Kombe la Mapinduzi litumike kuboresha soka visiwani

Friday December 30 2016

 

MSIMU wa 10 wa michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa mfumo unaotumika sasa, unatarajiwa kuanza leo Ijumaa na utaendelea mpaka Januari 13, mwakani, utakapochezwa fainali na kupatikana bingwa mpya.

Kwa msimu huu kuna timu tisa zinashiriki ikiwa watetezi wa taji hilo, URA ya Uganda pamoja na wawakilishi wanne wa Tanzania katika michuano ya kimataifa mwakani, yaani Yanga na Azam ya Tanzania Bara.

Pia kuna KVZ na Zimamoto zitakazoiwakilisha Tanzania Zanzibar, huku pia kukiwa na klabu za pinzani za Taifa Jang’ombe ‘Wakombozi wa Ng’ambo’ na Jang’ombe Boys, Simba pamoja na Jamhuri ya Pemba.

Kivumbi cha michuano hiyo kitaanza leo Ijumaa kwa Taifa Jang’ombe na Jang’ombe Boys zitakapovaana kwenye Uwanja wa Amaan majira ya usiku.

Kuanza kwa michuano hiyo ni faraja kubwa kwa mashabiki wa soka wa visiwani Zanzibar ambao, huwa ni nadra kuzishuhudia timu kubwa za Tanzania na hata za kigeni zikipambana kwenye ardhi yao.

Hivyo ujio wa msimu mpya wa michuano hiyo huwapa nafasi nzuri ya kuwaona nyota mbalimbali wa kitaifa na kimataifa sambamba na kupata burudani murua ya soka kwa muda wote wa michuano hiyo ya kusisimua.

Michuano hii huchezwa kwa wakati muafaka na huwa na faida kubwa kwa klabu wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Kombe la Mapinduzi hufanyika kila mwanzoni mwa mwaka ikiwa ni wiki chache kabla ya kuanza kwa michuano ya Afrika ambapo, kama wawakilishi wa Tanzania wakiitumia vema huwasaidia katika maandalizi yao ya kimataifa.

Kwa mfano tayari ratiba ya michuano hiyo ya Afrika imeshatolewa na klabu za Tanzania kufahamu zitaanza na timu gani na wapi, kwa maana nyumbani au ugenini, hivyo Kombe la Mapinduzi ni kipimo kizuri kwao kuelekea Afrika. Ukiondoa faida hiyo, pia michuano hiyo kama ikitumiwa vema na wenyeji ina manufaa makubwa katika kurejesha hadhi na msisimko wa soka visiwani humo.

Tangu kuzikwa kwa michuano ya Ligi Kuu ya Muungano iliyokuwa ikihusisha klabu kati ya sita, tatu kutoka kila upande wa Jamhuri, soka la Zanzibar limeporoka kiasi cha kustaajabisha na kutia aibu huku wadhamini wakiingia mitini.

Hata zile klabu zilizokuwa zikitetemesha katika soka la Tanzania miaka ya nyuma kama KMKM, Small Simba, Malindi, Miembeni, Kikwajuni, Black Fighters na nyingine kwa sasa zimebaki majina tu huku nyingine zikiwa ni historia kwa vizazi vya sasa.

Sio kwamba soka Zanzibar halichezwi, linachezwa kukiwa na Ligi Kuu na madaraja mengine, lakini ule mvuto na ubabe wa soka la visiwa hivyo kwa sasa ni kama haupo na ndio maana inashuhudiwa kila mwaka wawakilishi wa visiwa hivyo waking’olewa mapema kwenye michuano ya kimataifa.

Timu zao zimekuwa dhaifu kiasi cha kutisha, lakini rejea nyuma ambapo Malindi iliweza kufika mpaka hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Washindi mwaka 1995 kuonyesha kuwa soka la Zanzibar lilikuwa juu kwelikweli.

Nyota mbalimbali waliotetemesha na kutamba mpaka kwenye timu za taifa, Taifa Stars walitokea kwenye visiwa vya Zanzibar, lakini leo ni wachezaji wachache wa visiwa hivyo wanaotamba katika timu hiyo na wengi wao ni wale wanaocheza soka katika klabu za Ligi Kuu Bara.

Ndio maana Mwanaspoti inakumbusha mamlaka za soka za visiwani humo na Tanzania kwa ujumla kuwa, michuano ya Kombe la Mapinduzi itumiwe vema kama chachu ya kuleta mabadiliko katika soka.

Kwa mtindo huo huo wa kufanyika kila mwaka, Kamati ya Mashindano hayo inaweza kuboresha zaidi ili kuwa na msisimko zaidi na kuitumia kama njia ya mbadala ya kurejesha hadhi ya soka la Zanzibar.

Klabu shiriki kutoka visiwani humo na hata wachezaji kwa ujumla waitumie michuano hiyo kujifunza kitu kutoka kwa wachezaji wenzao wa nje ya visiwa hivyo, namna gani wanavyoweza kujitoa uwanjani kusaidia timu zao na hata kusonga mbele.

Hata makocha kupata fursa ya kukutana na wenzao wa nje ya nchi ni nafasi nzuri ya kuiga mbinu na ufundi na kuzitumia kwa vijana wao, ili kufanya timu zao kuwa bora na tishio hasa kwenye michuano ya kimataifa.