KONA YA MICHARAZO : Ligi kweli inanoga, ila hii ratiba kama haijakaa sawa

Muktasari:

Ndio! Kuanzia nyumbani Tanzania mambo yalikuwa mswano na hata kule majuu kadhalika wengi wao nyoyo zao zilisuuzika kutokana na matokeo yaliyopatikana wikiend

NAAMINI kabisa nyote mu wazima wa afya tayari kuianza wiki nyingine mpya, huku wale mashabiki wa soka roho zikiwa kwatu.

Ndio! Kuanzia nyumbani Tanzania mambo yalikuwa mswano na hata kule majuu kadhalika wengi wao nyoyo zao zilisuuzika kutokana na matokeo yaliyopatikana wikiendi.

Nyumbani Mnyama ikiwa kwenye ubora wake aliweza kuinyoosha Azam kwa bao la kiberenge Shiza Kichuya, wakati watani zao wakiwa ugenini waliweza kuwakwangua Mwadui ya Julio mabao 2-0.

Utamu zaidi ulikuwa kwa Mbao kufufukia Mabatini mbele ya Masau Bwire na kuitandika Ruvu Shooting mabao 4-1. Hujakosea, mabao manne yalitinga kwenye nyavu za Ruvu Shooting, huku Majimaji ikiendelea kuwa mnyonge kwelikweli.

Wanalizombe wamecheza mechi yao ya tano bila kuonja ushindi baada ya Ndanda Kuchele kuwanyoosha nyumbani kwao kwenye Uwanja wa Majimaji, huku Mtibwa Sugar ikiikandika Kagera mabao 2-0.

Simba ikirudi kileleni, mfumania nyavu anayeshikilia kiatu rekodi ya kusisimua VPL kwa kufumania mabao mengi kwa misimu minne mfululizo, Mrundi Amissi Tambwe ameanza kuwatia wenzake tumbo joto.

Ameendelea kutupia kama kawaida akiwakamata kilaini kina Mavugo, Bocco na wengine waliokuwa wamemtangulia, huku Ngoma akijikongoja.

Kifupi ni kwamba Ligi ya VPL imeanza kunoga na kufanya mashabiki kukaa roho juu, hasa wakati wakielekea kwenye pambano la watani Oktoba Mosi hakuna anayejua nani atapatwa siku hiyo kati ya Simba na Yanga.

Barani Ulaya hasa kule kwa bibi, Vijogoo vya Anfield walifanikiwa kulibomoa daraja la Stamford, huku watetezi, Leicester wakionyesha kuanza kufufuka EPL na Wapiga Mitutu wakiwapa burudani mashabiki wao kwa kushinda ugenini.

Kwingineko wababe wa soka wa La Liga, Ligue 1 na Bundesliga walitoa mikong’oko ya haja Barcelona, Real Madrid na mahasimu wao wa jiji hilo, Atletico Madrid walitakata kama ilivyo kwa PSG, Bavarian na Dortmund.

Wakati tukiianza wiki nyingine mpya tukiwa kamili gado, Mzee wa Micharazo lazima kwanza atoe pongezi kwa timu ya taifa ya vijana ya Tanzania, Serengeti Boys kwa ilipofikia katika mbio zake za kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.

Kwa hakika vijana wameonyesha nia yao ya kutaka kutufuta machozi Watanzania baada ya wawakilishi karibu wote wa nchi kutolewa na wao kukomaa na sasa wakisubiri mchezo mmoja tu, ili waende fainali za mwakani nchini Madagascar.

Ukiacha hilo la Serengeti Boys, pia nilikuwa nawapa kifyagio madada zetu wa Kilimanjaro Queens waliokuwa wakiipigania Tanzania Bara katika michezo wa nusu fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji kule Uganda.

Ni lazima tuwape heko Kili Queens bila kujali matokeo ya jana, kwani ndugu zao, Zanzibar Queens waliondoka kwa aibu baada ya kufumuliwa mabao 30-1 katika mechi tatu za michuano hiyo. Hata hivyo, soka ndivyo lilivyo wawakilishi wetu wa visiwani wajipange tu upya, ili warejeshe heshima yao ya mwaka 1986 walipotwaa ubingwa.

Kama kuna kitu ambacho kinanitatiza Mzee wa Micharazo ni ratiba ya Ligi Kuu kwa baadhi ya timu hasa vigogo Simba, Yanga na Azam kulinganisha na timu nyingine.

Inawezekana TFF na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) hawakuliona hili mapema, lakini ukweli ni kwamba ratiba kwa baadhi ya timu ni kama zinawatengenezea njia za ubingwa, huku wengine wakibaniwa.

Kwa mfano Simba inacheza mechi saba mfululizo za ligi hiyo jijini Dar es Salaam hata kama mechi inayoonekana itakuwa ugenini kwa maana dhidi ya JKT Ruvu na Yanga, ila ukweli ni kwamba sio ratiba inayovutia.

Iangalie sasa Toto Africans na ukata wake wote inasafiri kila uchao na haina muda wa kupumua, ukiangalia ratiba Azam ilipoenda Mbeya ilikaa jijini humo kwa siku chache na kumaliza mechi zake zote mbili za mji huo, Mbeya City ilienda Kanda ya Ziwa ikacheza karibu mechi zake zote za kanda hiyo.

Lakini iangalie Toto Africans sasa, ilitoka Mwanza ikaenda Shinyanga, kisha ikasafiri hadi jijini Mbeya kucheza na Prisons kisha ikarudishwa Dar es Salaam na kubakizwa kwa siku kadhaa kusubiri kucheza na Africans Lyon kisha itakaa siku chache kuifuata Ruvu Shooting pale mkoani Pwani ndipo irudie jijini Mwanza.

Nimetoa mifano hiyo michache kuonyesha jinsi gani ratiba ya msimu huu sio rafiki kwa baadhi ya timu na huku nyingine zikiinufaisha, kitu ambacho sio kizuri kama kweli tunataka kuona soka letu linainuka na kuzisaidia timu ambazo nyingi hazina uwezo.

Inawezekana namna ya upangaji na uhaba wa viwanja wenyeji kwa timu, lakini kwa nini Toto ilipoenda Mbeya haikupangiwa kucheza mechi zake mbili kisha labda iende Songea badala ya kulazimishwa kwenda Nyanda za Juu Kusini mara mbili tofauti na timu zenye uwezo mkubwa kiuchumi zikipewa nafuu?

TFF na Bodi ya Ligi zinatakiwa kuwa makini na upangaji wa ratiba bila ya kuzipendelea timu kubwa mabazo siku zote zimekuwa zikipewa nafasi ya kutwaa taji hilo.

Kwanini hatutaki kuzipa nafuu timu hizi? Nauliza tu wala msinichukie.