ROHO NYEUPE: Kaseja, Nizar watuambie ukweli juu ya umri wao

Friday March 17 2017Gift  Macha

Gift  Macha 

By GIFT MACHA

WAKATI mwingine inabidi tuambizane ukweli hasa katika maisha yanayohusu soka. Mapema wiki hii nilikuwa nikipitia takwimu za umri wa wachezaji wa timu mbalimbali za hapa nchini. Umri wao ulinishtua sana.

Katika wachezaji wote niliowatazama, sikupata mashaka na mchezaji mmoja tu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, nahodha wa Yanga. Rekodi zake zinaonyesha kwamba Cannavaro ana miaka 35. Ni nani anayebisha katika hili?

Ukimtazama Cannavaro anasadifu umri huo. Alianza kucheza Ligi Kuu ya Zanzibar mwaka 2003 na sasa ametimiza miaka 14 katika maisha yake ya soka la ngazi ya juu. Nani anataka kupingana na hili. Cannavaro anaonekana wazi kwamba anaendana na miaka yake. Sijawahi na sitawahi kuwa na mashaka naye.

Katika hali ya kawaida wachezaji wengi wa Tanzania wanaanza kucheza Ligi Kuu wakiwa na umri wa miaka 20 au 22. Ni vigumu kwa mchezaji wa kawaida kucheza Ligi Kuu chini ya umri huo. Kama wapo ni wachache. Hii ndiyo sababu ninaamini kwamba Cannavaro atakuwa alianza kucheza ngazi ya Ligi Kuu akiwa na miaka 21.

Wachezaji wengi wa Tanzania wanachelewa kucheza Ligi Kuu kutokana na udogo wa maumbile yao. Wachezaji wengi wa Tanzania wana maumbile madogo. Ukiwatazama wachezaji wa Serengeti Boys wengi wao hawana miili ya kuweza kucheza Ligi Kuu. Wana vipaji vikubwa lakini maumbo yao ni madogo.

Kutokana na udogo huo wa maumbile, wengi wanalazimika kusubiri angalau mpaka wafikishe umri wa miaka 21 ili kuweza kushindana Ligi Kuu. Ni nadra kwa mchezaji kutamba chini ya umri huo.

Hii ndiyo sababu inayonipa mashaka juu ya umri halisi wa baadhi ya wachezaji wa timu mbalimbali nchini. Baadhi ya wachezaji umri wao hauendani na historia yao. Kuna walakini kidogo.

Mchezaji wa kwanza anayenipa mashaka ni kipa Juma Kaseja. Huyu rekodi zinaonyesha kwamba ana miaka 32. Inahitaji roho ngumu kuweza kukubaliana na rekodi hizo za umri wake. Historia yake inapingana na namba hizo pia.

Kwanza, Kaseja ana historia kubwa katika soka la Tanzania. Alianza kucheza soka la ushindani mwaka 1999, hivyo mpaka sasa anatimiza miaka 18 ya maisha yake ya soka. Hii inamaanisha kwamba alianza kucheza Ligi Kuu akiwa na miaka 14. Haijawahi na haitawahi kutokea katika soka la Tanzania.

Kaseja alijiunga na Moro United mwaka 2001 na kuwa kipa namba moja wa timu hiyo. Kwa mujibu wa miaka yake ya soka ni kwamba alijiunga na timu hiyo ya Morogoro akiwa na miaka 16 tu. Haiwezekani na haitakaa iwezekane kwa mchezaji wa Tanzania kucheza Ligi Kuu akiwa na umri wa miaka 16.

Kaseja baadaye alitua Simba akadaka kwa miaka 10 na miaka miwili aliidakia Yanga. Mwishoe Kaseja akaporomoka na kuwa kipa wa kawaida. Inashangaza sana.

Inawezekanaje Kaseja aliyezaliwa mwaka 1985 anakuwa kipa wa kawaida wakati Buffon aliyezaliwa mwaka 1979 bado ni kipa namba moja wa Timu ya Taifa ya Italia? Kuna kitu kinajificha mahali hapa.

Mchezaji wa pili anayenipa mashaka ni Nizar Khalfan. Kwa mujibu wa rekodi za miaka yake duniani, Nizar ambaye aliichezea Moro United anaonyesha kwamba ameishi miaka 29. Inashangaza kidogo. Nyota huyo ambaye amehitimu mafunzo ya ukocha katika ngazi ya kati ni dhahiri kwamba soka la ngazi ya juu limemshinda sasa. Nizar amewahi kucheza soka la kulipwa Canada katika Klabu ya Vancouver White Caps kabla ya kuachwa na kurejea nchi kuitumikia Yanga.

Kiungo huyo baada ya kutemwa na Waamerika alijiunga na Yanga na kuichezea kwa miaka mitano. Nizar ni aina ya viungo ambao walikuwa wakifanya kazi nyingi uwanjani. Unyumbulifu wake ndiyo ulimpa sifa kubwa.

Kiungo huyo baadaye alijiunga na Mwadui na kisha Singida United. Kwa Nizar siku hizi soka siyo kazi yake ya msingi. Kiwango chake uwanjani hakitishi tena na ndiyo sababu alikwenda kusaka nafasi katika timu ya Ligi Daraja la Kwanza. Inatia mashaka kwa kiungo aliyewahi kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania kuporomoka hadi kucheza Ligi Daraja la Kwanza akiwa na miaka 28 tu. Haiwezekani na haitakaa iwezekane. Mchezaji anapofikia umri wa miaka hiyo ndiyo anakuwa katika kilele cha ubora wake.

Leo hii Leonel Messi ndiyo kwanza ana miaka 29, kiwango chake bado ni cha dunia. Zlatan Ibrahmovic ana miaka 35 lakini anaitikisa dunia. Yahya Toure ana miaka 33 lakini bado ameikamata Manchester City. Inawezekanaje Nizar ashuke tu kiwango ghafla akiwa na miaka 28? Kuna uongo umejificha mahali. Sina maana kwamba wachezaji hawa wamedanganya umri, bali ninamaanisha kwamba kuna kitu hakiendi sawa. Kama umri waliotaja ni sahihi, basi wana tatizo kubwa katika viwango vyao. Kama umri waliotaja siyo sahihi, basi wanastahili kuwapo hapo walipo.