JICHO LA MWEWE: Ngoja nimsaidie kazi Mkwassa kwa hili hapa

Muktasari:

Wiki chache zijazo tutacheza na Algeria Uwanja wa Taifa. Kwa lugha rahisi, wiki chache zijazo Taifa Stars itakuwa inacheza na timu bora zaidi ya taifa barani Afrika

RAIS wa TFF, rafiki yangu sana, Jamal Malinzi ametangaza Kamati ya ushindi ya TFF. Itaongozwa na rafiki yangu mwingine anaitwa Farough Baghozah. Ni wakati wa kujaribu mipango mingine ya ghafla ili mradi tujaribu kutimiza ndoto za kucheza Kombe la Dunia 2018 pale Russia.

Leo sitafanya kazi ya Faroukh. Nitajaribu kufanya kazi ya benchi la ufundi. Kazi ya kuwafanyia uskauti kwa timu ya taifa ya Algeria. Wakati mwingine timu za Tanzania zinafungwa kirahisi kwa sababu ya kushindwa kuelewa nguvu ya maadui.

Wakati mwingine, timu za Tanzania zinasajili wachezaji wabovu wa kigeni kwa uvivu tu wa kushindwa kutuma watu wa kufanya uskauti huko waliko kabla hawajatumiwa tiketi kuja nchini.

Wiki chache zijazo tutacheza na Algeria Uwanja wa Taifa. Kwa lugha rahisi, wiki chache zijazo Taifa Stars itakuwa inacheza na timu bora zaidi ya taifa barani Afrika. Si wakati wa kuwatisha wachezaji wetu wala kumtisha Kocha Charles Boniface Mkwassa lakini ni wakati wa kuambiana ukweli.

Haikuwa bahati mbaya Algeria kuwa hapo ilipo. Algeria ya sasa inatengenezwa na kizazi cha wachezaji mahiri sana. Achana na habari ya wachezaji wa Afrika Magharibi wanaokuja nchini kucheza na Taifa Stars huku wakihofia miguu yao, Algeria ina wachezaji wanaojituma sana.

Kuna huyu mtu anayeitwa Riyad Mahrez anakipiga Leicester City Ligi Kuu ya England. Huyu jamaa ni hatari sana. Kwa sasa anatakiwa na Arsene Wenger wa Arsenal na Luis Enrique wa Barcelona. Katika mechi nne za kwanza tu Ligi Kuu England msimu huu ameshatupia mabao manne. Kwa sasa ana mabao matano na anashika nafasi ya tatu kwa ufungaji England.

Riyad ni mwepesi, ana kasi, ana jicho la lango, anacheza kitimu, ana uwezo binafsi. Ni kama ilivyo kwa wanasoka wengi wa Algeria wa sasa, amezaliwa Ufaransa na kukulia Ufaransa. Anahitaji jicho maalumu na si kuilinda timu kama timu. Unahitaji umaalumu kwake.

Kuna huyu mwingine anaitwa Yacine Brahimi. Huyu ni hatari sana. anatakiwa na klabu kubwa duniani. Yupo Porto na anatisha sana katika Ligi ya Mabingwa. Anacheza winga ya kushoto na Shomari Kapombe atakuwa na kazi ngumu sana Dar es Salaam na Algiers.

Kama ilivyo kwa Riyad, Brahimi amezaliwa Ufaransa. Kazaliwa Paris na amekulia katika chuo maarufu cha soka cha Ufaransa ambacho wamepitia mastaa wakubwa wote wa Ufaransa, Clairefontaine.

Kuna mtu Sofiane Feghouli ndiye roho ya eneo la kiungo la Valencia pale La Liga. Ni mtu hatari na anahitajika na klabu kubwa za Ulaya ikiwemo Barcelona ambayo inamwona kama mbadala wa Xavi Hernandez. Katika siku za karibuni imesemwa kuwa Tottenham inaongoza katika mbio za kumwania.

Feghouli ambaye amezaliwa Levallois-Perret, Ufaransa ni kiungo wa kazi. Ana ubora katika kukaba na kusambaza mipira. Ana uwezo wa kucheza kama winga au kiungo mshambuliaji. Ana matumizi makubwa ya nguvu na akili.

Kuna jamaa anaitwa Islam Slimani anakipiga Sporting Lisbon ya Ureno. Huyu jamaa mwaka 2013 alikuwa mwanasoka bora wa Algeria. Ni mkali sana katika kufunga. Alizaliwa pale pale Algiers na anashika nafasi ya nane kwa ufungaji katika historia ya timu ya taifa ya Algeria.

Unamkumbuka Baghdad Bounedjah? Alikuja hapa na kikosi cha Etoile du Sahel ya Tunisia kukipiga na Yanga na aliwatisha sana Yanga kwa umbo lake kubwa. Bado anacheza Afrika lakini katika nchi jirani ya Tunisia.

Eneo la kiungo pia kuna mtu anaitwa Nabil Bentaleb anayekipiga Tottenham Hotspurs. Bentaleb ni miongoni mwa viungo roho wa Tottenham kwa sasa kutokana na soka lake maridadi ambalo wakati mwingine linamfanya afananishwe na Zinedine Zidane. Labda pia kwa sababu na yeye amezaliwa Ufaransa.

Kuna mastaa lukuki ambao sijawataja. Wanacheza katika timu mbalimbali Ulaya kiasi kwamba wanaweza kuanza kikosi chao wakiwa hawana hata mchezaji mmoja anayecheza ndani huku tukikumbuka kuwa timu yao USM itacheza fainali za ubingwa wa Afrika na TP Mazembe.

Kwa mfumo wa Mkwasa wa kuanza na viungo wachache uwanjani kama alivyoanza na Said Ndemla na Himid Mao tu katika pambano dhidi ya Malawi Dar es Salaam, basi Taifa Stars itateseka sana. Ni ngumu sana kupishana na Algeria kwa sababu hata katika Kombe la Dunia, mabingwa Ujerumani waliteseka sana kwa hawa jamaa katika mechi ya mtoano pale Brazil.

Kama ningekuwa kocha wa Stars ningeuchagua mfumo wa 4-5-1 na kujaza viungo wengi kwa ajili ya kudhibiti zaidi hasira za Waarabu hawa kuliko kujifanya tupo nao katika kiwango kimoja na tunaweza kucheza nao. Tunaweza kuwatoa, lakini tunahitaji wachezaji wenye roho za paka kwa dakika zote 180 hasa pambano la Algiers.