MICHARAZO: Mastaa wetu wasiige ushangiliaji au mitindo ya nywele tu!

BAADA ya mapumziko ya wikiendi, tumerudi tena kazini kuanza mihanjo ya wiki nyingine mpya. Asikuambie mtu jinsi mambo yalivyobana, kwa sasa ni rahisi kutofautisha kati ya wapiga dili na wale wavuja jasho kwa ukwelikweli.

Nasikia kwa sasa hata kwenye viti virefu, hakuna tena mambo ya ‘keep change’ na mtu ukimcheleweshea chake anakufuata huko huko kaunta, jicho hilooo!

Enewei, ilikuwa wiki tamu sana kwa mashabiki wa soka la ughaibuni, kwani zile tambo na kelele za wanazi wa Mashetani Wekundu na Wapiga Mitutu, imeisha. Wanaume wametoshana nguvu, ingawa wenyeji walikuwa na nafasi kubwa ya kuibuka kidedea kama sio kubaniwa tuta na Andre Marriner.

Vijogoo wa Anfield nao sijui kiliwakuta nini baada ya kushindwa kuendeleza wimbi lao la ushindi pale kwa Watakatifu wa Southampton, ila kilichovutia ni namna Jogoo wa White Hartlane, Spurs lilipotoka nyuma na kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Wagonga Nyundo wa London.

Kwingineko, bishoo Cristiano Ronaldo aliendeleza makali yake dhidi ya Atletico Madrid baada ya kuwapiga ‘hat-trick’, huku wababe wa Barca waking’ang’aniwa, kifupi wikiendi ilikuwa tamu katika soka la Ulaya. Hapa nyumbani kama mnavyojua, ligi ipo mapumzikoni, kinachoendelea ni vurugu za dirisha dogo la usajili na kabla ya yote nimpe pole, straika wa Vijana wa Jangwani, Malimi Busungu kwa ajali iliyomkuta eneo la Dawaka, Morogoro.

Kwa namna gari lake lilivyoharibika ilikuwa ni bahati kwake kupona na hilo ni jambo la kumshukuru Mungu, kwani ni miujiza yake imetenda kazi.

Wakati ligi ikiwa mapumzikoni ni wazi wachezaji watakuwa wanafuatilia kwa ukaribu zaidi mechi za ligi mbalimbali za Ulaya zinazoendelea.

Mapumziko hayo kwa wachezaji ni fursa nzuri ya kujifua na kujifunza kitu kipya kabla ya kuja kukionyesha kwenye duru la pili litakaloanza katikati ya Disemba, kama hakutakuwa na badiliko lolote la ratiba ya Ligi Kuu.

Kwa wajanja wanaweza kujifunza kitu wanapokuwa mbele ya runinga zao kufuatilia mechi hizo na kama vichwa vyao ni vyepesi wanaweza kurejea duru lijalo la Ligi Kuu Bara wakiwa kivingine kwa maana ya aina ya uchezaji wao.

Sio kipindi hiki tu, bali hata wakati mwingine kila wanapokuwa na nafasi nyota wetu wawe wanajifunza vitu vizuri vya kusaidia kuboresha viwango vyao vya soka na kujitengenezea nafasi za kutamba zaidi kitaifa na kimataifa.

Hivyo ndivyo vitu vya kujifunza kwenye runinga, kama unamuangalia Ronaldo anavyowaburuza mabeki wa timu pinzani na kufunga kwa madaha mbele ya makipa hodari, kwanini nyota wetu wasijifunze kitu kupitia Mreno huyo? Kama mtu anajiita Messi, vipi anashindwa kumfuatilia nyendo za Lionel Messi, nini maana ya kujibatiza jina kubwa kama uwezo wako ni mdogo?

Mastaa wetu wanaweza kujifunza mazuri na kuongeza makali yao kupitia mastaa wanaowaangalia kila wikiendi na katikati ya wiki katika mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi ya Ulaya ‘Europe League’ ama michuano mingine kibao.

Cha kusikitisha ni kwamba wengi wa mastaa wetu akili na macho yao uelekeza kwa mastaa wanaowashuhudia kwenye runinga jinsi wanavyonyoa ana kusuka nywele zao, aina ya ushangiliaji wao na upuuzi mwingine usiowasaidia.

Ndio maana unaweza kumuona mchezaji wa klabu kubwa nchini, kila wiki ana aina mpya ya mtindo kichwani mwake, lakini huoni badiliko lolote katika soka lake uwanjani na pengine wanacheza soka lao benchini ama jukwani.

Wala hawashtuki kuwekwa kwao nje ya uwanja, akili zao huwa zimeridhika na kujikita kuwa wanamitindo badala ya kucheza soka na pengine wakazama zaidi mpaka kwenye mtindo wa maisha wanaoishi mastaa wakubwa wa Ulaya. Kama wakisikia Ronaldo ana orodha ndefu ya mademu kiasi cha kuweza kuunda vikosi viwili vya timu ya soka, nao watafuata mkumbo huo, wakisikia Wayne Rooney alizamia harusini na kulewa chakari, nao watafuata nyayo hizo.

Wanachosahau ni kwamba wenzao wanaowaiga ni hodari wanapokuwa uwanjani na jezi za timu zao iwe klabu ama taifa, pia ni watu waliofanikiwa kwa kila kitu ndani na nje ya uwanja, tofauti na wao ambao hata Taifa Stars hawajawahi kuitwa tu achilia mbali kuichezea. Ndio maana Mzee wa Micharazo anawakumbusha wachezaji wetu, wajifunze mambo ya maana kwa mastaa wanaowazimikia, wasijikite tu kuiga mitindo ya nywele, uvaaji vipini aua miondoko ya kukimbia na kutembea tu. Wachezaji wetu wanapaswa kuiga ujuzi, mbinu na aina ya uchezaji soka walionao mastaa wanaowazimia na kuwa kiigizo chao ili watishe kama wanavyotisha nyota hao wa duniani.