JICHO LA MWEWE: Nne za Yanga ziheshimiwe, zimenikumbusha zamani

Muktasari:

  • Haitokei kwa Yanga kushambuliwa hivyo. Kwa akili ya haraka haraka mara ya mwisho Yanga kushambuliwa hivyo na timu ya Tanzania ilikuwa jioni ile ambayo Emmanuel Okwi aliwasha moto katika lango la Yanga Mei 6, 2012 wakati Yanga ilipolala 5-0 pale Taifa.

NILIKUWEPO uwanjani siku Mwamuzi, Nassor Hamduni kutoka Kigoma alimpomsimamia kipa wa Yanga, Steven Nemes avae glovu zake haraka pambano kati yao na Pamba ya Mwanza liendelee. Mpira ndio kwanza ulikuwa umeanza na Nemes aliamua kuwapumzisha mabeki wake.

Mabeki wake walionekana kuchanganyikiwa na kasi ya Pamba. Ile safu ya Pamba mbele kulikuwa na kina Kitwana Suleiman, Beya Simba, Hamza Mponda, Fumo Felician na wengineo. Ndani ya dakika tano tu walikuwa wamegongesha mwamba mara tatu. Nemes akaona isiwe shida. Akavua glovu zake na kujifanya kaumia. Alikuwa anapoza mashambulizi ya Pamba.

Siku hizi haitokei sana. Haitokei kwa Yanga kushambuliwa hivyo. Kwa akili ya haraka haraka mara ya mwisho Yanga kushambuliwa hivyo na timu ya Tanzania ilikuwa jioni ile ambayo Emmanuel Okwi aliwasha moto katika lango la Yanga Mei 6, 2012 wakati Yanga ilipolala 5-0 pale Taifa.

Zamani lilikuwa jambo la kawaida. Simba na Yanga zilikuwa zinawashiwa moto vilivyo na timu nyinginezo nchini kama Pamba, Tukuyu Stars, Mecco, Ushirika, Coastal Union na nyinginezo. Lilikuwa jambo la kawaida kabisa.

Siku hizi mpira umekufa kidogo nchini. Juzi Yanga imechezea kichapo ch amabao 4-0 na Azam pale Unguja katika michuano ya Kombe la Mapinduzi. Yanga haikuzidiwa sana katika mechi. Haikuwa taabani sana katika maeneo yote. Lakini ilikuwa ovyo katika safu ya ulinzi hasa baada ya kufungwa bao la kwanza na John Bocco katika dakika ya kwanza tu ya mchezo.

Bao hilo lilivuruga mipango yake yote kwa sababu katika miaka ya karibuni hapa nchini, Yanga huwa imezoea kuogopwa uwanjani. Wanacheza kwa kumiliki mpira na kushambulia zaidi. Bao la Bocco lilimaanisha kuwa Yanga ilikuwa na kazi mbili uwanjani. Kwanza itafute bao la kusawazisha, halafu pili ifunge mlango wake kwa kuhakikisha inakuwa makini na Azam haifungi tena.

Hili la pili Yanga haikuliweza tena. Haikuweza kuubalansi mchezo. Bahati nzuri, katika siku ambayo kipa wake, Deogratius Munishi alikuwa ovyo, Azam ilizitumia vema nafasi zake.

Tatizo ni kwamba katika siku za karibuni tuna mashabiki wapya katika soka. Tuna mfumo mpya pia katika soka. Zimekuja timu nyingi ambazo hazina upinzani kwa Simba na Yanga. Mashabiki wengi hawaamini kama Yanga inaweza kufungwa mabao manne na Azam.

Sasa kwa wale mashabiki wapya waliopo Jangwani ni lazima itatafutwa sababu. Kipigo hiki hakiwezi kupita bure. Ataanza kubebeshwa lawama kocha mpya, George Lwandamina. Baada ya hapo kuna wachezaji pia watabebeshwa lawama. Hapa ndipo mpira wa Tanzania ulipofia.

Hatujazoea ushindani. Hatujazoea kukubali ubora wa adui, tumezoea kulaumu mapungufu ya timu zetu. Mashabiki wamezoea kuona Yanga inakwenda Uwanja wa Taifa. JKT Ruvu anapata bao la kuongoza, halafu Yanga inarudisha, halafu inafunga la pili, halafu inafunga la tatu, halafu inafunga la nne. Huu ndio mpira wetu wa miaka ya karibuni.

Kama Simba na Yanga zingekuwa zinakumbana na makali kama ya Azam juzi katika mechi nyingi za Ligi Kuu, basi mpira wetu ungepanda kwa kasi. Tatizo tumelirudisha soka letu chini kiasi cha kuamini kwamba, Yanga haistahili kuchezea kichapo katika soka la ndani labda ifungwe na Simba tu.

Hapo hapo unajiuliza. Nguvu ya Barcelona na Real Madrid Hispania halafu bado zinakumbana na vichapo hivi. Unajiuliza jinsi Manchester United alivyochezea 4-0 kutoka kwa Chelsea msimu huu. Unajiuliza jinsi Manchester City alivyopigwa nyingi na Leicester City msimu huu. Unajiuliza jinsi Arsenal ilivyopigwa nyingi na Liverpool msimu huu. Ni kitu cha kawaida kwa wenzetu.

Ni heshima kubwa kwao pindi wanapoona soka lao halitabiriki. Ni fedhea kubwa kwetu kama tunaona kipigo cha Yanga ni aibu. Sio aibu. Ni kitu cha kawaida katika soka la ushindani. Sikumbuki mara ya mwisho ni lini nilienda Uwanja wa Taifa nikashuhudia Yanga ikifungwa na timu nyingine ya kawaida nje ya Simba na Azam. Ni zaidi ya miaka mitatu sasa.

Zamani Yanga ilikuwa inafungwa na Pilsner au Nyota Nyekundu. Siku hizi sisikii Yanga ikifungwa na JKT Ruvu wala Ruvu Shooting. Mashabiki wanalipa kiingilio kwenda kuangalia ushindi wa Yanga na si vinginevyo. Zamani ilikuwa tofauti.

Hata vikosi vya zamani vya timu ya taifa vilikuwa vinatuletea wachezaji mchanganyiko mafundi kutoka katika timu za mikoani kama kina Dadi Athumani, Costa Magoloso, Hussein Mwakuruzo, Ally Maumba, Idrisa Ngulungu na wengineo. Hawakuwahi kugusa Simba na Yanga lakini walikuwa wanaitwa katika vikosi vya timu ya taifa kutokana na moto waliokuwa wanauwasha dhidi ya  timu hizo.

Kipigo hiki cha Yanga kimenikumbusha mpira ule ambao ulikuwa hautabiriki.