MACHO MANNE : Gallas, Mkopi kwani hamjui sheria?

Muktasari:

  • Sehemu yoyote ile ya kazi ambayo umeajiriwa kwa mkataba labda uwe kibarua tu au deiwaka huruhusiwi kusaini mkataba mwingine labda kuwepo na makubaliano maalumu ambayo yanatambulika pande zote mbili.

PENGINE hawa wachezaji wetu kwenye soka huwa wanarubuniwa na watu wasiopenda maendeleo yao ndio maana husaini mikataba miwili miwili. Ama hawana watu wenye upeo mkubwa wa kuwaelewesha juu ya kuheshimu mikataba, au viongozi wa timu husika wanawadanganya kama sio kiburi, tamaa na jeuri zao tu kwamba hakuna sheria inayowabana.

Sehemu yoyote ile ya kazi ambayo umeajiriwa kwa mkataba labda uwe kibarua tu au deiwaka huruhusiwi kusaini mkataba mwingine labda kuwepo na makubaliano maalumu ambayo yanatambulika pande zote mbili.

Suala la Mohamed Mkopi aliyesajiliwa Mbeya City pamoja na William Lucian ‘Gallas’ kwenda Mwadui FC kubainika kuwa wana mikataba na timu zao za awali, ni kosa kisheria kwani limefanywa bila ya makubaliano ya pande mbili, kwa sababu Prisons aliyoichezea Mkopi msimu uliopita kuwa na mkataba naye huku Ndanda ikiwa imemuongeza mkataba mpya Gallas.

Shirikisho la Soka (TFF) limefanya kile ambacho linastahili kukifanya ili kukomesha udanganyifu huo, adhabu iliyoitoa inastahili na itawafunza wachezaji wote ambao hawako makini kuheshimu mikataba yao ya kazi, pia watakuwa makini kuwakwepa viongozi ambao wanawarubuni kwa fedha pasipo kufuata taratibu za usajili.

Kanuni na sheria zipo wazi kwamba wachezaji ambao wana mkataba wa mwaka mmoja hawapaswi kufanya mazungumzo na timu yoyote mpaka viongozi wenyewe na anastahili kufanya mazungumzo akibakiza mkataba wa miezi sita pekee, hilo mara nyingi huwa halifuatwi kwa wachezaji na viongozi wasiokuwa na nia njema na wachezaji husika.

Leo hii Mkopi ambaye ilielezwa tangu mwanzo kuwa bado ana mkataba na Prisons wa mwaka mmoja alienda kusajiliwa Mbeya City ambayo pia huenda haikuwauliza hata viongozi wenzao kujua ukweli juu ya mkataba wa straika huyo, iliamini kile ambacho mchezaji amesema, ikampa mkataba sasa kafungiwa, hiyo ni hasara kwa pande zote mbili.

Mbeya City imetoa fedha kumsajili Mkopi ikishindwa kufikia muafaka pesa yake itakuwa imekwenda na maji labda isubiri adhabu yake itakapomalizika ambapo sidhani kama itamhitaji tena kwa kiwango cha sasa na baadaye, Mkopi naye itakuwa imekula kwake mazima kwani hatacheza popote, hakika ni pigo ambalo linapaswa kuwa darasa kwa wengine.

Sheria ni msumeno na hakuna aliye juu ya sheria labda ipindishwe, Gallas kijana mdogo ambaye kazi yake ni soka tu, leo hii anafungiwa kucheza soka kwa mwaka mzima unadhani maisha yake yatakuwaje? Maamuzi bora kuwa umakini huku sheria zikikuongoza. Ukiwekwa msimamo huo ndio utakuwa mwisho wake, aombe Mungu huruma na busara za kibinadamu zitumike kwa watakaosikiliza rufani zao.

Mwadui inadai ilizungumza na Ndanda ambayo imekataa kufanya hivyo na imeweka msimamo huo. Kungekuwa na nia ya kweli kwani naamini Mwadui ilikuwa inafahamu kuwa Gallas ameongeza mkataba, basi ingemalizana mapema kuliko hatua hii iliyofikiwa kwa mchezaji. Hata kama yataisha ila sifa yake itakuwa imeshuka kwani uamunifu kwa timu nyingine utakuwa ni mdogo.