MTU WA PWANI: Naliona soka la Zanzibar ni kama maisha ya kenge

UGUNDUZI mwingi uliofanywa na mwanadamu ni matokeo ya roho ya kujituma na kujaribu kufanya jambo fulani pasipo kukata tamaa pale inapotokea amekutana na vikwazo mbalimbali.

Laiti kama Mungu asingempa binadamu roho ya ujasiri na kujituma, ni wazi kuwa vitu vingi tunavyoviona leo hii duniani visingekuwepo na pengine hata dunia yenyewe isingekuwa kama hivi tunavyoiona sasa.

Ni rahisi kwa mtu mwenye roho ya kuthubutu kuweza kupata mafanikio ya haraka kinyume na yule ambaye anaogopa kujaribu kwa sababu tu ya kuhofia kuwa huenda akashindwa kwa kile anachotaka kukifanya.

Hata hivyo, si kila mmoja wetu anaweza kuwa na moyo wa kujaribu au kuthubutu kufanya jambo fulani, hivyo inapotokea mtu wa kujitoa muhanga amepatikana ni vyema akapongezwa au kukosolewa na kupewa ushauri kama hicho anachokifanya ni sahihi au si sahihi

Dhana hii tunaiona kwa viongozi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakijitoa muhanga na kutumia kila walichonacho katika kuhakikisha visiwa hivyo vinapata uanachama katika Shirikisho la Soka Afrika (Caf) na lile la duniani (Fifa).

Harakati za Zanzibar kutafuta nafasi ya kuwa mmoja wa wanachama wa vyombo hivyo viwili vya soka, hazikuanza jana wala leo na zilikuwepo kabla hata Agnes Masogange na Wema Sepetu hawajaanza Shule ya Msingi.

Tupongeze juhudi za dhati zinazofanywa na viongozi wa ZFA pamoja na baadhi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambao wamekuwa wakiweka msukumo katika kuhakikisha wanazishawishi Caf na FIFA zikipe uanachama kisiwa hicho.

Na juhudi hizo hivi sasa zinaonekana kuelekea kufanikiwa baada ya kuwepo taarifa kuwa Caf iko mbioni kukipa uanachama kisiwa hicho jambo ambalo litakirahisishia kupata uanachama wa FIFA.

Mara kwa mara kumekuwa na malalamiko kutoka kwa ndugu zetu wa Zanzibar kuwa upande wa pili huku ndio tumekuwa tukiwakwamisha kupata uanachama, hivyo naamini sasa kama wakifanikiwa, basi angalau Tanzania Bara tutapumua kutokana na lawama hizo.

Hata hivyo, ingawa wakati Zanzibar inapambana kupata uanachama ni vyema pia ikatumia nguvu nyingi katika kuhakikisha inamaliza changamoto ambazo zinarudisha nyuma soka visiwani humo.

Changamoto kuu inayoumiza soka la Zanzibar nadhani inaeleweka kuwa ni hali ya ukata ambayo inatokana na kukosekana kwa uwekezaji wa kifedha kwenye medani ya soka katika visiwa hivyo.

Tofauti na Tanzania Bara ambako makampuni mbalimbali yameamua kujitosa na kuingiza fedha kwenye soka, kwa upande wa Zanzibar hali sio nzuri na mchezo huo unaendeshwa kifukara sana.

Hii inapelekea klabu nyingi za soka kwenye visiwa hivyo kushindwa kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa licha ya Zanzibar kubarikiwa kupata vijana wengi ambao wana vipaji vya hali ya juu vya soka pengine kuzidi hata wachezaji wa Bara.

Wachezaji kama Selemani Kassim ‘Selembe’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Haji Mwinyi, Awadh Juma ‘Maniche’, Adeyum Saleh, Aggrey Morris, Abdulhalim Humud pamoja na Khamis Mcha ni mfano tu wa vipaji vya soka ambavyo Zanzibar imezalisha.

Vipaji hivi kama hakuna pesa ya kuvilipa mshahara, posho, kuviweka kambini, kuwapatia makocha bora pamoja na huduma nyingine muhimu ambazo mchezaji anatakiwa kuzipata, ni wazi kuwa vitatimka kusaka malisho mazuri upande mwingine na kushindwa kuzisaidia timu za Zanzibar katika mashindano ya kimataifa.

Nani utamshawishi kuwa, Zanzibar iko tayari kuwa mwanachama kamili wa Caf na FIFA wakati ni hivi karibuni tu timu yake ilisafiri kwa basi kutoka hapa hadi Burundi kwa ajili ya kucheza mechi ya marudiano ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika?

Kabla haijapata uanachama inayohitaji, ni vyema kwanza kisiwa hicho kikawa na watu au makampuni ya kufanya uwekezaji kwenye soka kama ilivyokuwa kwa kina Mohammed Naushad na wengine ambao walizifanya timu kama Malindi na Mlandege kuwa tishio kubwa kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Enzi hizo, Zanzibar iliwatoa wachezaji mahiri ambao walizisaidia timu zao kutamba katika michezo ya Ligi ya Muungano na kuzitoa jasho timu za Tanzania Bara. Pia, wachezaji hao walizisaidia timu zao katika mashindano mbalimbali ya kimataifa. Pesa za kina Noushad zilisaidia kuwapa changamoto Wazanzibari kwa kuwapeleka wachezaji mahari kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Lakini pia uanachama wa Caf hauwezi kuisaidia Zanzibar kama bado soka lake litaendelea kusumbuliwa na migogoro ya mara kwa mara ndani ya ZFA pamoja na klabu zake.

Migogoro hiyo imesababisha ZFA pamoja na timu za Zanzibar kutumia muda mwingi kuimaliza badala ya kutafakari na kuweka mikakati ya kuhakikisha soka la visiwa hivyo linapiga hatua.

Ni wazi kuwa migogoro hiyo ni moja ya sababu zinazofanya makampuni yahofie kufanya uwekezaji kwenye soka la Zanzibar kwa sababu yanaogopa fedha zao kupotea bila kufanyiwa matumizi sahihi.

Hakuna mtu au kampuni ambayo inaweza kutumbukiza pesa zake huku ikiwa haina uhakika wa kunufaika na uwekezaji ambao imeufanya.

Kama itashindwa kuziondoa changamoto ilizonazo, ni wazi kuwa Zanzibar itakuwa inafanya kazi bure katika juhudi zake za kuomba uanachama wa FIFA na Caf.

Tulikabidhi soka la Zanzibar kwa Mungu na kuliombea ili wakati itakapofanikiwa kupata uanachama, ili nafasi hiyo waitendee haki lakini kama watapa uanachama huku hakuna pesa ya kuendesha mpira wao pamoja na kuendekeza migogoro itakuwa sawa na maisha ya kenge ambaye mvua inaponyesha, hukwepa matone kwa kukimbilia kwenye bwawa la maji.