Mzee akilimali, kiungo mahiri mkabaji tumpe na mbinu za kufunga

Muktasari:

Yeye na wenzake kwa sasa wapo katika mapambano kwelikweli dhidi mwenyekiti wa sasa wa Yanga, Yusuf Manji, ambaye tusisahau kwamba ni mtu tajiri sana. Ni pambano la kuvutia kati ya Daud na Goliath. Mwisho wake unatabirika sana.


NAPENDA kumsikiliza Mzee Akilimali. Kwa nini nisipenda kumsikiliza? Kila siku ana kitu kipya ambacho kinafunika hata mchezo wenyewe ndani ya uwanja. Napenda jinsi ambavyo haelewi sana kinachoendelea ndani ya uwanja lakini ni mtaalamu wa fitina anayeweza kuyumbisha vichwa vya watu wengi.

Yeye na wenzake kwa sasa wapo katika mapambano kwelikweli dhidi mwenyekiti wa sasa wa Yanga, Yusuf Manji, ambaye tusisahau kwamba ni mtu tajiri sana. Ni pambano la kuvutia kati ya Daud na Goliath. Mwisho wake unatabirika sana.

Ninapowasikiliza kina Mzee Akilimali navutiwa na hoja zao. Yupo na Jemedari wake anaitwa Salum Mkemi. Hoja zao wanazipangilia vizuri sana. Ninapomsikiliza Manji na watu wa upande wake navutiwa na hoja zao za kuitoa Yanga kutoka ilipo kwenda kwingine.

Kinachonikera kutoka katika upande wa kina Mzee Akilimali ni kwamba wanatumia muda mwingi zaidi kufafanua hoja za kuzuia kuliko kuonyesha nia ya wapi tunapaswa kwenda. Kifupi, Mzee Akilimali anaongoza katika kundi la watu ambao wanazuia Manji asikodishwe Yanga kuliko kuonyesha nini kifanyike. Binafsi nina matatizo na pupa ambayo Manji anaitumia kutaka kuichukua Yanga. Nina matatizo pia na mfumo anaotaka kuutumia kukodisha timu. Nashangaa pia kuwaachia Yanga majengo halafu akaitaka timu peke yake. Nashangaa pia kuendelea kuwa mwenyekiti wa timu halafu hapo hapo akawa mwekezaji mkubwa. Tutapimaje faida na hasara?

Yote haya na mengineyo ambayo kina Mzee Akilimali wanayafafanua yanaweza kuwa matatizo. Ni kama ambavyo Simba wana matatizo na asilimia 51 ambazo Tajiri Mohamed Dewji anataka apewe. Pamoja na matatizo haya ya kimifumo, bado hakuna haja ya kurudi nyuma.

Simba na Yanga haziwezi kurudi nyuma licha ya changamoto nyingi zilizopo katika mchakato unaoendelea kwa sasa. Inawezekana Manji na Mo wasipewe timu lakini bado haimaanishi tuendelee kubaki katika mfumo uliooza wa sasa ambapo klabu hizi zinaishi katika ujima.

Hatuwezi kuendelea kuwa na wenyeviti wa hiyari, hatuwezi kuendelea kuwa na klabu ambazo hazifanyi biashara, hatuwezi kuendelea kuwa na klabu zinazotegemea hisani za watu. Hatuwezi kuendelea kuwa na klabu ambazo hazina viwanja vya kisasa vya mazoezi.

Kina Mzee Akilimali wanaweza kuwa sahihi katika madai yao, lakini pia waje na majibu sahihi kuhusu namna inavyoweza kuendeshwa kisasa na kwa faida kubwa tofauti ilivyo sasa. Kukaba bila ya kushambulia haisaidii sana.

Naamini nyuma ya Mzee Akilimali kuna watu wazito ambao hawampendi Manji na hawapendi kujiingiza moja kwa moja katika vita ambayo wanahisi wanaweza kushindwa mbele ya safari. Lakini nawakumbusha watu hawa wampe Mzee Akilimali hoja ambazo zitaelezea namna ambavyo Yanga inaweza kuwa.

Tunaishi katika nchi ambayo kila mtu analalamika bila ya kutoa suluhisho. Hili ni tatizo kubwa kwetu. Simba na Yanga haziwezi kubaki hivi kwa miaka yote. Imetosha.

Vyombo vya habari navyo vimeingia katika ushabiki mkubwa wa suala hili. Kinachonisikitisha ni kwamba waliojiingiza katika huu mgogoro wanashindwa kuelimisha njia mbadala ya nini kinaweza kufanyika kuziondoa Simba na Yanga hapa zilipo. Hilo ni la msingi zaidi. Vinginevyo na wao wanajiingiza katika kazi ya Mzee Akilimali ya kukaba bila ya kushambulia. Mamlaka husika nazo zinatajwa kuzuia mchakato uliopo. Serikali inavumishwa kukataa mfumo unaosakwa na kina Manji. Sina tatizo. Tatizo langu ni kwamba watupe mfumo mbadala na wa kisasa ambao utaendana na dunia ya soka ya leo. Nazitazama Simba na Yanga kama klabu zinazopoteza mamilioni ya soka kila jua linapozama. Kuna mfumo gani utaokoa haya? Ni kweli wanachama wa sasa wanaokwenda katika ukumbi wa mikutano na kumchagua mwenyekiti anayeendesha timu kwa mapato ya mlangoni ndio linabakia kuwa suluhisho la matatizo ya Simba na Yanga? Tupo katika dunia ya ubepari lakini mwenyekiti anachaguliwa kwa ajili ya kuiongoza klabu katika mfumo wa kijamaa. Leo una timu kama Simba na Yanga halafu unaziongoza kwa ajili ya faida ya furaha ya ushindi tu bila kujipatia pesa yoyote. Hii ilikuwa fasheni ya zamani wakati wa ujima. Tusirudi nyuma. Hata kama Manji na Mo wasipopewa timu, lakini tusirudi nyuma. Klabu haziwezi kuendeshwa na maskini tena kwa msingi wa furaha. Klabu haziwezi kuongozwa na watu ambao hawasaki faida katika timu. Tuanzie hapo wakati tukiendelea kulumbana.