Pongezi kwa RT, safi DB kwa kushtuka

Monday May 15 2017

 

KAMA kuna shirikisho la michezo linaloonyesha tofauti kubwa ya utendaji na kuleta tija ndani ya mwaka 2017 basi ni Shirikisho ya Riadha Tanzania (RT).

Tangu uongozi mpya wa shirikisho hilo ulipoingia madarakani mwishoni mwa mwaka jana, kumekuwa na mabadiliko makubwa na mafanikio katika mchezo huo.

Achana na matokeo mazuri waliyopata wanariadha wetu kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa, lakini hata mwishoni mwa wiki imethibitika kuwa RT ya kina Wilhem Gidabuday siyo ya mchezo, baada ya timu ya taifa ya chini ya umri wa miaka 17 kufanya vizuri.

Timu hiyo imeitoa kimasomaso Tanzania katika mashindano ya vijana kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati baada ya kuzoa medali za kutosha kinyume na ilivyozoeleka ambapo Tanzania ilikuwa kama msindikizaji wa mataifa mengine katika mashindano hayo.

Kwa hakika kilichofanywa na wanariadha wa Tanzania katika michuano hiyo ni sifa kubwa kwa RT na taifa kwa jumla na kuonyesha dalili za wazi kuwa, kuna mambo makubwa yanayokuja chini ya uongozi huu wa kina Gidabuday.

Hata hivyo, Mwanaspoti inalitahadharisha shirikisho hilo kuwa, wasilewe sifa na kuona wamemaliza kazi, waongeze juhudi kubwa ili kuifanya riadha Tanzania iwe kama ile ya miaka ya 1970-90, wakati taifa letu lilipokuwa likitawala Afrika na duniani.

Tunaamini, huu ni mwanzo tu kwa viongozi hao kuweza kuongeza juhudi kubwa ili ifike timu zetu zinapokwenda katika michuano mikubwa kama ya Olimpiki, Jumuiya ya Madola, Mashindano ya Dunia na Michezo ya Afrika (All Africa Games), tutishe.

Ni muda mrefu Tanzania imekuwa wanyonge kwenye anga za kimataifa kupitia mchezo huo, lakini kilichoanza kuonekana chini ya uongozi huu wa RT kinatoa tumaini na wajibu wao kuchangamka zaidi ili heshima yetu irudi.

Muhimu na tunaloukumbusha uongozi huo wa RT, ni kuhakikisha vijana hao wa U17 wanatunzwa na kuendelezwa kwa nia ya kuja kuwa tegemeo la taifa katika miaka ijayo, kwani wameonyesha wana uwezo mkubwa katika mchezo wa riadha.

Mbali na kuwapa kifyagio RT, pia Mwanaspoti tumefurahishwa na hatua iliyoanza kuchukuliwa na Chama cha Mpira wa Kikapu cha Mkoa wa Dar es Salaam (BD) cha kutaka kuanzisha Ligi Daraja la Kwanza (1st Division) kwa nia ya kuongeza ushindani.

Uongozi wa DB umeona mbali na ni kama wamejishtukia kuwa, kuendesha Ligi ya Mkoa ya RBA, bila ya kuwepo kwa ligi nyingine ni mtihani katika kukuza mchezo huo na uamuzi wao wa kutaka kuanzisha michuano ya Ligi ni japo la kupongezwa.

Tunaamini kuwa, kuwepo kwa ligi hiyo kutasaidia kuzifanya timu zitakazoshiriki kupambana kwa nia ya kukwepa kushuka daraja na kupigia hesabu ubingwa.

Hii itafanya hata wachezaji kuwa makini na kuzipigania klabu zao kwa nguvu zote ili kuhakikisha zinaweka heshima na hata zinaposhuka maana yake kutakuwa na ligi ngazi ya chini na mchezo wa kikapu utapanuka zaidi tofauti na sasa.

Mwanaspoti linaamini kinachoanzishwa na DB kitakuja kuigwa na mikoa mingine na mwishowe kuja kuwa na Ligi ya taifa itakayokuwa ikitoa bingwa na wawakilishi wa nchi na kuufanya mchezo hu kuzidi kukua na kuibua vipaji vilivyosahaulika.

Tunaikumbusha DB kuwa wanapokwenda kuanzisha ligi hiyo, pia wakumbuke kusaka wadhamini kwa nia ya kuifanya ligi hiyo iwe na msisimko na ushindani zaidi kwa timu na wachezaji wao kuamini kuwa kuna zawadi wanazoziwania.

Wasiendeshe ligi kwa kuzituza klabu za ligi hiyo, kombe tupu na medali ama kuwapa vyeti kama tunavyoshuhudia kwenye michuano mingine na kufanya wachezaji wahisi kama wanacheza bonanza na siyo mashindano ya ligi.

Pia DB wazingatie suala la viwanja kwani tumeshuhudia mechi mbalimbali zikisimama kupisha mvua katika Uwanja wa ndani wa Taifa na hivyo kuzurotesha mchezo huo.

Endapo kutapatikana viwanja bora kwa ajili ya mchezo huo, ni wazi ligi itakuwa nzuri na hata vijana nao watajitokeza kwa wingi wakizingatia kuwa wanacheza katika mazingira mazuri na salama.

Tunawatakia kila la heri DB kwa mipango mkakati hiyo ya kuileta Ligi Daraja la Kwanza kwani tunaamini ni mwanzo mzuri wa kurejesha heshima ya Kikapu ambao miaka kadhaa iliyopita ulikuwa na hamasa kubwa kwa wapenzi wa michezo.