MAONI: Viongozi ndio tatizo katika timu za mikoani

HII NDIO MWADUI FC YA JULIO

Muktasari:

  • Lakini katika miaka ya karibuni kumekuwa na msisimko kwenye soka la Tanzania, ambapo umechangiwa na kuanza kukua kwa mikoa mingi kuwa na timu zinazoshiriki  Ligi Kuu na madaraja mengine.

SOKA la Tanzania limekuwa likipanda na kushuka, ambapo katika miaka ya nyuma kiwango cha soka letu kilikuwa juu sana. Hilo lilichangiwa na uwepo wa timu za mashirika ya umma na taasisi za serikali ambazo kila mmoja ilikuwa na timu imara iliyokuwa ikishiriki Ligi Kuu ama ile ya madaraja ya chini hivyo, kuongeza hamasa na msisimko.

Hata hivyo, itakumbukwa kuwa baadaye kutokana na mfumo wa mabadiliko ya serikali, mashirika na taasisi za umma zilijiondoa kwenye michezo hivyo, timu nyingi zikiwemo zile zilizokuwa na maskani yake kwenye mikoa mbalimbali nchini, kuanza kupotea taratibu na kusababisha soka la Tanzania kuyumba kwa kiasi fulani.

Lakini katika miaka ya karibuni kumekuwa na msisimko kwenye soka la Tanzania, ambapo umechangiwa na kuanza kukua kwa mikoa mingi kuwa na timu zinazoshiriki  Ligi Kuu na madaraja mengine.

Awali, timu nyingi zilikuwa na maskani yake Dar es Salaam, Pwani na Morogoro, lakini kwa sasa Mwanza, Mbeya, Mtwara, Songea, Shinyanga na Kagera kote kuna timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Hilo limerejesha hamasa kwa kasi kwa mashabiki, ambao kwa sasa wanakwenda viwanjani kuzipa sapoti timu zao zinapocheza.

Uwepo wa klabu za Ligi Kuu kwenye mikoa hiyo kumechangia kuibua na kukuza vipaji vipya ambavyo vilikuwa vimesahaulika kwa muda mrefu. Lakini pamoja na uwepo wa utitiri wa klabu hizo bado kuna changamoto kubwa ya kupata viongozi sahihi wa kuziongoza. Klabu zinakosa viongozi wenye mapenzi ya dhati na soka na wanaofahamu na kufuata kanuni za kuongoza mpira.

Klabu nyingi zimekuwa zikiongozwa kwa mazoea na kwa mtindo wa kujuana zaidi, jambo ambalo linazigharimu klabu haswa linapokuja kwenye jambo linalohitaji utaalamu hususan uingiaji wa mikataba ya kibiashara na udhamini.

Viongozi wengi hawana uelewa mpana wa mikataba wanayoingia na wadhamini jambo ambalo linasababisha matatizo ya kiuendeshaji. Kwa kutambua hilo, baadhi ya wadhamini ambao hawana mapenzi maema, wamekuwa wakiwasainisha viongozi hao mikataba ya hovyo inayolinda maslahi na matakwa yao badala ya klabu husika.

Tunasema hivyo, kwa sababu katika nchi zilizoendelea na klabu zenye viongozi makini na wanaosimamia maslahi ya klabu zao, mdhamini na klabu wanakaa mezani na kukubaliana mambo ya msingi tofauti na Tanzania, ambapo klabu inakuwa chini na mdhamini ndiye mwenye sauti.

Mikataba mingi inayoingiwa na viongozi wa klabu zetu imekuwa ikiwapa wadhamini nafasi kubwa ya kufanya maamuzi ikiwemo kuweka vipengele ambavyo havina maslahi kwa klabu pindi mkataba unapovunjwa bila kutoa fidia yoyote.

Tumeshughudia hapa Tanzania kuwa inapotokea mdhamini akaingia kwenye msuguano wa kiongozi wa klabu, anaweza kuamua kutangaza kujiondoa bila kuangalia masilahi mapana ya klabu kwa kuwa, hakuna kipengele ama kanuni inayombana iwapo atavunja mkataba huo. Hili ni tatizo kubwa na limekuwa likitokea mara kwa mara kwenye klabu zetu.

Hivi karibuni tatizo kama hilo limetokea kwa klabu za Majimaji na Stand United, ambazo wadhamini wake wamejiondoa na kuziacha zikihaha zisijue la kufanya ili kujiokoa.

 Tatizo kubwa linaloelezwa ni migogoro na figisufigisu za hapa na pale miongoni mwa wanachama na viongozi wa klabu hizo. Stand United na Majimaji zimekuwa na mivutano ya viongozi na wanachama mara kwa mara hivyo, kukosa uimara na watu wenye maamuzi sahihi kwa maslahi ya klabu.

Tunadhami umefika wakati sasa kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kama mlezi wa klabu kuingilia kati kwa kuweka sifa ambazo viongozi wa juu wa klabu wanatakiwa kuwa nazo ili kuondoa wababaishaji, ambao ndio chanzo cha migogoro.

Kama ilivyoziagiza klabu kuwa na makatibu watendaji wa kuajiriwa wenye sifa, basi iwe hivyo pia kwa wenyeviti, marais kwa kuweka sifa ikiwemo elimu, uzoefu na mambo mengi ili kuhakikisha klabu zinaendeshwa kisasa zaidi tofauti na ilivyo sasa.

Ukiangalia migogoro mingi inayoendelea kwenye klabu kwa sasa chanzo ni viongozi kuweka mbele maslahi binafsi zaidi hivyo, tunadhani hili linapaswa kukomeshwa. 

Haitakuwa na maana kama taifa tukipambana kukuza soka letu, wakati kwenye klabu kumejaa wababaishaji ambao wanashindwa kuendeleza kazi nzuri inayofanywa na makocha wanaoibua vipaji ili kuwa na hazina ya wachezaji wanaoweza kuleta tija katika timu za taifa.

Ikumbukwe kuwa klabu imara ndio msingi wa maendeleo na kukua kwa sola letu hivyo, kuwaacha wababaishaji wachache waendelee kutuvurugia mambo kwa kujali matumbo yao.