Pongezi Lipuli FC, Serengeti Boys, ila mjipange sana

JASHO la mtu halipotei bure. Serengeti Boys, timu ya taifa ya Vijana chinia ya miaka 17, imefuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika. Serengeti itakuwa ni miongoni mwa timu nane zitakazochuna kwenye fainali hizo zitakazofanyika Mei 24 hadi Juni 4 mwaka huu nchini Gabon.

Tanzania imepata fursa hiyo baada ya kushinda rufani yao waliyomkatia Langa Lesse Bercy wa timu ya Congo Brazzaville, ambaye alichezeshwa akiwa kijeba, kushinda Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Mchezaji huyo alikuwa akituhumiwa kuwa na umri mkubwa na kutakiwa kupelekwa CAF kufanyiwa vipimo kugundua umri halisi alionao, lakini Congo ikawa inakwepa kwani inatambua kuwa ilikiuka kanuni za mashindano hayo.

Tangu mapema ilionekana wazi nafasi ya Serengeti Boys kwenye michuano hiyo ilikuwa halali yao baada ya kupata ushindi wa 3-2 nyumbani dhidi ya Congo kabla ya kwenda kufungwa bao dakika za majeruhi na kuwang’oa michuanoni ndipo ikakatwa rufaa hiyo na kushinda. Kufanikiwa kwa Serengeti kwenda katika fainali hizo ni faraja kubwa kwa vile, ni miaka mingi imepita bila Tanzania kufikia hatua hiyo katika michuano yoyote ya Afrika tangu ilipocheza fainali za Afcon 1980 na Chan 2009.

Mwaka 2004 Serengeti Boys ilifuzu fainali kama hizo za Gabon, lakini kosa la kumchezesha kijeba kama walivyofanya Congo, iliiondosha timu hiyo katika fainali hizo na nafasi yao kuchukuliwa na Zimbabwe.

Mwanaspoti inaipongeza timu hiyo kwenda kwenye fainali hizo za Mei, lakini ikiwakumbusha wachezaji kuwa, kazi ndio inaanza. Lazima wakapambane ili kuhakikisha ushiriki wao unakuwa na tija ikiwamo kufika mbali zaidi. Bahati nzuri ni kwamba, michuano ya mwaka huu, timu zitakazotinga nusu fainali moja kwa moja zitaiwakilisha Afrika kwenye fainali za Kombe la Dunia za U17 zitakazofanyika Oktoba 8-28 mwaka huu nchini India.

Tunawamini vijana wetu kwa sababu rekodi zao kabla ya kufika hapo walipofika zinavutia, lakini bado kunahitajika maandalizi mazuri zaidi ili kuona Serengeti haiwi wasindikizaji wa wengine. Katika kundi lao la B, Tanzania ipo na Niger, Angola na Mali, huku Kundi A lina Guinea, Gabon, Ghana na Cameroon.

Ukiangalia makundi yalivyo ni wazi kama Tanzania itakomaa katika mechi zao za makundi, itaweza historia ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia za U17.

Wakati tukiipongeza Serengeti Boys na kuitakia kila la heri, pia tunaipa heko Lipuli FC ya Iringa kwa kufanikiwa kuwa klabu ya kwanza kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao baada ya kuvuna pointi za kutosha katika Ligi Daraja la Kwanza.

Kwa hakika Mwanaspoti linaamini Lipuli walistahili kupanda Ligi Kuu kwa kazi kubwa iliyofanya ikicheza nyumbani na ugenini, japo kulikuwa na maneno kuwa ilikuwa ikibebwa uwanja wa nyumbani.

Ukweli Lipuli imepigana na hatimaye kurejea Ligi Kuu baada ya zaidi ya miaka 15 tangu iliposhuka mwaka 2001. Walioshiriki kwa namna moja ama nyingine kuirejesha Lipuli Ligi Kuu wanastahili pongezi zao, lakini wakijua wazi kuwa, kazi ndio inaanza.

Ligi Kuu ya sasa sio ya mchezo mchezo na wajibu wao kujipanga kwelikweli ili wasiishiriki na kurudi walipotoka katika msimu mmoja.

Hata kwa klabu nyingine mbili zitakazoungana na Lipuli kukamilisha idadi ya timu tatu za kucheza Ligi Kuu msimu ujao, nazo kujipanga ili zisiumbuke.