Kauli moja tu ya Magufuli viwanja vyetu vinakuwa Old Trafford

Tuesday February 7 2017

 MCL

WAKATI mwingine Donald Trump hakukosea sana kuhusu mtu mweusi au Waafrika jinsi tulivyo. Kuna baadhi yetu walimtukana sana wakati wa kampeni zake. Waliamini kuwa alikuwa anawadhalilisha Waafrika na watu weusi popote walipo.

Hapana, kuna vitu vingi alikuwa anasema kweli. Mwafrika ni mzembe na amelala. Ana akili tegemezi. Hatazami kesho. Wachache sana wana maono ya mbali. Wengi wanaitazama leo. Wanakula wanalala.

Kila ninapofikiria kuhusu viwanja vyetu vya soka huwa nacheka sana. kwa sasa mechi za mikoani zinazochezwa mbele ya kamera za Azam TV zimegeuka kuwa kichekesho. Sehemu ya kuchezea ni aibu tupu. Mchezaji anaweza kupiga pasi lakini mpira huohuo ukadunda na kumpiga kanzu mwenyewe.

Mbaya zaidi unaambiwa hilo ni pambano la Ligi Kuu. Inakuwa vigumu kujua tofauti ya mechi ya Ndondo Cup na Ligi Kuu. Kinachochekesha zaidi kila mtu anaongea halafu anaacha iwe kama ilivyo. Huu ni uzembe wa Mtanzania. Ni uzembe wa asili.

Kuvirekebisha viwanja hivi ni suala la kusawazisha sehemu ya kuchezea na kupanda nyasi nzuri kisha kumwagilia asubuhi na jioni bila ya kusubiri mvua. Baada ya hapo unazikata vema na kumwagilia tena na tena kuanzia Jumanne ya wiki hii mpaka Jumanne ya wiki ijayo bila ya kujali kama kuna mechi au hakuna.

Inasemwa kwamba viwanja vingi nchi hii ni vya CCM. Ndiyo, walivichukua wakati wa kuelekea katika mfumo wa vyama vingi. Wakavihodhi ingawa vilitengenezwa kwa nguvu za wananchi. Vilipaswa kuwa viwanja vya serikali.

Kwa sasa Rais wetu ni mkali sana. Mheshimiwa John Pombe Magufuli. Akiongea neno nchi nzima inatetemeka. Bahati nzuri Rais mwenyewe ni Mwenyekiti wa CCM. Hauwezi kuamini kuwa Magufuli akitia neno moja tu kuhusu ubovu wa viwanja, hasa sehemu ya kuchezea basi kila kitu kitabadilika.

Utashangaa nyasi zimetoka wapi. Utashangaa mabomba yametoka wapi. Utashangaa uangalizi umetoka wapi. Utashangaa ghafla karibu kila uwanja unakuwa kama huu mkubwa wa Taifa. Kuanzia Mkwakwani Tanga, Jamhuri Dodoma, Jamhuri Morogoro, Majimaji Songea, Nangwanda Sijaona Mtwara na vinginevyo.

Magufuli akitoa kauli moja tu ndio utajua nani anahusika hasa na jukumu la kututengenezea sehemu ya kuchezea ndani ya uwanja. Magufuli akitokea kauli moja tu kila kitu kitakwenda sawa na tutaanza kusikia raha kutazama mechi za mikoani katika TV. Kama kuna anayebisha basi amtie Rais moto atoe amri.

Hivi ndivyo mtu mweusi anavyota. Hivi ndivyo mtu mweusi alipofika. Kama unabisha jaribu kujiuliza jinsi ambavyo imefika wakati unakutana na choo cha shimo kilichotengenezwa kwa msaada wa watu wa Marekani.

Unajiuliza, tatizo lilikuwa ardhi? Tatizo lilikuwa watu wa kuchimba? Tatizo lilikuwa zana za kuchimbia? Ni maajabu gani yamefanyika kutoka kwa Wamarekani? Hapa ndipo tulipofika. Hatutaki kuishirikisha akili katika mambo ya msingi na yale ya kawaida.

Kama kuna mtu anabisha basi atengeneze mazingira ya Magufuli kutoa kauli hii kwa ukali kwa wasimamizi wa viwanja. Atoe kauli kali kwa viongozi wa CCM wa mikoani. Hata akiwapa mwezi tu utashangaa kila kitu kimekwenda sawa.

Donaldo Trump hakukosea sana. akili zetu zimekaa katika namna hii. Jiulize, kabla hata Magufuli hajatoa neno unadhani kinashindikana nini kwa wahusika kuhakikisha viwanja vinakuwa na sehemu nzuri ya kuchezea.

Hatuhitaji majukwaa bora. Tupo tayari kusimama kwa dakika tisini ili mradi unachokiona uwanjani kinaeleweka. Kwa sasa tunachokiona ni aibu. Mechi nyingi hazistahili kuitwa za Ligi Kuu. Wahusika wamelala wanasubiri amri kali ya Magufuli.

Natamani mtu wa karibu wa Magufuli amfikishie hii makala ili atoe kauli kali halafu aache tu uone jinsi watu wanavyohangaika huku chini. Tumezoea kuishi kama mbwa. Tumezoea kupokea amri. Hatujazoea kuwa wabunifu na kuchoka ujinga tunaouona.

Binafsi kama nikipata fursa ya kuonana na Magufuli hiki ndicho nitakachomwambia kwa haraka kuhusu soka letu kabla hatujaongea kuhusu mambo mengine. Inakera kutazama mechi ya Simba na Mtibwa pale Morogoro halafu ikiwa haina tofauti na mechi ya mtaani kwetu.