Mzee Kilomoni anaponiongezea maajabu ya mwaka 2016

Muktasari:

Kinachoumiza si mambo hayo ya kushangaza, jambo ambalo linaumiza ni jinsi ambavyo watu wanayaona mambo hayo kuwa ya kawaida.

VITUKO havijawahi kuisha katika nchi hii. Kila kukicha utasikia jambo limetokea mahali fulani, utashangaa halafu utaendelea na shughuli zako.

Kinachoumiza si mambo hayo ya kushangaza, jambo ambalo linaumiza ni jinsi ambavyo watu wanayaona mambo hayo kuwa ya kawaida.

Inashangaza kuona majambazi yanateka mtaa mzima na kufanya uhalifu kwa saa mbili tena katika jiji kubwa kama la Dar es Salaam, na hakuna anayeshangaa.

Siku ya pili maisha ya watu yanaendelea kama kawaida kana kwamba siku iliyopita hakukuwa na utekaji wa majambazi uliofanyika.

Dunia inakoelekea inanishangaza kwa sababu mambo ya kutisha na kustaajabisha yanatokea, lakini hakuna anayeonekana kushtuka. Maisha yanaendelea kama kawaida.

Umefika Lagos? Mtu anaweza kugongwa na gari, akabaki pekee yake barabarani mpaka anakufa, hakuna mtu anayejali. Kila mtu anaendelea na shughuli zake utadhani hakuna jambo ambalo limetokea.

Dar es Salaam haiko mbali sana na mfano kama huo wa Lagos, mambo yanatokea ya kustaajabisha, hakuna anayejali.

Vitoto vinabakwa mitaani mpaka kufariki dunia, hakuna jirani anayesaidia au kujali. Kila mtu yupo bize na maisha yake.Nini kimetokea?

Kuna tatizo kubwa limetokea. Maisha yamewafanya watu kuwa na msongo wa mawazo, na ili kupunguza msongo huo wa mawazo hakuna mtu anataka kutafuta matatizo ya watu wengine. Kila mtu kaamua kubaki na maisha yake.

Kiongozi anaweza kumuabisha mtumishi wa umma kwenye mkutano, na hakuna mtu anayejali, kila mtu anaendelea na shughuli zake.

Katika nchi ambazo zimeendelea, kiongozi anapomdhalilisha mtumishi wa chini yake huwa haachwi hivi hivi, angechukuliwa hatua hata kujiuzulu, lakini kwetu hakuna anayejali kwa sababu kila mtu anaangalia mkate wake.

Ndiyo maana unaposikia kauli ya miongoni mwa wadhamini wa Simba, Hamis Kilomoni kutaka kuzuia mkutano wa klabu hiyo, unarudi kulekule kukutana na mambo ya kustaajabisha.

Sijui kama Kilomoni anajua majukumu ya wadhamini? Kama alikuwa hajui, kazi kubwa ya wadhamini ni kusimamia mali za klabu.

Hana mamlaka ya kuzuia mkutano ambao unaitishwa kikatiba. Hana mamlaka ya kupingana na Ibara ya 20 na 22 ya Simba ambayo kwa kifupi inazungumzia kuhusu mikutano na kwamba Rais akishirikiana na kamati ya utendaji ndio wenye mamlaka.

Sina ugomvi na Kilomoni anapotaka Takukuru kuchunguza fedha za usajili wa Emmanuel Okwi, kwa sababu kazi ya bodi ya wadhamini ni kusimamia mali za Simba.

Lakini Kilomoni ameniongezea mambo ya kustaajabisha kwa kutaka kuzuia mkutano wa kujadili mabadiliko ya klabu hiyo Desemba 11.

Kwa sababu Kilomoni ni mwanachama wa Simba, asiwe na wasiwasi, kama hataki mabadiliko hayo aende katika mkutano huo, atoe hoja zake, ashawishi na wanachama wengine ili wakatae mabadiliko hayo.

Uamuzi wa kubadilisha katiba au kuendelea nayo ya sasa, hauwezi kufanywa na bodi ya wadhamini ya Simba, uamuzi huo hufanywa na mkutano mkuu wa wanachama.

Bodi ya wadhamini wa Simba wamekasimishwa madaraka ya kusimamia mali za klabu hiyo ya Msimbazi, si kuzuia mkutano. Hawana ubavu huo.

Tena mbaya zaidi wanaomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam azuie mkutano. Kwanini wanakimbilia huko wakati kuna polisi au msajili wa vyama vya michezo na klabu au hata TFF.

Mwaka huu, kuna mambo mengi yamenishangaza, lakini yamepita hivi hivi, nadhani Kilomoni naye ameniongezea jambo la kushangaa mwaka huu.

Ifike pahala Watanzania tujifunze namna ya kufahamu mipaka ya mamlaka tulizopewa na kufanya mambo yetu katika mipaka hiyo. Kama ni kiongozi wa klabu basi ufahamu mipaka yako.

Kama hawa kina Kilomoni na wenzake wangekuwa wanafahamu mipaka yao pengine wasingefanya haya. Pengine Kilomoni angesubiri mkutano mkuu ili aweze kutoa hoja zake na siyo kuzuia mabadiliko.