HISIA ZANGU : Mabosi TFF wanapandisha timu za kumshangaa Kamusoko uwanjani

Muktasari:

Unawaza Azam kuwa bora kuliko Zamalek au Al Alhy au TP Mazembe? Zote hizo sio ndoto zangu.

UNAWAZA Simba kuchukua ubingwa wa Afrika? Unawaza Yanga kuchukua ubingwa wa Afrika? Unawaza nini katika soka la Tanzania?

Unawaza Azam kuwa bora kuliko Zamalek au Al Alhy au TP Mazembe? Zote hizo sio ndoto zangu.

Nina ndoto moja tu. Wachezaji wa Tanzania kujaa Ulaya. Itakuwa njia ya mkato kuipaisha timu ya taifa. Tutapata kina Mbwana Samatta wanaofahamu wanachokifanya uwanjani. Kuna mataifa ya Afrika Magharibi yamekombolewa na mfumo huu.

Vinginevyo sina ndoto nyingine na soka la Kibongo. Linaendeshwa kijingajinga na nahisi naweza kuingia kaburini nikiwa bado sijaifaidi Taifa Stars ikicheza michuano ya kimataifa. Unaweza kuniuliza kwa nini? Una sababu zako na mimi nina zangu.

Nakupa moja tu. kila siku unasikia kuna ngumi katika Ligi daraja la kwanza. Unajua kwa nini? Kwanza hakuna anayejali sana kinachoendelea daraja hilo. Mwamuzi kupigwa daraja la kwanza sio habari kubwa sana kuliko Yanga kusafiri kwenda kucheza na Majimaji Songea au Simba kwenda kucheza Morogoro na Mtibwa Sugar.

Matokeo yake kule daraja la kwanza kuna maigizo ya mpira badala ya mpira wenyewe. Hakuna anayejali kwa hiyo na wao wanafanya ujinga hadharani.

Viongozi wa TFF wana timu zao za mikoani ambazo wanataka zipande kwenda Ligi Kuu.

Bwana Mkubwa aliyepo katika kiti cha enzi anajua mpango mzima. Inamuia vigumu kwake kufanya lolote kwa sababu anatazama zaidi kura zake za wakati wa uchaguzi ujao kuliko kujali sana ujinga unaondelea daraja la kwanza.

Kule Iringa kuna maajabu yanaendelea. Inalazimishwa kuwa lazima Lipuli lazima ipande. Kuna viongozi wa TFF makao makuu kwao ni Iringa wanalazimisha timu ipande.

Nasikia viongozi wa timu pinzani wananyang’anywa simu zao wakati wa kwenda uwanjani.

Nasikia Morogoro inalazimishwa lazima Ligi Kuu irudi kwa sababu ya mapato. Watake wasitake. Na hata kule Mwanza inatakiwa timu nyingine. Baada ya hapo vinavyofuata ni vihoja. Mwamuzi kukataa mabao ya wazi ya timu pinzani, mwamuzi kupendelea hadharani bila ya aibu.

Mwamuzi anakuwa hana wasiwasi kwa sababu ana maagizo. Kule katika daraja la kwanza kamati ya saa 72 haipo. Kule ni Ligi ya giza. Nani anajali wakati mashabiki na waandishi wa habari akili wamezielekea katika Simba na Yanga?

Unachoshangaa zaidi ni kwamba timu inalazimishwa kupanda kwa kila sababu wakati haina uwezo. Ni timu ambayo inataka kupelekwa Ligi Kuu mbele ya macho ya kiongozi mkuu kwa sababu analinda kura zake za mkoa huo. Hataki achukiwe.

Lakini hapo hapo ni kwamba timu hii itapanda Ligi Kuu. Itapanda bila ya kuwa na uwezo wowote mkubwa. Baadaye watacheza Ligi Kuu dhidi ya timu kubwa kama Simba, Yanga na Azam. Watafungwa mabao mengi huku tukiamini kuwa Simba, Yanga na Azam ni timu nzuri sana. kumbe katika michuano ya kimataifa hakuna kitu.

Hii yote ni kwa sababu hawapati upinzani wa kutosha kutoka katika timu zinazopanda daraja. Katika ligi za wenzetu, timu zinazopanda daraja zinakuwa na wakati mgumu katika Ligi Kuu kwa sababu bajeti yao ya pesa inakuwa imebana kidogo.

Hapa nchini hizi timu zinapata wakati mgumu kwa sababu zilibebwa katika Ligi Daraja la kwanza. Kwa staili hii unapata vipi timu imara ya taifa kwa wachezaji ambao wamepandishwa kuja Uwanja wa Taifa kumshangaa Thaban Kamusoko akicheza? Hauwezi kupata timu imara ya taifa. Na ndio maana njia sahihi na mwafaka ya haraka ya kuikomboa Taifa Stars ni kupata wachezaji wengi wanaocheza katika soka linaloeleweka.

Huku Ligi Kuu kumeoza halafu bado kila mwaka zinapandishwa timu kwa matakwa ya mabosi wa TFF kwa sababu mbalimbali za uchaguzi au siasa au mapato. Mpira wetu unazidi kuharibika. Programu za vijana hazieleweki, mpira wa madaraja haueleweki.

Jaribu kuulizia. Timu nzuri zinabakia daraja la kwanza kwa sababu mbili. Kwanza hazina pesa za kuhonga, pili mkoa wao una bifu za kiuchaguzi na uongozi uliopo madarakani kwa sasa. Huu ndio mpira wa Tanzania ambao umeniachia ndoto moja tu. Nataka wawepo kina Samatta wengi tuachane na mpira huu wa kihuni kabisa.