MACHO MANNE: Mavugo achana na presha utachemka mapema

Muktasari:

  • Mavugo alitua Simba kwa kuvutiwa na uungwana ulioonyeshwa na viongozi wa Simba, pale alipoenda kufanya majaribio Ufaransa huku akiwa tayari ameshakula chao, huku viongozi wa klabu hiyo kutoonyesha nia ya kumshtaki kwa utapeli.

HAKUNA asiyejua kuwa, Simba inafanya vizuri kwa sasa hasa katika mechi zake nne za mwanzo za msimu wa Ligi Kuu Bara unaoendelea, ikizoa pointi 10. Hata hivyo, mashabiki wengi wa timu hiyo macho na masikio yao ni kuona straika wao Laudit Mavugo akitupia kila mechi.

Mavugo raia wa Burundi amesajiliwa na Simba msimu huu, japo alikuwa akishubiriwa kwa hamu tangu mwaka jana ila alishindwa kujiunga kutokana na uongozi wa timu yake ya Vital’O kumwekea ngumu kutokana na kuwa na mkataba naye kipindi hicho.

Mavugo alitua Simba kwa kuvutiwa na uungwana ulioonyeshwa na viongozi wa Simba, pale alipoenda kufanya majaribio Ufaransa huku akiwa tayari ameshakula chao, huku viongozi wa klabu hiyo kutoonyesha nia ya kumshtaki kwa utapeli.

Alipotua Msimbazi kila mmoja alitaka kumuona Mavugo anafanya nini uwanjani kutokana na historia yake ya Burundi alipotwaa kiatu cha dhahabu kwa misimu miwili mfululizo akiisaidia hata timu yake kubeba taji la ligi na michuano mbalimbali.

Ukiangalia mechi za Simba na ukiwafuatilia mashabiki wa klabu hiyo na hata timu pinzani humwangalia Mavugo anafanya nini uwanjani kwa kila hatua anayogusa mpira.

Anaposhindwa kufunga muda mwingine inakuwa ni shida kwani huwa wanamuona bado kiwango chake si kile walichokitarajia.

Mchezaji huyo amekuwa akiingia uwanjani muda mwingine akiwa na presha kubwa kutoka kwa mashabiki, akijenga hofu kwamba endapo akishindwa kufunga watamchukuliaje na kujikuta akishindwa kufanya yake kwa ufanisi.

Msimu ndio kwanza umeanza, Mavugo anapaswa kutuliza akili ili aweze kuonyesha uwezo wake halisi na mambo mengine yatafuata baadaye. Hapaswi kuendeshwa na presha za mashabiki kwani zinaweza kumvuruga zaidi.

Kuna wakati Mavugo anaonekana uwanjani akitaka kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja na mwishowe kuharibu kwa sababu tayari inaonekana amekubali presha ya mashabiki wanaotaka kumuona akifanya mambo kama malaika uwanjani.

Ukiachana na hofu aliyonayo, pia ila bado straika huyo ana tatizo la mazingira, Mavugo bado hajazoea vizuri mazingira ya soka la Bongo, viwanja tatizo ambalo aliliweka wazi kuwa linamsumbua kwani viwanja vya hapa ni vizuri kuliko vya kwao, timu kuozeana yaani kucheza kitimu kutokana na wachezaji wengi kuwa wapya huku kocha pia akiwa mpya ambaye amekuja na mfumo wake.

Hivyo basi, Mavugo hapaswi kuuruhusu moyo wake kuingiwa na hofu anaposhindwa kufunga kwenye mechi.  Lazima ajiamini  na kujua kuwa akishindwa leo basi kesho ataweza.

Kama hatafanya hivyo, ategemee kuendeshwa puta na mashabiki ambao wao akili zao ni kutaka matokeo mazuri bila kujua timu na wachezaji wao wanacheza na wenzao ambao nao wanataka matokeo mazuri kama wao.

Nimshauri tu Mavugo asiifanye miguu yake ikishika mpira ipigwe na shoti ya umeme kwa maneno ya mashabiki na kujikuita akibutuabutua tu uwanjani jambo ambalo litamfanya ashindwe kukaa Msimbazi kwa muda aliojiwekea.

Atulie, afuate maelekezo ya kocha wake, atoe ushirikiano kwa wenzakeili nao wampe ushirikiano na kuifanya Simba iwe na mafanikio ya wachezaji wote.  Kelele za chura hazimzuii tembo kunywa maji. Akishindwa kufunga katika mchezo mmoja, afunge mwingine.