NINACHOKIAMINI: Malinzi tena! Mbona vituko kwenye soka haviishi!

Muktasari:

  • Hivi umewahi kujiuliza na kujua ni kwanini watu wasiojiamini hupenda kuwa na washauri wa kiwango cha chini. Watu ambao hawastahili kazi hiyo ya ushauri ndio hupewa nafasi kubwa. Inasikitisha.

WATU wasiojiamini huwa na tabia kadhaa ambazo mara nyingi hukwamisha maendeleo. Ni ukweli usiopingika kuwa kuna baadhi ya watu wenye madaraka, lakini hawajawahi kujiamini.

Watu wa aina hii huwa wanapenda kuzungukwa na wapambe kwa ajili ya kuwalisha uwongo pamoja na mambo mengine ya kuwapendezesha.

Watu hao wasiojiamini hupenda kuzungukwa na watu wajinga, au ambao upeo wao ni mdogo kuliko wao. Hawa watu wasiojiamini kamwe huwa hawapendi kukaa pamoja na watu wenye akili.

Unaweza kuangalia mazingira yanayokuzunguka, angalia viongozi wengi wamezungukwa na watu wa aina gani? Angalia matajiri wengi wamezungukwa na watu wa aina gani?

Hivi umewahi kujiuliza na kujua ni kwanini watu wasiojiamini hupenda kuwa na washauri wa kiwango cha chini. Watu ambao hawastahili kazi hiyo ya ushauri ndio hupewa nafasi kubwa. Inasikitisha.

Watu wasiojiamiani na hasa walio katika nafasi fulani kwenye jamii huwa hawapendi kupingwa wala hawapendi kukosolewa na ndio maana hutaka kujibu kila tuhuma wanayoisikia mtaani.

Hawa ni aina ya watu ambao wataacha majukumu yao ya kila siku na kuanza kupambana na watu wanaodhani wanawapinga. Huwa hawataki kabisa kusikia mtu mwingine akiwapinga au kuwapa ushauri.

Watu wa namna hii huwa hawapendi kukaa pekee yao, hupenda kulindwa kwa kuzungukwa na wapambe popote walipo. Hujitahidi kuwa na wapambe ambao watawasapoti popote.

Viongozi wa aina hii huwa wanahisi mapinduzi kila wakati, hudhani wataondolewa madarakani, hudhani hawako salama, lakini hizo huwa ni hisia tu na huwa hakuna ukweli hata kidogo.

Viongozi wa aina hii hugeuza majungu kuwa ajenda za vikao na mambo yote muhimu hujadiliwa katika mengineyo tena kwa haraka haraka sana.

Na ndio maana huwezi kushangaa kusikia Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi akitetea nafasi yake ya uenyekiti wa Mkoa wa Kagera kwa kura 21 kati ya 22.

Malinzi, ambaye aliingia madarakani TFF miaka mitatu iliyopita yupo katika wakati mgumu kutokana na kupata upinzani mkali kutoka kwa wadau wa soka nchini.

Kama kuna mambo kumi alitakiwa kuyafanya, unaweza kumsifu kwa kuifanya timu ya taifa ya vijana ‘Serengeti Boys’ kufanya vizuri katika mashindano ya vijana kufuzu kwa Mataifa ya Afrika.

Ndio, katika mambo kumi unaweza kumpa sifa kwa kitu kimoja hicho cha Serengeti Boys, lakini unaweza ukasema amefeli katika mambo tisa yaliyosalia.

Malinzi amemuacha hoi kila mdau wa soka nchini kwa sababu kama Rais wa TFF amejidhalilisha kugombea na kushinda nafasi ya mwenyekiti wa chama cha soka Kagera.

Nani atakayeigusa Kagera Sugar, hakuna! Nani atamgusa mwamuzi yeyote kutoka Mkoa wa Kagera? Hakuna.

Malinzi ameuweka Mkoa wa Kagera katika mazingira magumu, kwa sababu kila watakachokifanya itaonekana kwa sababu ya rais huyo wa TFF kuupendelea mkoa ambao pia yeye ni mwenyekiti.

Malinzi anaweza kujitetea kuwa Katiba ya TFF haisemi lolote kuhusu hilo, lakini kwa kufikiria tu yeye mwenyewe alipaswa kujua kuwa kuna mgongano wa kimaslahi.

Ndio, kuna mgongano wa kimaslahi na mtu ambaye anajiamini asingethubutu kuwania nafasi ndogo wakati tayari ana nafasi kubwa ya kitaifa.

Tunaposikia chaguzi nyingine mikoani zimekuwa zikifanywa kwa ushawishi mkubwa wa viongozi wa TFF unaweza kudhani ni uwongo, lakini jambo hili linatufanya tuamini kila kisemwacho.

Sisi wengine tunajua kuwa uchaguzi wa TFF utafanyika mwakani na kwa sababu Malinzi hana uhakika wa kutetea nafasi yake anahangaika sana ikiwa pamoja na yeye mwenyewe kushika nafasi ya uenyekiti wa Kagera.

Malinzi amewania nafasi hiyo ya Kagera si kwa sababu ya masilahi ya soka, lakini anataka kujiongezea kura katika uchaguzi wa mwakani.

Watu wanampinga Malinzi, lakini ngoja nimpe hongera kwa kutumia akili ya hali ya juu katika hiki alichokifanya kwa sababu amejiongezea kura moja, nyie mlitaka afanye nini?