NINACHOKIAMINI: Serikali haitaki Simba, Yanga zichukuliwe na watu binafsi

HAKUNA jambo ambalo linatisha watu kama mabadiliko. Iwe ni mabadiliko ya uongozi serikalini, kwenye taasisi au sehemu yoyote, watu wengi huwa na hofu kubwa.

Kwa kawaida binadamu hupenda kuishi maisha aliyoyazoea, au kuishi katika mfumo fulani wa siku zote na ndio maana huwa anakuwa mbishi kunapokuwa na mabadiliko.

Katika jambo ambalo limefanya taasisi nyingi kutopiga hatua au kushindwa kuendelea ni kuwa na wafanyakazi ambao wamefanya kazi muda mrefu.

Wafanyakazi ambao wamefanya kazi muda mrefu huwa wabishi, hawataki mabadiliko na mara nyingi huwa ni kikwazo kwa taasisi nyingi katika kupiga hatua kiamaendeleo.

Na ndio maana makampuni mengi duniani siku hizi yanaajiri vijana chipukizi ambao, hawana uzoefu ili wakalete mapinduzi katika taasisi hizo.

Inahitaji kuwa na fikra chanya ili kuleta mabadiliko mahali popote, vinginevyo mabadiliko yanaweza kulazimishwa, lakini watu wakayakataa na yakashindwa.

Serikali za Kusini mwa Jangwa la Sahara zimekuwa makini sana inapofika suala la mabadiliko. Viongozi wengi wa serikali huogopa mabadiliko yoyote, hudhani yanatishia utawala wao.

Ukiangalia suala la mabadiliko ya uendeshaji ambayo Simba na Yanga wamepanga kuyafanya utagundua kuwa serikali haipo tayari katika hilo.

Ukisikia kauli anayoisema Katibu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Mohammed Kiganja utagundua kuwa serikali haitaki mabadiliko ya uendeshaji wa Simba na Yanga.

Amekuwa akitumia lugha laini kuwa klabu hizo zifuate taratibu ikiwa ni pamoja na kubadilisha katiba kabla ya kufikia kufanya mabadiliko.

Lakini, kuna kauli ambayo amekuwa akiirudia mara kwa mara kuwa, ‘wanaozitaka Simba na Yanga waanzishe timu zao’.

Kama anasema klabu hizo zifuate utaratibu wa kubadilisha Katiba, ni kwanini anarudia mara kwa mara kuwa ‘wanaozitaka Simba na Yanga waanzishe klabu zao.’

Katibu wa BMT si mtu mdogo, ni mwakilishi wa serikali, anachokisema si kitu cha kukidharau hata kidogo.

Ingawa amekuwa akisema katiba zibadilishwe, utagundua kuwa hata kama mabadiliko hayo yatafanyika Simba na Yanga zitaendelea kuendeshwa kwa mfumo wa sasa, ambao umekuwa kikwazo kwao.

Wiki iliyopita, Kiganja alisema kwa wanaotaka kufanya mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hizo, wakasome historia ya Uhuru wa Tanganyika, waone mchango wa klabu hizo.

Ingawa hataki kusema moja kwa moja, Kiganja anataka kusema kuwa klabu hizo zitaendelea kuwa za wanachama na haziwezi kupewa mtu mmoja au kundi la watu wachache kuziendesha ama kuzimiliki.

Jambo la kushangaza ni kuwa serikali huwa haitoi fedha wala ruzuku kwa klabu hizi ili zijiendeshe. Zinaendeshwa kwa fedha za watu binafsi, zinaendeshwa kwa kutegemea mapato kidogo ya mlangoni na michango ya wafadhili.

Kwa miaka 80 ya klabu hizi, klabu hizi mbili zinatakiwa ziendeshwe kwa mfumo ambao upo duniani kote. Kama si hisa basi hata kuuzwa kama zilivyofanya klabu nyingine duniani.

Ni rahisi mtu kusema mazingira yetu ni tofauti, lakini anasahau kuhoji inapofika kutoa fedha mazingira huwa ni yaleyale tu.

Ukitaka kujua kuwa ni vigumu kwa mabadiliko katika klabu hizi mbili, angalia Yanga ilipotumia nguvu kubwa kufanya mabadiliko mwanzoni mwa miaka ya 2000, bila mafanikio.

Yanga Kampuni ilipigwa vita kila mahali kiasi kwamba, wazee waliokuwa wameanzisha kundi la Yanga Asili wakaonekana ndio washindi baada ya kukwamisha mambo.

Unaposikia kauli ya Kiganja akisema wanaotaka klabu hizo waanzishe klabu zao unaona kabisa serikali haitaki mabadiliko ya uendeshaji.

Yanga na Simba watafanya mabadiliko ya katiba, lakini sidhani kama hilo tu linatosha, kwa sababu serikali imeshaamua kuwa haitaki mabadiliko.

Na kwa sababu haitaki mabadiliko, tusitarajie kuona soka letu likikua hasa ikizingatiwa kuwa kwa sasa mchezo huo ni biashara kubwa duniani na lazima fedha ziwekezwe kwanza ndipo mafanikio yafuate.