KONA YA MCHARAZO: Simba shauri yenu, mkijivuruga tu, imekula kwenu!

Muktasari:

  • Inawezekana ni kweli kipa Vincent Angban amefungwa mabao laini kwa uzoefu wake wa mechi za kimataifa, lakini ndio sababu ya kutafutiwa mbadala wake?

KWA hakika haikuwa wiki nzuri hata kidogo. Kwani kumekuwa na vifo mfululizo vya vigogo serikali na wanamichezo kwa jumla.

Vifo vya Samuel Sitta, Joseph Mungai, Hafidh Ali Tahir na Said Mohammed ni baadhi ya vifo vilivyofululiza ambavyo vimeacha simanzi sio kwa wanafamilia, ndugu na jamaa za wahusika, bali hata wanamichezo kwa ujumla.

Binafsi na kwa niaba ya wasomaji wa kona hii, tunawaombea ndugu zetu waliotangulia mbele ya haki wasamehewe na kupokelewa vema na Mola Muumbaji wa Mbingu na Ardhi, huku tukifanya maandalizi ya safari yetu.

Naam kwa hakika kila nafsi itaonja mauti na hakuna atakayesalimika, muhimu ni kuhakikisha tunamuomba Mungu atujalie tufe katika njia sahihi. Inshallah!

Licha ya majonzi hayo mazito ya vifo vya wenzetu, lakini maisha ya soka yaliendelea kama kama kawaida, ingawa Ligi Kuu Bara imemaliza mzunguko wake wa kwanza, ikishuhudiwa Simba ikimaliza kileleni.

Mashabiki wa soka pamoja na kukosa uhondo wa ligi ya ndani na ile ya kimataifa, lakini mechi kadhaa za kusisimua za kuwania Fainali za Kombe la Dunia kwa mwaka 2018 ziliendelea huku ikishuhudiwa baadhi ya vigogo wakigawa dozi.

Taifa Stars ambayo haishiriki michuano yoyote kwa sasa baada ya kufanya vibaya katika mashindano yote waliyoshiriki, ilikuwa ugenini Zimbabwe kucheza kirafiki na wenyeji wao na sina shaka matokeo mmeyasikia.

Lakini wakati tukitafakari mapumziko ya Ligi Kuu Bara, tukumbuke pia kuwa, pazia la dirisha dogo la usajili linafunguliwa kesho Jumanne na zoezi kitadumu kwa mwezi mzima mpaka Disemba 15, siku chache kabla ya duru la pili la ligi hiyo kuanza tena (kama TFF haitazingua tena ratiba iliyoitoa mapema).

Kipindi hiki cha dirisha la usajili ni neema kwa wachezaji na hata wapiga dili waliopo ndani ya klabu kubwa ambazo kila usajili wao wamo.

Licha ya kutaka kuwashtua wachezaji kuwa makini katika kipindi hiki, ili wasije wakapotea, pia nilikuwa natoa angalizo kwa makocha na mabosi wa klabu zitakazojitosa kwenye usajili huo wa dirisha dogo.

Sio lazima kila klabu ifanye usajili kwa sasa, ila kwa maeneo ambayo ni muhimu ama yaliyoonekana kupwaya katika duru la kwanza.

Kwa mfano sasa zimeanza kusikika tetesi kwamba vinara Simba baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo, ipo kwenye mpango wa kupangua kikosi chake kwa maeneo ya kipa, mabeki na ushambuliaji.

Sitaki kuuingilia maamuzi ya viongozi wa Simba ama kuwapinga, ila wajiulize ni kweli timu yao inahitaji mabadiliko kwa sasa, wakati timu inaonekana kuwa imara msimu huu kuliko misimu kadhaa iliyopita?

Inawezekana ni kweli kipa Vincent Angban amefungwa mabao laini kwa uzoefu wake wa mechi za kimataifa, lakini ndio sababu ya kutafutiwa mbadala wake? Kidogo linaloingia akilini ni kupatikana kwa mabeki wa pembeni wa kumsaidia Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na mtu wa kufiti nafasi ya beki ya kulia.

Hamad Juma na Malika Ndeule bado hawajaaminiwa kikosini, lakini ni wazuri kuliko hata Janvier Bukungu ambaye kiasili ni beki wa kati.

Kwenye safu ya mbele, inawezekana ni kweli Emmanuel Okwi anahitajika kurejeshwa, lakini mbona kuna wachezaji wazuri tu katika nafasi hiyo, ila muda mfupi wa maandalizi ya duru la kwanza huenda imechangia kuyumbisha safu hiyo, ambayo hata hivyo imefanya vema mpaka sasa.

Simba ndio timu inayoshikilia nafasi ya pili kwa kuwa na mabao mengi nyuma ya Yanga, huku beki yao ikiwa imara ikiruhusu mabao machache mbele ya timu zote za ligi hiyo.

Kwa mfano Laudit Mavugo anasakamwa, lakini watu wakumbuke hakuanza katika maandalizi ya Simba chini ya Joseph Omog mjini Morogoro, ndio maana anaonekana kuwa tofauti na wenzake kinyume na matarajio ya wengi. Lakini naamini kipindi hiki anaweza kulishwa mbinu na kocha wake na kuja  kutisha duru lijalo nani anajua, hivyo ni sawa na Ame Ali ‘Zungu’ na wengine.

Wana Msimbazi ni kama wamepaniki kwa matokeo ya mechi mbili za mwisho dhidi ya African Lyon na Prisons, lakini ni wajibu wao kutuliza akili ili kurekebisha mapungufu yaliyopo kwa sasa kikosini, timu yao bado ina nafasi ya ubingwa. Naamini Simba ni msimu wao wa kutwaa ubingwa, muhimu wasijivuruge kabisa kwani hata msimu uliopita walijichanganya wenyewe na kutoa mwanya kwa Yanga na Azam kuwazidi akili wakati nafasi ilikuwa yao dhahiri.

Ni ushauri tu!