KUTOKA BONDENI : Tuiandae Serengeti Boys kwenda Afcon 2021

Muktasari:

  • Sasa Watanzania wanatarajia kuiona Serengeti Boys kwa mara ya kwanza ikishiriki kwenye fainali hizo zitakazofanyika nchini Gabon.

HATIMAYE Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), limeiondoa timu ya vijana ya Jamhuri ya Kongo katika Fainali za Vijana wenye umri chini ya miaka 17 Afrika, na nafasi hiyo kupewa timu ya Serengeti Boys baada ya rufani yao kukubaliwa.

Sasa Watanzania wanatarajia kuiona Serengeti Boys kwa mara ya kwanza ikishiriki kwenye fainali hizo zitakazofanyika nchini Gabon.

Wengi wetu tunafahamu njia ambayo Serengeti Boys imepitia hadi kufikia hatua hii. Tunajua panda-shuka nyingi ambazo zimeikumba timu hii katika safari yake hadi kufikia hatua ya kukata rufaa CAF baada ya Kongo kumchezesha ‘kijeba’ katika mechi ya mwisho.

Yote hayo yamepita na sasa kinachosubiriwa ni kuwashuhudia vijana wetu kwenye fainali hizi za Gabon.

Serengeti Boys imekuwa timu ya mwisho kupata nafasi hii. Ikumbukwe kuwa timu nne zitakazoingia hatua ya nusu fainali, zitapata tiketi ya moja kwa moja kucheza Kombe la Dunia kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17.

Kwa mantiki hiyo, fainali hizi za Gabon ni muhimu kwa timu yetu sio tu kwa ajili ya kuonyesha uwezo wa vijana wetu, bali pia kusaka tiketi ya Tanzania kucheza fainali za Kombe la Dunia kwa vijana kwa mara ya kwanza.

Fainali zitakazofanyika nchini India Oktoba mwaka huu.

Baadhi ya timu shiriki zimeanza maandalizi ya muda mrefu kwa ajili ya kujiweka sawa kwa fainali hizo. Mataifa mengine yamepeleka timu zao ughaibuni kwa ajili ya kuwaweka sawa wachezaji wao kutoa ushindani mkubwa na hata ikibidi kutwaa kikombe hicho.

Hakuna uchawi katika kufikia mafanikio, cha muhimu ni maandalizi ya kutosha ikiwa ni pamoja na vijana kuwekwa sawa kiakili kwa ajili ya michuano hiyo.

Wakati wa safari nzima ya kuelekea kufuzu kwa fainali hizi, vijana wa Tanzania walionyesha kandanda safi ambalo lilitoa matumaini ya Tanzania kuwa na timu bora ya soka ya taifa siku za usoni. Ikumbukwe kuwa timu bora ya taifa, lazima ianze kuandaliwa kuanzia hatua ya chini kabisa. Tusitarajie kuwapata wachezaji bora wa Taifa Stars ikiwa hatutakuwa na maandalizi mazuri kwa ‘yosso’ wetu wa leo.

Kama jinsi tunavyopiga kelele kila siku kuhusu timu za Ligi Kuu kuzilea vizuri timu zao za vijana, hivyo hivyo ndivyo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linavyotakiwa kuzilea vema timu zote za vijana za leo kwa ajili ya kuwa na timu bora ya Taifa Stars kesho.

Ikiwa Serengeti Boys itapewa maandalizi mazuri licha ya kusalia muda mfupi wa maandalizi ikilinganishwa na wenzetu, upo uwezekano wa kufikia walau nusu fainali ya michuano hii ya Afrika kwa vijana.

Kama nilivyosema awali, uwezo walioonyesha vijana wetu wakati wa mechi za kufuzu, ndio unaotupa matumaini kuwa timu inaweza kabisa kufanya vema kwenye mashindano hayo.

Kufika nusu fainali ina maana kuwa tayari tumekata tiketi ya kucheza Kombe la Dunia kwa vijana. Na safari haitaishia hapo tu, kwani vijana hawa watakuwa tayari wamepata uzoefu mkubwa wa soka la kimataifa na hivyo kuanza kujenga timu bora ya Taifa Stars kwa miaka ijayo.

Mpaka sasa, hakuna dalili za mpango wowote madhubuti wa kuandaa kikosi kwa ajili ya kufuzu kwa fainali za Afrika (Afcon) mwaka 2019.

Licha ya wengi kudai kuwa ‘eti’ Tanzania tumepangwa katika kundi laini, lakini kutokuwepo kwa mipango ya mapema ni dalili tosha ya kutokufuzu kwa Afcon 2019.

Tukiweza kuwekeza kwa ukamilifu kwa vijana wetu hawa wa leo wa Serengeti Boys, upo uwezekano walau wa kuweza kuota ndoto za kufuzu kwa fainali za Afcon 2021.

Hebu tujaribu kuwekeza sasa kwa vijana hawa wa Serengeti Boys wa leo huku tukilenga vijana hawa kutupatia tiketi ya kufuzu kwa Fainali za Afcon 2021. Siku zote ndoto za kupiga hatua katika michezo huanza kwa vijana chipukizi, sasa vijana hawa wameonyesha njia kwa hiyo kilichobaki ni kuwashika mkono na kupanda.