Kiganja amethibitisha michezo sio kipaumbele chetu

Muktasari:

Jibu la haraka na lisilo na shaka linalonijia kichwani kila ninapotathmini na kuzichambua kwa umakini kauli hizo za Kiganja ambazo ndio msimamo wa baraza hilo, ni kwamba sekta ya michezo sio kipaumbele katika nchi hii.

NIMEKUWA msikilizaji mzuri wa kauli na matamko yanayotolewa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) hasa kupitia Katibu Mkuu, Mohammed Kiganja juu ya mabadiliko yanayotaka kutokea kwa klabu za Simba na Yanga.

Jibu la haraka na lisilo na shaka linalonijia kichwani kila ninapotathmini na kuzichambua kwa umakini kauli hizo za Kiganja ambazo ndio msimamo wa baraza hilo, ni kwamba sekta ya michezo sio kipaumbele katika nchi hii.

Zaidi ya mara tatu, Kiganja amenukuliwa akisema serikali haitambui aina ya mabadiliko ambayo klabu hizo mbili zinataka kuyafanya na watu ambao wanataka kufanya uwekezaji ndani ya klabu hizo ni vyema wakaanzisha timu zao.

Kiganja ameendelea kusisitiza hivyo wakati ambao wanachama wa Simba na Yanga wameonekana kuhamasika na hoja ya kuleta mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hizo mbili kongwe nchini.

Mwanzoni nilipata shida kumuelewa Kiganja kwa kuamini labda alizungumza kauli ya kuzuia mabadiliko ya kimfumo wa uendeshaji kwa timu hizo mbili kutokana na presha ya mtifuano ulioibuka baina ya wanachama wa Yanga pindi ulipoitishwa mkutano mkuu wa klabu hiyo Oktoba mwaka huu kwa lengo la kupewa mrejesho wa hatma ya ukodishwaji wa timu hiyo.

Lakini msisitizo alioutoa majuzi wakati alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya kufunga kozi ya ukocha kwa wanawake wanaosoma kwenye vyuo vikuu mbalimbali nchini, kuwa BMT halibariki mabadiliko hayo, umenifanya nithibitishe kuwa sekta ya michezo kwenye nchi hii haipewi kipaumbele.

Hakuna shaka, kuna mabadiliko makubwa yaliyoikumba sekta ya michezo duniani kote hasa soka, kutoka kwenye mfumo wa ridhaa na kuifanya iwe ya kibiashara kupitia uwekezaji uliofanywa na watu binafsi au kampuni mbalimbali duniani.

Mabadiliko hayo yameifanya sekta ya michezo kuhitaji uwekezaji wa kiasi kikubwa cha pesa katika kutengeneza miundombinu ya kuchezea kama viwanja na hosteli za wachezaji na kugharamia mishahara na huduma nyingine kama matibabu kwa wanamichezo na maofisa wanaosimamia.

Kwa muda mrefu sasa, sekta ya michezo nchini hasa soka imedorora na timu zetu zimekuwa hazifanyi vizuri pindi zinapokwenda kushiriki mashindano ya kimataifa, sababu hasa ikiwa ni nguvu hafifu ya kiuchumi zilizonazo kulinganisha na timu kutoka nchi nyingine.

Bado hakuna uwekezaji wowote uliofanywa na ama serikali au watu binafsi ambao pengine ungeweza kuziondoa timu zetu kutoka hapa zilipo hivi sasa na kuzipeleka katika mfumo bora zaidi wa kisasa ambao utazifanya ziweze kupiga hatua na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa badala ya kuwa wasindikizaji.

Kwa kuwa serikali imeshindwa kufanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya michezo, tulitegemea njia pekee ya kuinua michezo hapa nchini ni kufanya mabadiliko kwenye uendeshaji wa klabu zetu na kuruhusu wenye fedha wafanye uwekezaji ili angalau tuweze kushindana na wenzetu waliopiga hatua.

Kwa bahati nzuri, wafanyabiashara wawili nchini Yusuf Manji na Mohammed Dewji wamelitazama na kuligundua hilo na kuamua kujitosa kwenye timu za Simba na Yanga kutangaza nia ya kubadilisha mfumo wa uendeshaji wake.

Kwa Yanga, Manji anataka aikodishe kwa muda wa miaka 10 huku Dewji akitaka kuibadili Simba iingie kwenye mfumo wa hisa huku yeye akiomba kumiliki 51%.

Nia hiyo ya Manji na Dewji inaonekana kupokelewa kwa mikono miwili na wanachama na mashabiki wa timu hizo mbili kutokana na mazingira halisi yanayozikabili Simba na Yanga hasa yale ya kifedha kutokana na kuendeshwa kwa kutegemea fedha viingilio na wadhamini kwa muda mrefu jambo linalofanya zisipige hatua.

Lakini wakati wanachama wa Simba na Yanga wakianza kupata imani juu ya ukombozi wa klabu zao ambazo kwa miaka mingi zimeshindwa kujiweka katika sura ya kibiashara, matamko ya BMT yanaashiria wazi kuwa serikali haina nia ya kutaka kuona klabu hizo zinabadilisha mfumo wa uendeshaji wake.

Soka ni mchezo unaohitaji uwekezaji wa kiasi kikubwa cha pesa ili timu iweze kupata mafanikio tofauti na uendeshaji wa sasa wa klabu zetu ambao umezifanya zidumae na kushindwa kushindana na timu ambazo zimefanya uwekezaji wa kutosha.

Timu zetu haziwezi kufanikiwa kama zitaendelea kutegemea fedha za mapato ya milangoni, malipo ya ada za uanachama pamoja na kutegemea wafadhili na wahisani na badala yake zinahitaji kujiendesha kwa mfumo wa kibiashara na sio kuwa ombaomba.

Katika nchi ambayo hata bajeti yake ya Wizara ya Michezo kwa mwaka ipo chini zaidi ya dau la usajili la kiungo Mkenya, Victor Wanyama ambaye alinunuliwa kutoka Southampton kwenda Tottenham, tulitegemea kuwa ukombozi pekee kwa timu zetu ni kuruhusu watu wenye fedha kufanya uwekezaji ambao utazifanya ziweze kujisimamia.

Inawezekana isiwe ni Manji au Dewji lakini tukubaliane kuwa uwekezaji kwenye klabu zetu na sekta ya michezo kwa ujumla ndio njia pekee ya kutuwezesha kushindana na timu au nchi zilizopata mafanikio michezoni.

Nilitegemea baraza ndilo lingekuwa taa kwa klabu zetu katika kuyaendea mabadiliko hayo ambayo watu wanayapigania hivi sasa, lakini matamko yanayotolewa yanazidi kukatisha watu tamaa kuwa michezo kwenye nchi hii inaonekana kama ni sekta isiyo na manufaa yoyote.

Nadhani baada ya muda mrefu wa kujiuliza juu ya hatma ya maendeleo ya sekta ya michezo nchini na sapoti ya serikali katika kuhakikisha inapiga hatua, nadhani baraza limeamua kututhibitishia michezo sio kipaumbele Tanzania.

Ni wazi serikali inaona michezo kama jambo la kujifurahisha tu, Kiganja na BMT wametumika kama mabalozi wa kutufikishia ujumbe huo nasi tumeupokea!