MSINIBISHIE: Sawa Nyosso kakosea, ila hii adhabu hapana!

Muktasari:

Unaweza kuona adhabu hiyo ilivyokuwa kubwa kwa mchezaji kama huyo, licha ya kuwa tukio kama hilo liliwahi kufanywa pia katika nchi zilizoendelea kisoka

TUKIO ambalo limeonekana kuwavuruga watu wengi hasa wapenda soka katika siku hizi tano ni lile la beki wa Mbeya City, Juma Nyosso kumdhalilisha mshambuliaji wa Azam FC, Jonh Bocco ‘Adebayor’.

Ni tukio ambalo lilionekana kukemewa na karibu asilimia kubwa ya wapenda soka na hata watu ambao unaweza kusema hawahusiani kabisa na mchezo huo pendwa.

Kwa kuliona hilo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Bodi ya Ligi iliamua kumfungia beki huyo wa zamani wa Simba kutocheza soka kwa miaka miwili.

Unaweza kuona adhabu hiyo ilivyokuwa kubwa kwa mchezaji kama huyo, licha ya kuwa tukio kama hilo liliwahi kufanywa pia katika nchi zilizoendelea kisoka.

Awali, Nyosso aliwahi kufungiwa kwa kutocheza soka kwa mechi nane kwa tukio kama hilo akimdhalilisha mshambuliaji wa Simba wa wakati huo, Elias Maguli.

Picha ya tukio la Jumapili iliyopita katika Uwanja wa Azam Complex zilianza kusambaa kwa fujo katika mitandao ya kijamii kama WhatsApp na Facebook kwa kila mmoja kumshutumu mchezaji huyo huku wengine wakiomba adhabu kubwa kwake.

Kweli! Walilotaka likawa, Nyosso akaingia hatiani na kuhukumiwa miaka miwili nje ya uwanja kwa kosa hilo huku utata zaidi ukiibuka.

Awali, nilikuwa na wasiwasi juu ya tukio hili, lakini baadaye nikafanikiwa kuiona video iliyokuwa ikionyesha vizuri tukio hili, hakika kuna mambo ambayo TFF hawakuzingatia katika adhabu yao.

Kwa tukio kama hili, ambalo mwamuzi hakuliona, TFF walipaswa kufanyia kazi video ya mchezo husika badala ya kuangalia picha mnato kama ambavyo wamefanya.

Sitaki kubishana hapa, lakini ukweli ni kwamba tukio hili lilianzia kwa Bocco mwenye, ambaye anaonekana kuanza kumpiga teke Nyosso ugokoni. Sina tatizo na kosa alilofanya Nyosso, lakini ninachotaka kusema hapa ni kwamba adhabu amepewa Nyosso, huku Bocco akionekana msafi, kitu ambacho si cha kweli.

Kama TFF ingeangalia video ile, ambayo inaonyesha mchezo ulikuwa umesimama wakati Bocco akitumia ujanja kukwaruzana na Nyosso, wangebaini makosa ya nyota wote wawili na kuwapa adhabu iliyostahili kama ambavyo aliadhibiwa Diego Costa wa Chelsea aliyeonekana baadaye katika video.

Lakini hata adhabu yenyewe ukiangalia ni kama inakomoa vile. Hakuna adhabu ya mchezaji kufungiwa miaka miwili katika soka. Gonzalo Jara wa Chile aliwahi kufanya tukio la zaidi ya Nyosso. Jara alikamatwa videoni akimdhalilisha mshambuliaji wa Uruguay, Edinson Cavani katika mchezo wa robo fainali ya Copa America mwaka huu. Lakini kilichotokea uwanjani, Cavani alionekana akijibu mapigo kwa kibao na kuonyeshwa kadi ya pili ya njano iliyomtoa uwanjani, wakati Jara akifungiwa kutocheza mechi zote zilizobaki za mashindano hayo, ambazo kimsingi zilikuwa mbili tu.

Sikatai Nyosso amekosea, lakini jinsi adhabu hii ilivyoangaliwa na ukubwa wake ni vitu viwili tofauti, kuna haja ya kuangalia upya badala ya kutoa adhabu za kukomoana.

Hili ni soka, tunaangalia kila kukicha mechi za wenzetu, Jara wa Chile angekuwa wapi kwa tukio lake ambalo lilikuwa mara tatu katika sekunde mbili, achilia mbali Nyosso?