ROHO NYEUPE: Kwa Simba hii, hata Hans Pluijm angelaumiwa

Muktasari:

Leo hii unataka Simba icheze kwa kiwango sawa na Yanga wakati staa wa timu hiyo, Mussa Hassan ‘Mgosi’ ni mkongwe na hawezi kucheza kwa dakika 90? Ni miujiza pekee inahitajika.

SIMBA tayari imeanza mambo yake. Baadhi ya viongozi wa timu hiyo wanadai kuwa timu yao inacheza chini ya kiwango, licha ya kwamba inapata matokeo ya ushindi.

Wanajaribu kuilinganisha timu yao na watani zao Yanga. Wanasema kuwa Yanga inacheza vizuri na ndiyo sababu inapata matokeo makubwa. Uchungu huu wa viongozi wa Simba umetokana na namna timu yao ilivyocheza dhidi ya Stand United na kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0, tena nyumbani.

Mabosi hao wanadai kwamba timu yao pia ilicheza vibaya dhidi ya Kagera Sugar, licha ya kwamba ilipata ushindi. Wanaona kama Yanga imewaacha mbali sana kwa namna inavyocheza na kutoa adhabu za maana.

Kuna taarifa kuwa, viongozi hao hawana furaha na soka la Mwingereza Dylan Kerr. Wanasema timu yao inacheza hovyo na haina pumzi ya kutosha. Unawasikiliza na kugeuka ili uchekee pembeni, wanachokitamani ni kituko.

Unawezaje kutamani Simba icheze soka kali kama la Yanga? Unawezaje kutamani Simba ipate matokeo makubwa kama ya Yanga? Viongozi wa Simba wanakuwa wazito kidogo kukubaliana na uhalisia. Maisha siyo rahisi hivyo.

Yanga imesajili wachezaji bora pengine kuliko timu nyingine yoyote Ligi Kuu. Iliipiku Simba karibu kwa kila nyota iliyomhitaji. Ilimsajili Deus Kaseke, Geofrey Mwashiuya, Matteo Saimon na Malimi Busungu ambao walikuwa pia wanawaniwa na Simba. Yanga ilisajili pia nyota wawili kutoka Zimbabwe, Donald Ngoma na Thabani Kamusoko. Ni nyota wenye uwezo wa juu na kazi yao inaonekana uwanjani.

Ukiitazama Yanga ni kwamba imekamilika kila idara. Ina safu imara ya ulinzi, safu ya wastani ya kiungo na safu hatari ya ushambuliaji.

Katika benchi pia kumekaa nyota wa maana na hata wakinyanyua bango kufanya mabadiliko unatamani kulia kwani anayeingia anaweza kuwa mzuri zaidi ya yule anayetoka.

Sasa hapa ndipo ugonjwa unapoanza. Unailinganishaje Simba iliyokamilika eneo la kiungo pekee dhidi ya Yanga iliyokamilika kila idara? Hii itakuwa ni kichekesho.

Unafikiri ni mchezaji gani wa Simba kwa sasa kama akienda Yanga atapata nafasi katika kikosi cha kwanza? Labda mmoja ama wawili pekee. Lakini bado unataka Simba icheze na kutoa vipigo vikubwa kama Yanga? Hii ni sawa na kusubiri treni kituo cha basi.

Simba ilitaka wachezaji wa viwango vya kawaida wakati wa usajili na lazima ikubali kucheza soka la kawaida kwenye Ligi. Unawezaje kuwa na timu ambayo inategemewa kubebwa na Ibrahim Ajibu ama Hassan Isihaka ambao kama wakienda Yanga wanaweza kukosa hata nafasi za benchi?

Unawezaje kuilinganisha Simba na Yanga wakati timu hiyo inategemea kubebwa na straika wa mkopo kutoka Azam, Joseph Kimwaga? Huu ni utani wa ngumi.

Simba kwa sasa inamtegemea Hamis Kiiza kama straika wake hatari, wakati huo huo Yanga ina mastraika wanne hatari. Busungu pekee ambaye anakaa benchi pale Yanga anaonekana kuwa hatari pengine kuliko Kiiza. Unaanzaje kuzilinganisha timu hizi mbili?

Kinachotokea Simba kwa sasa ni matokeo ya fikra finyu za baadhi ya viongozi wao kuwa timu yao haihitaji wachezaji wa viwango vya juu kwa kuwa haina majukumu ya kimataifa mwakani. Timu ikaishia kusajili wachezaji wa viwango vya kawaida na ndiyo maana wanacheza soka la kawaida.

Leo hii unataka Simba icheze kwa kiwango sawa na Yanga wakati staa wa timu hiyo, Mussa Hassan ‘Mgosi’ ni mkongwe na hawezi kucheza kwa dakika 90? Ni miujiza pekee inahitajika.

Hicho ndicho kinachotokea kwa sasa katika kikosi cha Taifa Stars ambapo wakati mwingine katika kikosi cha kwanza kunakosekana hata nyota mmoja wa Simba. Mchezo dhidi ya Malawi, juzi Jumatano alianza Said Ndemla pekee kwa upande wa Simba wakati huo huo Yanga ilikuwa na nyota wanne katika kikosi cha kwanza.

Viongozi wa Simba wanatakiwa kufika sehemu waheshimu angalau kile kinachofanywa na Kerr kwa kuwa timu hiyo uwezo wa wachezaji wake uko chini ukilinganisha na Yanga na Azam.

Leo hii hakuna mchezaji wa Simba anayeweza kupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha Azam. Ni wachache pia wanaoweza kupata nafasi katika kikosi cha pili cha Azam.

Hata hivyo, licha ya ubora wa nyota hao wa Azam bado timu yao haijawa katika kiwango bora japo inashinda. Kikubwa kinachohitajika ni kuweka nguvu na kusaidia pale penye mapungufu na siyo kuona kuwa timu yao inacheza vibaya.

Hata kocha anayeaminika kuwa bora nchini kwa sasa, Hans Van Pluijm  ambaye anakifundisha kikosi cha Yanga, bado asingeweza kuifanya Simba itoe vipigo vikubwa kwa timu pinzani kama anavyofanya katika timu yake hiyo.

Wachezaji waliopo bado siyo wa kiwango cha dunia. Pluijm naye angeishia kupewa lawama.