ROHO NYEUPE: Wavulana wa Arsenal hawawezi kutwaa ubingwa

WAKATI mwingine huwa tunapenda kubishana na ukweli. Ni wazi kuwa Arsenal haina ubavu wowote wa kushindana na timu kubwa za Ulaya kwa sasa, tunawaonea bure kuwataka wafanye hivyo.

Matokeo ya kipigo cha mabao 5-1 kutoka kwa Bayern Munich usiku wa juzi Jumatano ilikuwa mwendelezo tu wa filamu tamu ya vijana hao wa London kutaka kufanya mambo yaliyowazidi uwezo.

Nadhani hata wenyewe sasa wanafahamu kubwa uwezo wao umeishia pale, hawawezi kuwa na jipya.

Mara ya mwisho Arsenal kukaribia kutwaa ubingwa huo wa Ulaya ilikuwa mwaka 2006 walipopoteza kwa Barcelona katika mchezo wa fainali. Hata hivyo, bahati mbaya kwa Arsenal ni kwamba ilipata pigo la kadi nyekundu katika dakika za mwanzo tu na kucheza pungufu kwa zaidi ya dakika 70.

Hata hivyo, wakati huo Arsenal ilikuwa inaundwa na wanaume kibao. Golini alikuwepo Jens Lehmann ambaye ndiye alionyeshwa kadi nyekundu. Safu ya ulinzi ilikuwa na Emmanuel Eboue, Ashley Cole, Kolo Toure, Sol Campbell.

Safu yao ya ushambuliaji iliundwa na Freddie Lumberg, Robert Pires na Thiery Henry. Kwa kifupi ni kwamba kikosi hicho kilikuwa na mvulana mmoja tu, Cesc Fabregas, wengine wote walikuwa wanaume.

Baada ya hapo wanaume wakaanza kuondoka Arsenal. Aliondoka Henry, Toure, Pires na wengineo. Na hata Fabregas alipoanza kuwa mwanaume naye aliuzwa kwenda Barcelona. Hii ndio Arsenal ya kizazi kipya, Arsenal ya mwendokasi.

Baada ya hapo Arsenal sasa imecheza miaka sita bila kuvuka hatua ya 16 bora ya taji hilo la Ulaya, ni aibu iliyoje. Timu kama Arsenal ambayo kila mwaka inashiriki michuano hiyo inashindwaje kusonga mbele kwa angalau kufika robo fainali?

Hata hivyo, hayo ni matokeo ya vitu viwili vikubwa. Tatizo la msingi ni aina ya wachezaji ambayo Arsenal inayo kwa sasa. Wachezaji wa daraja la dunia wapo watatu tu. Yupo Alexis Sanches na Mesut Ozil katika safu ya ushambuliaji na katika safu ya ulinzi yupo Shkodan Mustafi. Mwanaume mwingine ni Granit Xhaka lakini hana utulivu wa akili.

Katika hali kama hiyo unawezaje kushindana na timu zilizojaa wanaume? Bayern Munchen imejaa wanaume. Kipa wake, Manuel Neuer ni mwanaume wa shoka. Mabeki wake, Philip Lahm, Matt Hummels na David Alaba ni wanaume achilia mbali Frank Ribery, Arjen Robben na Robert Lewandowsky. Timu ya Arsenal iliyojaa wavulana inawezaje kuwafunga ama kuwaondoa wanaume kama hawa kirahisi?

Hao ni Bayern tu, zipo timu kama Barcelona, PSG, Juventus, Real Madrid na Napoli zimejaa wanaume. Timu hizi zote si saizi ya Arsenal ambayo iliwahi kutolewa na Monaco katika hatua hiyo ya 16 Bora miaka miwili iliyopita.

Kama Arsenal haitapambana kujaza wanaume katika kikosi chake ni wazi kwamba itaendelea kutalii tu, katika mashindano ya kimataifa. Unafikiri unaweza kushinda taji la Ulaya kwa kuwategemea Alex Chamberlain na Theo Walcott?

Tangu nimemfahamu Walcott yupo vile vile, hakui. Uwezo wake umebaki kuwa wa kuchezea Arsenal tu, hakuna timu yoyote ya daraja la juu anayoweza kwenda na akacheza. Chamberlain naye yupo vile vile tu, hakui. Ni kama wana laana fulani vile.

Tatizo la pili la Arsenal ni kocha wake, Arsene Wenger. Kocha huyu uwezo wake wa kufikiri ni kama umefika mwisho. Akili yake anaijua mwenyewe. Wenger wa sasa sio yule wa mwaka 2001, 2003 ama 2004.

Wenger wa siku hizi kinachomtofautisha na makocha wengine ni ukubwa wa koti analovaa tu, hana mbinu mpya.

Kwanza ni vigumu kufahamu anahitaji kitu gani. Haeleweki katika mashindano manne anayoshiriki kwa msimu analenga kushinda taji gani. Kwanza ataanza kuondolewa katika Kombe la Ligi maarufu kama Emirates Cup (EFL).

Pili ataondolewa katika Kombe la FA kisha Uefa na baadaye ataondoka kabisa katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England. Mara nyingi timu yake inacheza vizuri pindi inapokuwa ikipambana kuhakikisha inamaliza katika nafasi nne za juu. Ni ajabu na kweli. Huyu ndiye Wenger wa sasa, kocha wa mwendokasi. Uzuri kwamba watu wa Arsenal hawafahamu kama wanamhitaji Wenger ama la. Kuna wakati wanabeba mabango kutaka afukuzwe, lakini kuna wakati wanajazana uwanjani na kuanza kumsifu. Hilo ni tatizo la wana Arsenal wenyewe.

Hata hivyo, ni lazima tukubali tu kuwa kwa aina ya wachezaji wa Arsenal pamoja na mbinu za kizee za kocha wake, Wenger hawawezi kushinda taji hilo la Ulaya, labda kama wataliiba na kulificha, ila kwa uwanjani hawana uwezo huo.

Ubaya zaidi ni kwamba sio kwa mwaka huu, ni kwamba hawataweza kulishinda kwa siku za karibuni hasa ikizingatiwa kuwa timu kama PSG na Manchester City zinawekeza fedha nyingi ili kuweza kuweka heshima hiyo Ulaya.ROHO