Mwakyembe anzia hapa ili usikwazike

Muktasari:

Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo sasa ni Dk. Harrison Mwakyembe, aliyeteuliwa juzi Alhamisi asubuhi.

Filamu inaendelea. Ndivyo ninavyoweza kusema baada ya mengi kutokea katika wiki ya mabadiliko ya kiuongozi nchini.

Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo sasa ni Dk. Harrison Mwakyembe, aliyeteuliwa juzi Alhamisi asubuhi.

Mwakyembe anachukua nafasi iliyoachwa na Nape Nnauye aliyetenguliwa juzi hiyo asubuhi akiwa Arusha kikazi.

Nnauye, ambaye ni Mbunge wa Mtama, alitenguliwa kwa kile kinachodaiwa ni sakata la uvamizi wa Clouds Media na uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Machi 21.

Kwa kipindi ambacho Nape amekuwa madarakani katika wizara hiyo, kuna mambo mengi yaliyokuwa ya mafanikio kwake.

Hilo linaweza kuwa pigo kwa tasnia ya michezo na burudani hasa kwa wale ambao walikuwa wamezoea jinsi ya kufanya kazi naye.

Lakini tunaweza kuzungumza mengi tukabishana, ila Mwakyembe, ambaye ni Mbunge wa Kyela ana changamoto kubwa, hasa kufanya kazi na waandishi wa habari.

Kubwa ambalo kwa sasa anatakiwa kuanza nalo kabla ya kuangalia changamoto nyingi zilizopo katika wizara yake, ni jinsi ya kufanya kazi na waandishi ambao ndio daraja.

Unaweza kubisha, lakini ukweli ndio huo, anaweza kuanzia pale katika mkutano wa mwisho wa Nape na waandishi wa habari wakati mbunge huyo wa Kusini alipoonyeshwa bastola akitakiwa kurudi garini.

Imani kubwa kwa waandishi hasa wa habari za michezo wamekuwa na Nape kwa mafanikio, na kilichotokea ni kuhisi kuonewa.

Inawezekana tukio la uharaka wake katika kuchukua hatua juu ya tukio la uvamizi likahusika au la, ila jinsi waandishi walivyokuwa pamoja na Nape, imekuwa simanzi kwao.

Kwa mapokeo ya waandishi katika mkutano wa Nape, unaweza ukawa na picha yenye maana kwa Mwakyembe katika kufanya majukumu yake kwa amani na kutambulika uwepo wake.

Kuna watu wanataka tu kubisha hilo siwakatazi, lakini kwa mwenye akili timamu anaweza kuisoma mioyo ya waandishi wa habari, ambao wamesusia kufanya kazi na Makonda.

Jukwa la Wahariri Tanzania (TEF) lilitoa kauli ya kutofanya kazi na mkuu huyo kutokana na kile alichokifanya Clouds.

Lakini lililotokea wakati waziri akijaribu kutafuta haki na kuenguliwa ghafla limeacha kitu kwa waandishi na Mwakyembe asipolielewa hilo ataukumbuka huu ukurasa.

Sina tatizo na Mwakyembe kwa upande wangu, lakini najua hata yeye anaweza kuwa na kitu kichwani juu ya waandishi kwani si yeye aliyejiweka katika nafasi hiyo na hahusiki kwa kuondoka kwa Nape.

Mwakyembe najua una mambo mengi ya kusimamia katika wizara yako mpya, hilo ndilo jambo la msingi zaidi katika nafasi yako, lakini angalia hili, linaweza kuwa daraja. Mimi nimemaliza.