NINAVYOJUA : Namwona Pogba kama pundamilia ndani ya swala

Muktasari:

  • Ilikuwa si kawaida kuwaona wachezaji wenye viwango vya dunia wakitiririka kutafuta marisho England, haikuwezekana! Hata wale Wabrazili walioingia England miaka ya 1990 na kuelekea huku walikuwa ni Wabrazili wanaocheza soka lisilo na mvuto miguuni mwao, walikuwa ni Waajentina wasiokuwa mafundi kama kina Gabriel Henzie, Gilberto Silva na wengineo lakini wale mafundi wa ukweli ilikuwa si rahisi kuwakuta England, hao utawakuta kwa wingi Italia, Hispania, Ujerumani na Ufaransa kwa nini!

MIAKA ya 2000 kurudi chini ilikuwa ni vigumu kuwaona wachezaji zaidi ya watatu wanaotoka Brazil ama nchi yoyote ya Amerika ya Kusini ambao kwa muda huo walikuwa ni wachezaji wanaochezea timu zao za taifa, kuwapo ndani ya Ligi Kuu ya England wakizichezea Arsenal, Chelsea, Manchester United na nyinginezo.

Ilikuwa si kawaida kuwaona wachezaji wenye viwango vya dunia wakitiririka kutafuta marisho England, haikuwezekana! Hata wale Wabrazili walioingia England miaka ya 1990 na kuelekea huku walikuwa ni Wabrazili wanaocheza soka lisilo na mvuto miguuni mwao, walikuwa ni Waajentina wasiokuwa mafundi kama kina Gabriel Henzie, Gilberto Silva na wengineo lakini wale mafundi wa ukweli ilikuwa si rahisi kuwakuta England, hao utawakuta kwa wingi Italia, Hispania, Ujerumani na Ufaransa kwa nini!

Huko walifuata soka lenye mpangilio na linalotazamika linalotoa burudani, wao kwao kwanza ilikuwa burudani na kisha ushindi, Wabrazili wa kipindi kile walikuwa wakifuata soka zuri na siyo pesa! Ndio maana ilikuwa vigumu kwa Sir Alex Fergurson kumpata Ronaldinho Gaucho pamoja na pesa yote kubwa aliyotaka kutoa, ikawa vigumu pia kwa Manchester City kumpata Ricardo Kaka pamoja na pesa nyingi waliyokuwa wamepanga kumpa. Bado yeye binafsi aliichagua Real Madrid kwa kuwa alitaka kwenda kucheza soka analolitaka huku akijilinganisha kiwango chake na cha wale anaotaka kwenda kucheza nao.

Miaka inakwenda kwa kasi sana, hivi sasa Ligi Kuu ya England imeanza kuvutia sura nyingi za wachezaji wenye viwango vikubwa wanaotoka kwenye nchi zenye ubora wa dunia. Ukienda Arsenal utawakuta Wajerumani, Mesut Ozil na Per Mertesacker wenye viwango vikubwa kina Hector Bellerin, Alexis Sanchez na wengineo ukienda Man City na Chelsea utawakuta wachezaji waliokataa kwenda timu kubwa duniani kama Barcelona na Real Madrid na badala yake wakatua Uingereza kama Diego Costa, Sergio Aguero, Nolito na kadhalika ambao kwa sasa huwaoni wakifuata soka zuri, bali wanatafuta marisho bora, wamefuata pesa ndefu wanayolipwa nchini England. Bado kwenye ingizo hili kuna rundo la makocha bora duniani wenye rekodi kubwa walioamua kuingia nchini humo wakiongozwa na Pep Guardiola, Jurgen Klopp, Antonio Conte, Jose Mourinho na wengineo. Hawa wote wanaifanya Ligi Kuu England kuanza kupata sura tofauti.

Hayo yote tisa kumi ni ujio wa wachezaji ghali na bora kwa sasa, Paul Pogba na Zlatan Ibrahimovic ndani ya kikosi cha Manchester United ! Ukiwaangalia kwa makini wachezaji huwa ndani ya michezo michache waliyocheza utaona jinsi walivyojitofautisha kwa uwezo na wachezaji wenzao wengi kuanzia wale wanaocheza nao hadi wa timu pinzani. Kila hatua waliyokuwa wakiifanya iliwaonyesha kuwa na viwango tofauti na vya kina Wayne Rooney, Marouane Fellaine, Chris Smalling na wengine waliokuwa nje. Kila nyendo aliyokuwa akiifanya mfano Paul Pogba ilikosa mchezaji mwenye muono kama wake wa kumpa sapoti ya namna gani wanatakiwa kulifikia lango la wapinzani kirahisi. Yale madoido mengi ya kwake nayaona kama vile ni mageni kwenye Ligi Kuu England na kwenye timu yake pia. Nakiona kiwango chake kama vile alitakiwa kucheza kwenye kikosi cha maajabu cha Manchester United cha 1999 hadi kuishia 2010. Kwenye kikosi cha sasa unawaona wachezaji hawa wakipwaya sana na kuwafanya wahangaike kutafuta wachezaji watakaojuwana nao vizuri. Namuona Pogba akiwa ndani ya kundi tofauti kiasi na hiki ndicho kitu kinachoweza kuzitofautisha timu kubwa za England za Manchester United, Chelsea, Man City, Liverpool na timu kubwa za Hispania za Barcelona na Real Madrid na ile ya Ujerumani kama Bayern Munich na nyinginezo, ambazo ukimweka Pogba ndani yao unaweza usimtambue mara moja kwa sababu wapo wachezaji wengine watakaokupa ubora wa kumzidi.

Watakupa vionjo vingi vinavyoweza kumpoteza Pogba na akaonekana wa kawaida ndani ya timu, lakini kwa England mara unapoiona Manchester United licha ya tofauti yake kimuonekano bado atakapogusa mpira tu utaiona tofauti na wachezaji wengine hususan wa Kiingereza.

Hiki ndicho kitu kinachosaidia na kuifanya timu hata ya Taifa ya Uingereza kukosa mafanikio kimataifa kwa kuwa ligi yao ambayo wachezaji Waingereza wengi wanacheza na hawataki kutoka nje. Hawazalishi wachezaji wa Kiingereza walio bora wenye uwezo na viwango vya kimataifa. Wanapata sifa nyingi wakiwa ndani ya ligi yao kwa sababu watu wanalinganisha mchezaji mmoja mmoja tu wa ndani ya ligi ya England badala ya kuwalinganisha na wachezaji wanaocheza ligi za nje! Tatizo watu hawataki kutoka nje kuwapa uzani sawia na wengine wanatoa rekodi nyingi zinazomhusu mchezaji wa Kiingereza kwa matukio ya ndani tu huku wakishindwa kuwapa ubora wa kimataifa. Kundi la swala linaweza kuwa kundi la timu nyingi tu za ndani ya Uingereza lenye wachezaji wengi wa Kiingereza wanaocheza kila siku wao kwa wao na hawawezi kutoka nje.

Hata wakitoka bado hawatoi ushindani wa dhati kwa sababu hawana kina Pogba wa kutosha. Pogba huyu aliyeshindwa kuingia kwenye kikosi bora cha wachezaji wa Ulaya mwaka huu ndiye anayeweza kuonekana bora ndani ya EPL msimu huu.