Mambo kama haya, TFF ya Malinzi itakosolewa tu

Muktasari:

  • Rais huyo alilalama wanahabari wamekuwa wakitafuta mambo ya ovyo juu ya utawala wake ndani ya TFF kumchafua, aligusia suala la kusakamwa kwa panga pangua ya kila mara ya ratiba ya msimu uliopita bila kuzingatia jiografi ya nchi.

WIKI iliyopita kwenye hafla ya utoaji wa Tuzo za Ligi Kuu Bara msimu uliopita wa 2015-2016, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi alichukua muda mrefu katika risala yake kulalamika namna uongozi wake unavyoshambuliwa.

Malinzi alifikia hatua ya kudai wanahabari ambao ndio waliokuwa walengwa wake wakuu akiwashtumu wanavyomuandama na kumgeuza (yeye)  Malinzi kuwa kama dodoki lao la kujisafishia kwa kutengeneza habari kuponda shughuli azifanyazo.

Rais huyo alilalama wanahabari wamekuwa wakitafuta mambo ya ovyo juu ya utawala wake ndani ya TFF kumchafua, aligusia suala la kusakamwa kwa panga pangua ya kila mara ya ratiba ya msimu uliopita bila kuzingatia jiografi ya nchi.

Mwanaspoti halina lengo la kutaka kuirejea risala hiyo ya Malinzi wala kutaka kutoa ufafanuzi kama alikuwa sahihi kutumia muda mrefu kulalamika badala ya kutoa salamu kwa shughuli iliyokuwa ikifanyika siku hiyo kwenye Hotel ya Double Tree.

Lakini kwa namna baadhi ya mambo yanayoendelea kujitokeza ndani ya shirikisho hilo, tunaamini kuna kila sababu wanahabari kutonyamaza. Lazima waseme ili pengine kusaidia kurekebisha matatizo ya aina hiyo, kwa mfano juzi imetolewa taarifa juu ya sakata la wachezaji wa klabu za Namungo ya Lindi na Stand Misuna zilizokuwa zikishiriki Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) ambao walibainika walitumia majina ya mabandia tofauti kwenye michuano hiyo.

Yapo maswali mengi ambayo yanaweza kusumbua vichwa vya mashabiki wa soka juu ya usimamizi wa uongozi huo wa TFF na kamati zake hasa katika suala zima la usajili wa wachezaji.

Inafahamika katika zoezi la usajili kuna mapingamizi ya kuhakiki uhalali wa mchezaji kabla ya kuruhusiwa kucheza ligi husika, vipi wachezaji wa timu hizo waliweza kupitishwa na kucheza ligi nzima bila ya kubainika mapema?

Achana na hilo hata Kamati ya Mashindano katika maamuzi yake iliyoyatoa hivi karibuni ya kuitoza faini Namungo ya Sh 500,000 kwa kila mechi ambayo ilimtumia mchezaji mamluki, kisha kuipandisha Ligi Daraja la Pili (SDL).

Kwa hakika kituko kama hiki hakiwezi kumezewa na wanahabari, lakini vyombo vya habari vitakiripoti kwa uchambuzi, tayari inakuwa nongwa. Mwanaspoti linadhani ili kuepuka lawama hizi za mara kwa mara, Malinzi na wenzake wanapaswa kuwa wa kwanza kuhakikisha hawatoi mwanya kwa wanahabari kuwandama.  Nako ni kuhakikisha wanafanya mambo yao kwa umakini na weredi mkubwa. Haiwezekani mchezaji anasajiliwa na kucheza ligi mbili tofauti kwa majina tofauti asibainike wakati kuna picha na saini zao, ina maana usajili unaofuatiliwa kwa umakini zaidi ni wa timu za Ligi Kuu Bara tu? Huu ni udhaifu. Timu iliyofanya udanganyifu inakuwaje inapandishwa daraja? Huu nao ni udhaifu.

Wanahabari likiwamo Mwanaspoti linapenda kuona soka la Tanzania linaendeshwa kwa ufanisi na umakini, ndio maana wamekuwa wepesi kulisemea jambo kila pale wanapoona halipo sawa. Wamefanya hivyo katika mpango wa Maboresho ya Taifa Stars, panga pangua ya Ligi Kuu kwa ajili ya kuruhusu timu moja kwenda kushiriki mechi za bonanza nje ya nchi. Vyombo vya habari vimepiga kelele kusimama kwa ligi baada ya kucheza mechi chache kisha kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili. Wanahabari wamepiga kelele kuahirishwa kwa ligi kwa muda mrefu ili kupisha maandalizi ya Stars katika kambi nje ya nchi, ilihali sio timu zote zenye wachezaji katika timu hiyo. Vimepiga kelele kuona mechi za viporo kutoka timu moja hadi nyingine kuwa nyingi kwa nia ya kutaka kuona soka la Tanzania linakuwa imara. Je, haya ni makosa?