MTAA WA KATI: Mourinho anapoendesha Ferrari kama Scania

Muktasari:

  • Wapo waliofika mbali zaidi na kumhesabia mechi kwamba mpaka sasa hajafunga. Na wala hajatoa asisti hata moja.

JOSE Mourinho amenunua Ferrari, lakini anataka kuiendeesha kama scania.

Utampaje staa wa Euro 110 milioni kazi ya Nemanja Matic. Kazi ya N’Golo Kante. Haya ni matumizi mabaya.

Tangu Manchester derby imalizike, stori inayozungumzwa kila kona kwa sasa kiwango cha Paul Pogba kwenye mechi hiyo. Wapo wanaosema kwamba hakuonekana uwanjani. Hakufanya jitihada za ziada.

Wapo waliofika mbali hata kuanza kujadili ada yake ya uhamisho iliyotumika kwenye kuinasa saini yake.

Wapo waliofika mbali zaidi na kumhesabia mechi kwamba mpaka sasa hajafunga. Na wala hajatoa asisti hata moja.

Ilimradi tu kila mtu amesema analolifahamu yeye kuhusu staa huyo. Mwenyewe hakusema kitu kuhusu kiwango chake kwenye mechi hiyo zaidi ya kusema wamepoteza mechi na hilo ni somo wamejifunza. Ibrahimovic amejaribu kuwatuliza watu. Akisema wengi wanaomsema Pogba baada ya mechi ya Manchester derby na kumhesabia mechi zilizopita, wanasumbuliwa na wivu.

Wanaona wivu kwa kuwa mchezaji ghali duniani na ndiyo maana watasema mengi mabaya ili kumchafua, lakini yeye anamwona kila siku Pogba jinsi anavyofanya na ipo siku wenye wivu watameza maneno yao. Ibra huyo maneno yake. Sisi tuachane naye.

Tutamzame Pogba kiufundi. Pale Juventus alikuwa akifunga sana mabao na kupiga asisti za kutosha. Sasa yupo Man United unajiuliza, asisti zimekwenda wapi?

Ni jambo dogo tu. Kuna kitu kinaitwa mfumo. Mstari wa kwanza kabisa katika makala haya, kuna maneno yanayosema Jose Mourinho amenunua ferrari, lakini anataka kuiendeesha kama scania.

Hiki ndicho anachokifanya Mourinho kwa Pogba. Amembadilishia majukumu. Hafanyi tena kile alichokuwa akikifanya Juventus. Mourinho anamtumia Pogba kuwa kiungo wa kati.

Anajaribu kumtafutia pacha wake kuwa Marouane Fellaini. Pogba anacheza chini sana, afanye kazi moja kunyang’anya mipira na kuwalinda mabeki wa kati.

Hii kazi Pogba haiwezi, hawezi kuifanya kwenye ubora wake. Kwa sasa Mourinho anamtumia kwa kumchezesha chini, tofauti na eneo la ubora wake.

Pale Juventus, Pogba alikuwa akicheza kwa kuachwa huru ndani ya uwanja, kitu ambacho Man United kwa sasa kitu hicho kinafanywa na Wayne Rooney.

Kwenye majukumu mapya aliyopangiwa kuyafanya, Pogba atahitaji muda kabla ya kuanza kuonyesha makali yake hapo.

Kwenye mechi ya Manchester derby hakuruhusiwa kabisa kupanda mbele na hata alipofanya hivyo, Jose Mourinho alinyanyuka kitini kutazama itakuwaje.

Pogba alizoea kucheza kwenye safu ya viungo watatu na si viungo wawili kama anavyopangwa kwa sasa na Fellaini. Mourinho anafahamu wazi kitu ambacho anakifanya na ndiyo maana hataki matunda ya haraka haraka kutoka kwa mchezaji huyo.

Kitu hicho kinapaswa kutambulika na mashabiki pia, Pogba wa Man United anaandaliwa tofauti na yule aliyekuwa Juventus.

Ni jambo la kusubiri na kuona kama ataweza kuyamudu majukumu yake mapya au Mourinho ataamua kumrudisha kwenye eneo la ubora wake ambalo lilimfanya atoe pesa nyingi kuinasa saini yake.