ROHO NYEUPE : Azam inajenga ghorofa, kisha inaezeka kwa nyasi

Muktasari:

  • Nimeona kwa wiki nzima hii rundo la wachezaji wakitua kwenda Azam kufanya majaribio. Ni wachezaji wengi kweli kweli. Kuna hadi kipa wa mwendokasi kutoka Hispania.

KUNA tatizo mahali pale Azam, sasa nimeanza kuamini. Tena tatizo hili siyo dogo kwani linazidi kuitafuna timu hiyo siku hadi siku. Yawezekana ni tatizo la utawala ama ni la mfumo, soma hapa halafu utaniambia mwenyewe.

Nimeona kwa wiki nzima hii rundo la wachezaji wakitua kwenda Azam kufanya majaribio. Ni wachezaji wengi kweli kweli. Kuna hadi kipa wa mwendokasi kutoka Hispania.

Hoja ya Azam, ni kwamba wanataka kocha wao mpya Zeben Hernandez awatazame nyota hao ili apitishe wale atakaovutiwa nao kwa ajili ya kusuka kikosi kipya cha msimu ujao. Yawezekana ni mfumo mzuri kwa Hernandez.

Hata hivyo, utaratibu huu wa majaribio tayari ulishafeli pale Azam na ni ajabu kuona bado unaendelea kutumika. Ni sawa na kutaka kuezeka ghorofa kwa nyasi.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita nyota zaidi ya saba wamekuja kufanya majaribio Azam, lakini cha ajabu ni mmoja tu alikuwa na kiwango angalau cha wastani, ni Jean Mugiraneza ‘Migi’. Wengine? Ilikuwa ni aibu, hakuna aliyekuwa na msaada wowote wa maana na wote wameshaachwa.

Kwanza kabisa alikuja straika mmoja kutoka Ivory Coast, anaitwa Ismail Kone, akafanya majaribio halafu akafuzu. Cha ajabu ni kwamba jamaa alicheza nusu msimu pale Azam bila lolote la maana. Muda mwingi alikuwa mgonjwa na hakufunga hata bao la kuotea. Mwishowe akawa amefanya tu majaribio na kula mshahara wa bure. Azam ikamtema. Msimu uliofuata Azam ikawaleta Leon Saint Preux na Ismail Diara. Hawa jamaa walifuzu majaribio kwa kishindo, lakini uwanjani wakawa vituko. Nyota hao walicheza kwa nusu msimu tu na kuonekana kuwa wamekuja kufanya maonyesho nchini. Azam ikaachana nao.

Msimu uliopita ikawaleta Allan Wanga, Racine Diouf na Migi. Baada ya msimu kumalizika ni Migi pekee alionyesha juhudi, japo siyo kwa kiwango cha kutisha. Mwisho wa msimu Azam imeachana na nyota hao na sasa inaanza tena majaribio.

Ni jambo la kushangaza sana kuona bado Azam inategemea wachezaji wa majaribio licha ya mpango huo kufeli tena moja kwa moja katika miaka mitatu iliyopita. Huu mfumo aliupeleka nani pale Azam? Kwa nini hawajifunzi kutokana na makosa? Unamnufaisha nani hasa? Kuna maswali mengi ambayo hayana majibu.

Kutokana na wachezaji wengi wa majaribio kuchemka pale Azam nilitazamia kuona mabadiliko katika mfumo huo wa usajili, lakini cha ajabu bado unaendelea.

Ni vigumu sana kumpata mchezaji mzuri kwa mfumo wa majaribio. Mchezaji mzuri anaonekana uwanjani katika mechi tena ya ushindani na siyo katika majaribio. Kwenye mechi utaona uwezo halisi wa mchezaji. Unaona uwezo wake wa kukokota mpira, kupita pasi na kufanya maamuzi. Haya huwezi kuyaona katika mazoezi.

Katika mazoezi wachezaji hawaonyeshi ubora wao kwa asilimia 100. Kunakuwa na utani mwingi na ubishoo. Hii ndiyo maana mchezaji anaweza kufunga mabao 10 mazoezini na kwenye mechi asilenge hata shuti moja langoni. Kwa nini Azam inaung’ang’ania mfumo huu mbovu?

Mpaka leo hii wachezaji wa kigeni wanaotamba Azam kama Kipre Tchetche na Sergie Wawa walisajiliwa baada ya kuonwa kwenye mechi na siyo majaribio. Tchetche alitamba na kikosi cha Ivory Coast kilichokuja kama waalikwa katika michuano ya Kombe la Chalenji hapa na aliposajiliwa uwezo wake umeonekana. Wawa alionekana pindi Azam ilipocheza na El Merreikh na alisajiliwa uwezo wake ukaonekana. Hawa wengine ni wa majaribio na ndio maana wanakuja usiku na kuondoka Alfajiri. Sijui kwa nini Azam haitaki kubadili mfumo huu. Katika hali ya kawaida huwezi kumleta kipa kutoka Hispania kuja kufanya majaribio Azam chini ya uangalizi wa kocha wa makipa kutoka Hispania, halafu ukatarajia kupata kilichobora. Hapana, tutakuwa tunadanganyana.

Kwa hatua iliyofikia Azam kwa sasa tulitegemea kuona wanasajili katika timu zinazoshiriki michuano ya Afrika kama Medeama ya Ghana ama Mo Bejaia ya Algeria. Tulitegemea kuona makocha wao wakitazama mechi hizo kupata nyota wa kuwasajili. Tulitegemea kuona timu hiyo inaenda kusaka wachezaji katika michuano ya Chan ama katika ligi mbalimbali zinazoendelea kwa sasa kama ile ya Kenya, Rwanda, DR Kongo na nyinginezo kuliko kutuletea rundo la wachezaji wa majaribio.

Katika mfumo huu wa usajili sitegemei kuona Azam ikipata mchezaji mzuri wa kariba ya Tchetche ama Wawa. Pia, sitarajii kuona Azam ikipata mchezaji ambaye atadumu na timu kwa zaidi ya mwaka mmoja. Sitarajii kuona wakipata vipaji halisi vya soka. Kadhalika sitarajii kuona Azam ikisogea zaidi ya hapo ilipo sasa kwa mfumo huu wa usajili. Sitarajii kuiona Azam ikiziacha nyuma Simba na Yanga kwa mfumo huu wa usajili. Sitarajii kuiona Azam ikitikisa Afrika kwa mfumo huu wa usajili. Mabadiliko ya mfumo ndiyo yatakayoitoa hapa ilipo.