NINAVYOJUA: Ni mapema mno kuzipeleka Simba, Yanga Chamazi

Muktasari:

  • Ni Tanzania tu ndipo unapowakuta wapenda mpira wote wakiwa wamegawanyika kiushabiki kwa timu hizo mbili huku wakiwa wanaziongoza klabu nyingine.

TANZANIA ni taifa la ajabu, hasa unapozungumzia suala la ushabiki wa soka hasa kwa timu zetu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom na hata zile zilizowahi kutamba katika ligi hiyo kama vile Tukuyu Stars, Coastal Union, Pamba na nyingine.

Timu hizo kwa namna zilivyotamba nchini ilitarajiwa ziwe zimejitengenezea himaya ya mashabiki wake katika miji yao.  Lakini wapi ni kama leo timu zenye uzoefu wa ligi hiyo kama Mtibwa Sugar, Prisons, Mbeya City, Toto Africans na kadhalika nazo zikishindwa kufanya hivyo.

Ndio maana nasema Tanzania ni nchi ya ajabu sana, kwani ni aghalabu kumkuta Mtanzania mpenda soka asiwe na ushabiki wa pande za Simba na Yanga. Ni Tanzania tu ndipo unapowakuta wapenda mpira wote wakiwa wamegawanyika kiushabiki kwa timu hizo mbili huku wakiwa wanaziongoza klabu nyingine.

Hakuna mtu atakayebaki salama hapa awe ni kiongozi wa Mbeya City, Ndanda, Kagera Sugar, Azam, JKT Ruvu, Mwadui ama kocha au daktari wa timu hizo ambaye hashabikii timu hizo kongwe ama Simba au Yanga. Ndio maana haishangazi kusikia kiongozi wa Kagera Sugar ama Toto kushiriki uchaguzi ama mkutano wa klabu hizo kubwa na kujitamba bila kujisikia soni.

Hata kwa wanahabari,  kwa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na vyama vyake shiriki nako unazi wa klabu hizo mbili unatawala. Hii ndio tofauti kubwa kati ya Tanzania na Afrika Kusini, Ghana, Misri, Tunisia ana nchi nyingine achilia mbali huko Ulaya.

Ndio maana Simba na Yanga zinapocheza kwenye uwanja wowote hapa nchini iwe ni Chamazi, Kirumba, Mkwakwani, Nelson Mandela, Sokoine, Jamhuri, Kaitaba na kokote kule huwa kama zinacheza nyumbani. Klabu hizo huwa hazina mechi za nyumbani wala za ugenini kwa jinsi zinavyoungwa mkono. Kinachobadilika tu ni kwamba Yanga ikicheza Mbeya dhidi ya Prisons mashabiki wa Simba wa jiji hilo wataonekana kuishangilia Prisons. Vivyo hivyo siku maafande hao wakicheza na Yanga wale wa Simba wataipiga tafu na sio kama wanaoshangilia ni mashabiki wa klabu hiyo ya Prisons.

Hali hiyo utaikuta Ruvuma, Mwanza, Shinyanga na kwingine ambapo  Simba na Yanga huwa zinaenda kucheza. Uingereza, Hispania, Ujerumani na kwingine huko Ulaya kuna michuano mingi ambayo huzikutanisha timu kubwa dhidi ya timu ndogo zinazomiliki viwanja vinavyochukua watazamaji wachache sana.

Mfano msimu uliopita Real Madrid ilicheza dhidi ya Cornella, ni timu ndogo na ilifanikiwa kuitoa kwa jumla ya mabao 13–2 katika Copa de Leroy, huku Barcelona ikicheza dhidi ya Huesca na kuifunga  mabao 16-1 katika hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo. England kwenye michuano kama ya ‘Capital Cup’ ambapo timu kubwa kama Manchester United inaweza kwenda kucheza kiwanja kidogo cha ‘Community’ kinachomilikiwa na Colchester kikibeba watazamaji 10,105 tu na soka likachezwa bila ubishi. Sawa tu na Liverpool ikisafiri hadi kwenye uwanja unabeba watu 11,582 uitwao ‘Priestfield’ unaomilikiwa na timu ndogo ya Gillingham na soka likapigwa bila tatizo huku mashabiki wa Liverpool wakipewa tiketi zao chache na kuwaacha wana wa Gill wakijinufaisha na idadi ya viti vyao vingi!  Lakini watu wajue kuwa katika mji huo wa Colchester wapenzi wote wa soka waliopo hapo ni mashabiki wa timu hiyo na siyo mashabiki wa Machenster United. Ulaya kila timu ya nyumbani inapocheza kwake inapata sapoti kutoka kwa mashabiki wake wa eneo hilo na wala hawajagawanyika kutokana na timu chache pengine kubwa, ukienda Newcastle utawakuta mashabiki wote wa jiji hilo wanaishabikia timu ya hapo hii ni tofauti sana na hapa kwetu. Hii ni mifano mingi ambayo watu wamekuwa wakiunga mkono wito wa viongozi wa Klabu ya Azam kuitaka TFF  kuipa haki ya kucheza nyumbani dhidi ya timu zote za Ligi Kuu zikiwamo Simba na Yanga. Wanaaminisha ombi hilo kwa kutolea mifano timu za Ulaya kama Manchester United na nyinginezo. Binafsi nadhani bado Tanzania hatujafikia ustaarabu huo walionao wenzetu, hivyo mchezo wa Azam dhidi ya Simba au Yanga kuchezwa kwenye uwanja wa Chamazi unaokadiriwa kuchukua watazamaji wasiozidi 8,000 kwangu naiona hatari ya uwingi wa watu kujazana Chamazi kuzitafuta nafasi 5,000 ni mkubwa na sijui wale 20,000 watakaobaki nje mtawapeleka wapi?  Tunakumbuka uharibifu mkubwa uliofanywa kwenye Uwanja wa Taifa pale Yanga ilipocheza dhidi ya TP Mazembe na watazamaji kuingia bure. Ile kazi kubwa waliyopewa wanausalama kulinda au kuzuia watazamaji ilivyokuwa ngumu. Hata pale milango ilipokuwa imefungwa bado hali haikuwa salama, sijui watu hawalioni hilo?  Wale wanaosema tiketi zitolewe kadhaa kwa mashabiki wa Simba ama Yanga mashabiki gani hasa, nani atawakataza wanaotoka Bagamoyo, Tandale, Ubungo na wasifike Chamazi kwa kigezo gani.

Tukumbuke kuwa Azam ni moja kati ya timu kubwa Tanzania na michezo yake dhidi ya Simba au Yanga imekuwa ikivuta hisia kubwa kwa wapenda soka ambao wote hutaka kwenda uwanjani kuangalia na si vinginevyo. Tusifanye majaribio  yatakayotuletea majuto baadaye.