maana mashabiki wa timu hiyo hawana shukrani za kutosha kwa Kocha Ranieri kwa kuwa wanajua kwamba katika maisha yao kuna nafasi kubwa kwamba hawatashuhudia tena timu yao ikishinda Ligi Kuu ya England.

Hata hivyo, kocha huyu hajapata nafasi kumaliza msimu na klabu ambayo anaipenda na ambayo ametengeneza historia kubwa.

Ni kweli ni muhimu sana kwa Leicester kuendelea kucheza katika Ligi Kuu, lakini, kutokana na Kocha Ranieri kuwapa klabu hiyo ubingwa wa Ligi Kuu ya England, binafsi niliamini alistahili kumaliza msimu akiwa na timu hiyo.