Kelele za chaguzi za mikoani zichunguzwe

Muktasari:

  • Kadhalika wanataka kuona kama atakaporejea kutetea kiti chake atafanikiwa kukitetea mbele ya wapinzani watakaojitokeza ambao baadhi yao wamekuwa wakitajwa japo wenyewe hawajawahi kukanusha wala kukubali watajitosa.

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) unatarajiwa kufanyika Oktoba mwakani, ikihitimisha miaka minne ya uongozi wa Rais Jamal Malinzi.

Malinzi na wenzake waliingia madarakani Oktoba 27, 2013 na kwa mujibu wa Katiba ya shirikisho hilo muhula mmoja wa uongozi ni miaka minne.Tayari kumeanza kampeni za chini chini kuelekea uchaguzi huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na wadau wa soka, hasa kutaka kujua kama Rais Malinzi atarejea kutetea kiti chake ama atawapisha wengine.

Kadhalika wanataka kuona kama atakaporejea kutetea kiti chake atafanikiwa kukitetea mbele ya wapinzani watakaojitokeza ambao baadhi yao wamekuwa wakitajwa japo wenyewe hawajawahi kukanusha wala kukubali watajitosa.

Lakini katika kuelekea uchaguzi huo, tayari baadhi ya vyama vya soka vya mikoa ambao ni wanachama wa TFF, vimekuwa vikifanya chaguzi zao, vipo ambavyo vimeshapata viongozi wao wapya na vipo vingine vinaendelea kuchaguana.

Katika chaguzi hizo za vyama wanachama wa mikoa wa TFF zimekuwa zikielezwa kujaa utata, figisufigisu na sintofahamu hasa kwa baadhi ya wagombea ambao hujitokeza kuwania nafasi kwenye vyama hivyo ama wale waliochaguliwa.

Asilimia kubwa ya chaguzi zilizofanyika ama zinazoendelea kufanyika kumekuwa na kelele nyingi za wadau wa soka juu ya kuwepo kwa mizengwe na hali ya kubaniwa kwa baadhi ya wanaojitokeza kuwania nafasi kwenye chaguzi hizo.

Mizengwe imekuwa ikielezwa kufanyiwa kwa viongozi wanaowania nafasi za juu ama zile zinazowapa fursa waliozishikilia kushiriki uchaguzi mkuu wa TFF, kitu kinacholeta sura na hisia mbaya kuwa kuna kitu nyuma ya mizengwe hiyo.

Kadhalika sehemu kubwa ya nafasi za juu au zenye kutoa fursa ya viongozi wake kushiriki uchaguzi mkuu wa TFF zimekuwa ama zikiwania na mtu mmoja bila mpinzani au wale wanaojitokeza wakati mwingine wakiwa na sifa hujitoa ama kung’olewa dakika za mwishoni.

Hili halipo kwenye chaguzi za ngazi za mikoa tu, hata kwenye chaguzi za wilaya imekuwa ikishuhudiwa hali hiyo, ikizingatiwa kuwa viongozi wa wilaya ndio wanaoshiriki chaguzi za mikoa zinazotoa viongozi wa kwenda uchaguzi wa TFF.

Kutokana na hali hiyo na kuzidi kwa kelele za kuwepo kwa hila za makusudi zinazofanywa kwa kile kinachoelezwa kutengenezwa mtandao wa kuelekea  uchaguzi mkuu wa mwaka wa TFF tulidhani kuna haja ya suala hili kufuatiliwa.

Inawezekana kelele hizo zikawa na mashiko na zinaweza zikawa kama za mfa maji, lakini bado kuna umuhimu wa kufuatiliwa kwa chaguzi hizi, ili kubaini ukweli wa kinachozungumzwa kila uchao.

Yapo madai ambayo hayajathibitishwa kuwa, wanaojipanga kuwania uchaguzi ujao wa TFF na hasa baadhi ya viongozi waliopo madarakani ndani ya taasisi hiyo wanaweka watu wao katika vyama vya mikoa ili kurahisisha nafasi zao mwakani.

Haya ni madai, yanayoweza kusemwa na yeyote, ila ili kupata ukweli wake ni lazima uchuguzi ufanyike, ndio maana Mwanaspoti linadhani ipo haja mamlaka zilizopo hasa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kuingia kazini.

Kwa mujibu wa sheria za nchi hasa za chaguzi, ni kosa kubwa mtu kutengeneza mazingira ya ushindi kwa hila, iwe kwa siri ama dhahiri. Kufanya hivyo kwa mtu kutengeneza mazingira ya ushindi kwenye uchaguzi iwe wa kitaifa ama ule wa vyama kama TFF na vyama vingine maana yake ni kununua madaraka kwa hila. Ndio maana tunaamini, Takukuru na idara nyingine za kisheria zinaweza kuanza sasa kufuatilia chaguzi hizo za vyama vya soka kuanzia wilayani hadi mkoani ili kuona kana kuna ukweli wowote.