SHERIA 17 : Kadi za Blagnon, Himid Mao na umakini wa mwamuzi

Muktasari:

  • Ni timu zilizosheheni wachezaji wenye uwezo wa ndani pamoja na wa nje ya nchi, ulikuwa ni mchezo wa kuvutia na hii ilichangiwa pia na umakini wa Mwamuzi, Elly Sasii, mwamuzi kijana aliyejitaidi kuchezesha vizuri mechi hiyo.

MCHEZO wa Ligi Kuu Bara kati ya Azam na Simba uliochezwa juzi Jumamosi umedhihirisha ubora wa timu hizo na namna ambavyo timu hizo zina mashabiki wengi katika soka la Tanzania.

Ni timu zilizosheheni wachezaji wenye uwezo wa ndani pamoja na wa nje ya nchi, ulikuwa ni mchezo wa kuvutia na hii ilichangiwa pia na umakini wa Mwamuzi, Elly Sasii, mwamuzi kijana aliyejitaidi kuchezesha vizuri mechi hiyo.

Kwa mwonekano tu mwamuzi alikuwa makini na alichokuwa akikiamua, hakuwa mwenye kubahatisha katika maamuzi yake, alikuwa anajua nini alichokuwa akikifanya.

Alielewa vizuri sheria na namna ya kuzitafsiri kwa vitendo, kwa umakini huo huo aliweza kuwamiliki wachezaji wa timu zote mbili na kutumia vizuri mamlaka aliyokuwa nayo kama mwamuzi. Na si vibaya nikisema kwamba alistahili kuwa nyota wa mchezo huo. Ndio kwani mwamuzi anapokuwa uwanjani naye kiutaratibu ni mmoja wa wachezaji.

Katika mchezo huo kuna baadhi ya mambo yaliyojitokeza kwa wachezaji wa timu zote mbili, upande mmoja ni mabaya na kwa upande mwingine ni mazuri na yanastahili sifa.

Kwa mfano katika dakika ya 25 ya mchezo huo, mchezaji wa Simba, Ibrahim Ajib alijitengenezea nafasi nzuri kabisa ya kufunga bao lakini kwa kutokuwa makini alipoteza nafasi hiyo.

Kwa wachezaji makini kama Zamoyoni Mogella enzi zake akiwa Simba au Robbie Fowler wa Liverpool ya enzi hizo au Raul Gonzalez aliyekuwa Real Madrid kwa nafasi kama zile ilikuwa hawakukosi.

Kwa Ajib ilikuwa nafasi nzuri ya kumchambua kipa atakavyo, lakini alikosa utulivu wa kuitumia nafasi ile na akaamua kupiga shuti ilimradi tu lilielekea golini.

Japo ni wazi kwamba hakupenda akose bao lile lakini kwake kama mshambuliaji tegemeo wa kufunga halafu anakosa bao kama lile halikuwa jambo zuri kwani ameinyima timu kitu kizuri.

Lakini pia pongezi ziende kwa kipa Aishi Manula kwa kuokoa mpira ule, alitekeleza wajibu wake, alijua ni wakati gani atoke golini ili kumkabili Ajib na akafanikiwa katika hilo.

Pia, katika dakika ya 88, Fredrick Blagnon wa Simba alishindwa kuitumia nafasi baada ya Mugiraneza kushindwa kuucheza mpira alioukusudia kuutoa nje akaukosa na kuanguka chini, Blagnon akiwa katika nafasi nzuri ya kuendelea kuikimbiza mpira ule lakini akajitengenezea faulo, kwa kujikwaa kwenye mguu wa Mugiraneza na kujiangusha chini akitafuta huruma ya mwamuzi.

Hata hivyo, tukio hilo lilimsababishia kupewa kadi ya njano kwa kosa la kujaribu kumdanganya mwamuzi. Ilikuwa kadi sahihi kabisa kwake na hapa ndipo Mwamuzi Sassi alipofanya jambo ambalo hata mwamuzi wa kati aliyechezesha mechi ya Chelsea na Liverpool Ijumaa iliyopita alishindwa kuling’amua kosa la aina hiyo lililofanywa na Lucas wa Liverpool, mwamuzi alimwadhibu Lucas wakati hakuwa na kosa.

Katika mchezo wa Simba na Azam mwamuzi pia alimuonyesha Himid Mao kadi ya njano katika dakika ya 17, hii pia ilikuwa kadi sahihi kutokana na kosa la kumwangusha Shiza Kichuya ingawa Mugiraneza akiwa umbali wa mita kama 10 hivi kutoka kwenye tukio hilo alimkimbilia mwamuzi akionyesha ishara ya kupinga kadi aliyopewa Mao.

Kama ningekuwa mimi ndiye mwamuzi ningeachana na Mao na ningeshughulika na Mugiraneza kwani alikuwa akitetea na kuchochea uvunjifu wa sheria za soka hivyo, ilipaswa aanze kuadhibiwa yeye pengine kabla hata ya Mao.

Katika dakika ya 20, mwamuzi aliashiria ishara ya faida ya mchezo (Advantage) kwa mchezaji Aboubakar Salum baada ya kufanyiwa faulo na mchezaji mmoja wa Simba lakini mpira ulimfikia Jon Bocco na mwamuzi akaruhusu mchezo uendelee, lilikuwa jambo zuri.

Katika dakika ya 57 Kadi ya njano ya Shiza Kichuya ilikuwa sahihi baada ya kufanya kosa la kupoteza muda kwa kupiga mpira uliokufa ambao uliwekwa ili uanzishwe tena.

Mwamuzi huyo alishapiga filimbi na kuashiria mpira upihwe kwenda upande wa Simba, lakini ukiwa umeshatengwa Kichuaya akaenda kuugusa na kuurudisha nyuma.

Kwa ujumla mchezo ulikwenda vizuri na mwamuzi alijitahidi sana kuumuliki ingawa makosa madogo madogo ya kibinadamu hayawezi kukosekana, alishirikiana vizuri na wasaidizi wake na kwa jumla hawakupishana katika maamuzi.

Kama ningekuwa kamishna wa mchezo huo ningempa mwamuzi wa kati alama 8.7 na wasaidizi wake wote ningewapa alama 8.5 kwa kazi nzuri waliyoifanya mwamuzi wa kati kumsaidia kuchezesha vizuri pambano hilo.