Kilichofanywa na viongozi wa Simba hakikubaliki

Muktasari:

Ligi hiyo pia ilifikia tamati ikishuhudiwa Azam ambao kwa misimu mitano mfululizo ilikuwa haijawahi kushuka ndani ya Mbili Bora, ikimaliza msimu huu katika nafasi ya nne ikizidiwa maarifa na wakata miwa wa Kagera Sugar walitwaa nafasi ya tatu.

MSIMU wa Ligi Kuu Bara kwa mwaka 2016-2017 umefikia tamati juzi Jumamosi kwa kushuhudiwa timu za Toto Africans na African Lyon zikiungana na JKT Ruvu kushuka daraja na msimu ujao zitatua Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Kadhalika ilishuhudiwa Yanga ikimaliza msimu kwa aibu kwa kuchapwa bao 1-0, licha ya kutwaa ubingwa waliokadhibiwa Jijini Mwanza, likiwa ni taji lao la 27 tangu michuano ya ligi kwa Tanzania Bara ilipoanzishwa rasmi mwaka 1965.

Ligi hiyo pia ilifikia tamati ikishuhudiwa Azam ambao kwa misimu mitano mfululizo ilikuwa haijawahi kushuka ndani ya Mbili Bora, ikimaliza msimu huu katika nafasi ya nne ikizidiwa maarifa na wakata miwa wa Kagera Sugar walitwaa nafasi ya tatu.

Simba imekamata nafasi ya pili baada ya kuzidiwa ujanja na Yanga kwa tofauti ya uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa. Kifupi ligi imemalizika kwa staili ya aina yake, ila doa ni kitendo kilichofanywa na viongozi wa Simba cha kukataa kupokea medali zao za ushindi wa pili kwa madai wanaamini wao ndio mabingwa, eti tu kwa kuwa wamekata rufaa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).

Huu hauna tofauti na uhuni kwa klabu kubwa yenye miaka zaidi ya 80 kushindwa kuelewa taratibu na kanuni za soka na aina ya uendeshaji wake ulivyo na kuwatia aibu wanachama na mashabiki wengine wenye hadhi yao.

Hata kama Simba imekata rufaa, bado haikuwazuia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuendelea na taratibu zao za kuhitimisha ligi kwa maana ya kuwapa taji lao waliomaliza kileleni mwa msimamo wa ligi ya msimu huu, Yanga.

Inashangaza kwa viongozi Simba kuendesha ama kufanya mambo kama wahuni wa klabu za mitaani. Hii haikubaliki, ni lazima Simba iwaombe radhi mashabiki wa soka kwa kitendo hicho.

Rufaa haiwezi kuzuia mambo mengine kuendelea na wala sio mara ya kwanza kuwepo kwa rufaa, lakini mambo yakaendelea kusubiri maamuzi ambayo ndio yatakayoweza kuja kuweka mambo sawa, hata kama muda ukiwa umepita sana.

Tumeshuhudia Serengeti Boys ilipokata rufaa yao dhidi ya Congo Brazzaville bado Shirikisho la Soka Afrika (CAF) liliendelea kuitambua Congo kama wafuzu halali wa michuano ya Fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa Vijana U-17 na kuitoa baada ya kujiridhisha walitenda soka na kuwaondoa hata kwenye ratiba, lakini wakati huo Congo ilikuwa ikitambulika kama mshindi wa mechi hiyo, vipi Simba hawakuliona hilo. Uhuni ulioje huu.

Bahati mbaya ni kwamba Simba haikuikatia Yanga rufaa, bali inapinga maamuzi ya kupokwa pointi za mezani inazolilia baada ya kupoteza mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar kwa madai wapinzani wao walimchezesha kimakosa beki Mohammed Fakhi, akiwa na kadi tatu za njano.

Simba ilipewa pointi za dezo na Kamati ya Saa 72 kabla ya Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi ya Wachezaji kutengua uamuzi huo baada ya kubaini hakukuwa na udhibitisho wowote wa Fakhi kuwa na idadi hizo za kadi.

Hata hivyo, Simba imekuwa ikisisitiza itakata rufaa ikikumbushia hata mambo yaliyopita ambayo yalishaaamuliwa na TFF kwa makubaliano ya klabu hizo juu ya straika Mbaraka Yusuf, kama njia ya kutaka irudishiwe ushindi wa mezani.

Kama rufaa yao ingekuwa inaweza kuzuia michezo ya mwisho ya ligi, ingekuwa sahihi na kama viongozi wa soka waliopo katika klabu nyingine wangekuwa na maamuzi ya mwendokasi kama ya wenzao wa Simba, Azam nayo juzi ingegoma Kagera Sugar kupewa medali ya ushindi wa tatu.

Ndiyo. Hii ni kwa sababu kama Simba itapewa ushindi huo wa dezo, maana yake Kagera itapungukiwa pointi na kutoa mwanya kwa Azam kumaliza nafasi ya tatu juu ya Kagera Sugar, hivyo hata wao wangekataa ligi kuisha kabla ya rufaa kutolewa uamuzi.

Mwanaspoti linaamini viongozi wa Simba waliteleza kwa walichokifanya cha kuwazuia wachezaji wao wasipokee medali zao ama walifanya kusudi ili kutaka kuficha udhaifu wao mbele ya wanachama wao kwa kushindwa kubeba taji kwa msimu wa tano, ili ionekane TFF na watendaji wake wamewabania ubingwa.

Katika dunia ya sasa ambayo soka linaendeshwa kisomi na kisasa zaidi, viongozi wa klabu wanapaswa kufanya mambo kwa weledi na umakini kuepuka kuleta mambo ya aibu kama yaliyofanywa juzi kwenye Uwanja wa Taifa.

Tunaamini Simba wana haki ya kusubiria rufaa yao ili kusaka pointi wanazozitaka, lakini bado walipaswa kuheshimu mashabiki na wachezaji ambao ni heshima kwao kuvaa medali kwa nafasi waliyoipigania timu yao.

Hivi kama Fifa itashindwa kutoa maamuzi ya kuwapa pointi za mezani, itakuwa na maana gani kwa wachezaji ambao labda watakuwa wameshatawanyika makwao kupumzika kwani, msimu umeisha kwa kutokuwa na kumbukumbu ya medali waliyozipigania kwa miezi tisa ya ligi ya msimu huu?

Kwa hakika hii siyo sawa na viongozi wa Simba watumie uungwana.