Kilichoikumba Stand United ni matokeo ya siasa

Muktasari:

  • Lazima migogoro hiyo itatoa mwanya wa ufujaji na matumizi mengine mabaya ya madaraka ambayo si rafiki kwenye uwekezaji wowote si kwenye michezo pekee hata katika sekta zingine.

JANA Alhamisi ilikuwa ni siku mbaya kwa mashabiki wa Stand United baada ya mdhamini mkuu wa klabu hiyo ambaye ni Kampuni ya Madini ya Acacia kutangaza kujitoa.

Uamuzi huo mgumu wa Acacia umefikiwa kutokana na kile wadhamini hao walichodai kwamba ni mgogoro uliopo baina ya viongozi kugombea madaraka na umiliki wa klabu huku wakishindwa kutekeleza makubaliano ya mkataba.

Acacia wanadai kwamba hali hiyo imekuwa si rafiki kwao kuwekeza kwenye klabu hiyo kwani kile wanachopangilia hakifanikiwi. Katika hali ya kawaida si Acacia tu, hata muwekezaji yoyote hawezi kutumbukiza fedha zake sehemu ambayo haijatulia, kwa vile katika hali kama hiyo si tu hawezi kufanikisha azma yake ya kujitangaza lakini hata matumizi ya fedha hayawezi kuwa sawa.

Lazima migogoro hiyo itatoa mwanya wa ufujaji na matumizi mengine mabaya ya madaraka ambayo si rafiki kwenye uwekezaji wowote si kwenye michezo pekee hata katika sekta zingine.

Kumekuwa na makundi kwa miezi kadhaa ndani ya Stand la viongozi wa kuchaguliwa na wale wanaotaka timu hiyo kuwa kampuni.Hali hiyo imeendelea kwa muda ndani ya timu hiyo ingawa mdhamini huyo alivumilia na kuendelea kulipa gharama mbalimbali ikiwemo makocha, wachezaji pamoja na mambo mengine ya uendeshaji.

Kinachoonekana kuiponza Stand ni siasa na uroho wa madaraka, jambo ambalo tunasikitika kuliona katika klabu changa ambayo tulitarajia kwamba ingeingia na staili mpya kwenye soka la kisasa kwavile imeanzishwa na vijana wengi ambao wanaelewa mambo yanavyokwenda kwenye dunia ya sasa.

Maoni yetu ni kwamba klabu ziachane na migogoro isiyokuwa na tija. Kilichotokea Stand kitaikwamisha kwenye ufanisi wao katika Ligi Kuu Bara na pengine huenda migogoro ikazidi zaidi kama itashindwa kumshawishi mtu mwingine kuwadhamini katika kulipa gharama mbalimbali.

Kuna wachezaji wa kigeni, makocha wa kigeni pamoja na gharama nyingine ambazo kwa udhamini pekee wa Azam Tv na Vodacom hauwezi kutosha. Matokeo yake ni nini? Huenda ikaanza migomo ya hapa na pale, wachezaji wakavunjika moyo wa kufanya kazi na vilevile hata mashabiki wakapungua kwa kiasi kikubwa uwanjani.

Jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo binafsi ya timu. Tunadhani, kama kuna uwezekano viongozi wakae chini walitafakari hilo kwa kina na ikiwezekana waelezane ukweli badala ya kukomoana.

Wapo baadhi ya viongozi wa Stand watakuwa wakifurahia kujiondoa kwa mdhamini ili wawakomoe wenzao lakini hilo siyo sahihi, timu ikifanya vibaya wataumbuka wote na hakuna ambaye atashangilia na kitakachotokea ni kudhohofisha soka la Shinyanga na Kanda ya Ziwa kwa ujumla.

Bila kubadilika na kuwa kitu kimoja, Stand haiwezi kuendelea wala kufika popote pale kisoka. Vilevile ni kipindi kama hiki ambacho mlezi wa klabu ambaye ni shirikisho linapaswa kuingilia kati na kuhakikisha kwamba migogoro inakomeshwa ili wadhamini waone mazingira rafiki kwenye soka na wavutike zaidi kuwekeza.

Hakutakuwa na ligi imara kama klabu zisipokuwa na fedha za kujiendesha na kulipa gharama mbalimbali.

Shirikisho lisifumbie macho haya mambo kwavile yataturudisha kwenye soka dhaifu la miaka ya nyuma ambalo lilikuwa likitoa nafasi kwa timu za Dar es Salaam tu kutamba kwavile zilikuwa vizuri kiuchumi.

Ni wakati huo ambapo klabu za mikoani zilikuwa zikipanda na kushuka msimu huohuo kutokana na ukata.

Tusifikie huko, tuachane na migogoro na siasa ambazo hazitusaidii tucheze mpira uwanjani na kila mtu atekeleze wajibu wake, siyo lazima wote tuwe viongozi wa soka wengine wabaki kuwa mashabiki.