NINAVYOJUA : Kwa hili, hakika Yanga imejiponza yenyewe kimataifa

Muktasari:

  • Katika mfumo wa zamani, Simba iliweka rekodi mwaka 1993 ilipofika fainali za CAF lililokuja kuunganishwa na Kombe la Washindi ili kuwa Kombe la Shirikisho.

IELEWEKE wazi kuwa hii ni mara ya kwanza kwa klabu ya Tanzania kushiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, kwa mfumo huu wa sasa japo Yanga hiyo hiyo na Simba ziliwahi kucheza hatua hiyo kwa Ligi ya Mabingwa.

Katika mfumo wa zamani, Simba iliweka rekodi mwaka 1993 ilipofika fainali za CAF lililokuja kuunganishwa na Kombe la Washindi ili kuwa Kombe la Shirikisho.

Kwa timu za Afrika Mashariki ni Gor Mahia ya Kenya pekee iliyowahi kutwaa taji hilo, lakini baada ya miaka mingi hatimaye Yanga ilikuwa klabu pekee iliyofuzu hatua hiyo na kusalia katika michuano mikubwa Afrika kwa ukanda huo.

Hili sio jambo la mzaha, ni hatua kubwa ambayo Yanga inastahili pongezi. Lakini bado haikuwa sahihi kwa mashabiki waliodhani kitendo cha Yanga kuingia hatua hii tayari imepata wasaa wa kutinga hatua ya nusu fainali na kisha fainali.

Hayo yalikuwa ni matumaini yasiyo na ulinganifu wowote. Niliwahi kueleza hapo nyuma kuwa, kwa kufika hatua hiyo tu Yanga ilikuwa inaanza kujenga uzoefu wa namna ya kushiriki mashindano hayo. Kwanza kushiriki halafu baadaye kujenga dhana ya ushindani na mwisho kujua namna ya kushinda michezo yote ya nyumbani na ugenini.

Hili lilitosha kuwa sababu kubwa ya ushiriki, japo ndani ya ushiriki haikumaanisha kuwa Yanga ilitakiwa kutoshinda na hata kama ingefanikiwa kushinda michezo kadhaa na kufanikiwa kufika fainali bado hali hiyo ingekuwa kama bahati.

Hata hivyo, Yanga ilikuwa na nafasi ya kufanya vizuri kwenye kundi lake angalau hata kufika nusu fainali, lakini kuna sababu za kiufundi na za kisaikolojia zilizoifanya ishindwe kufanya vizuri.

Usajili mpya haukuziba mapengo

Kila mdau wa soka nchini alikuwa anayaona mapengo mawili makubwa ya Yanga moja likiwa ni kukosekana kwa kiungo mzuiaji ‘defensive midfielder’ mwenye uwezo sawa au zaidi ya Thabani Kamusoko ambaye uwepo wake hapo ungemfanya Kamusoko awe huru na raha ya kucheza atakavyo huku akitengeneza mashambulizi kila mara. Mchezaji ambaye angeweza kukaba na kupandisha timu bila tatizo! Sikutegemea kuona usajili wa mshambuliaji Obrey Chirwa.

Pengo lingine lilokuwa limeanza kuonekana na kwa muda limeisababishia Yanga matatizo ni la beki wa kushoto, kitendo cha Haji Mwinyi kuyumba kiuchezaji kwa muda mrefu ni wazi kuliifanya Yanga itabike sana na katika kutabika huko tayari kuliinyima ulinzi mzuri klabu hiyo na kusababisha kufungwa magoli kadha kupitia kushoto ambako Mbuyu Twite alianza kucheza na kujikuta akihama zaidi na kuingia ndani huku Joshua akifanya makosa yaliyozoeleka.

Kuvurugwa kombinesheni ya Tambwe na Ngoma.

Kulikuwa na makosa mawili ya kiufundi ambayo binafsi na hata wadau wengine wamekuwa wakiyashuhudia ndani ya Yanga kwa sasa, moja ni kitendo cha makocha wa Yanga kumuondoa kiaina Amissi Tambwe katika eneo sahihi analocheza kwa ustadi.

Hakuna ubishi si Ngoma wala Chirwa anayeweza kufanya kazi ya umaliziaji vizuri kama anavyoweza kufanya Tambwe iwe ni kwa kutumia miguu yake au kichwa bado Tambwe atabaki kuwa bora.

Unapomwondoa Tambwe kama mshambuliaji wa mwisho na kumpanga Ngoma au Chirwa unapunguza upatikanaji wa magoli kirahisi, pia unawanyima raha Ngoma na Tambwe kwa nafasi zao tofauti. Pia Ngoma na Chirwa wanaonekana wazi ni wazuri na kucheza kwa uhuru pale wanapocheza nyuma ya mshambuliaji wa mwisho huku Tambwe akikosa uwezo wa kufunga na raha anapocheza nyuma ya mshambuliaji wa mwisho.

Pili ni kitendo cha makocha wa Yanga kulazimisha ingizo la moja kwa moja ndani ya kikosi cha kwanza kwa mchezaji mpya (Chirwa) katika timu asiyoijua wala kuizoea. Chirwa alionekana kutokuwa timamu kimwili alipowasili na kucheza kwake dakika zote 90 kwenye michezo mingi hakujazaa matunda mazuri. Nilitegemea kumuona Chirwa akianza kuingia taratibu ndani ya kikosi cha kwanza na baada sasa ya kuzoeana na wenzake ndipo angeweza kuanza moja kwa moja.

Mgogoro wa Yanga dhidi ya TFF

Hili lilikuwa ni anguko la kwanza kabla ya michuano hii kuanza lilikuwa ni tatizo la kisaikolojia! Awali Yanga iliingia kwenye mgogoro wa kikatiba na TFF likihusu uchaguzi kitu ambacho kiliwafanya Yanga kwa muda kuanza kuwaza namna ya kufanya uchaguzi na sio kushiriki kwenye michuano hiyo waliokuwa wanakaribia kufuzu na hata walipofuzu siku za uchaguzi zilikuwa zikikaribiana na zile za maandalizi.

Hata baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa klabu hiyo, huku ikiwa imeshacheza mchezo mmoja ugenini Yanga iliingia katika mgogoro mwingine na TFF kuhusu haki ya kuonyesha michezo yake kwenye televisheni ikidai kutoshirikishwa.

Hali hiyo ilipelekea uongozi wa Yanga kuucheza mchezo wao dhidi ya TP Mazembe wazi bila kiingilio, hilo lilichochea chuki baina yao na TFF na hivyo, kuifanya Yanga kukosa ushirikiano. Mambo haya na mengine machache kwa kiasi kikubwa yameifikisha Yanga hapa ilipofika na linapaswa kuwa funzo.