JICHO LA MWEWE: Jonas Mkude, ndio nahodha wangu wa mwendokasi

Muktasari:

  • Simba wakajikuta wakicheza 10 uwanjani huku bao la Tambwe likiendelea kuwa bao. Unaweza kumtetea Mkude kwamba eti alikasirika sana, hapana alifanya ujinga kwelikweli.

AMISS Tambwe aliunawa mpira kabla hajafunga. Tuanzie hapo. Sioni kama kuna utata katika hili. Ni kweli, Tambwe uliutuliza mpira kwa mkono akamfunga kipa wa Simba. Narudia tena hakuna utata katika hili. Picha za video zimerudia. Picha za mnato za magazetini zimeonyesha.

Baada ya sekunde moja tu ya kutafakari, wachezaji wa Simba wakamvaa mwamuzi, Martin Saanya wakiongozwa na nahodha, Jonas Mkude. Kazi ya nahodha ni kumiliki hasira za wachezaji wake. Mkude alikuwa anaongoza hasira za wachezaji wake badala ya kuzimiliki.

Mwishowe baada ya kumsukuma mwamuzi alipewa kadi nyekundu. Simba wakajikuta wakicheza 10 uwanjani huku bao la Tambwe likiendelea kuwa bao. Unaweza kumtetea Mkude kwamba eti alikasirika sana, hapana alifanya ujinga kwelikweli.

Yanga ilifungwa bao la aina hiyo na Madaraka Suleiman Machi 31, 2002. Walimzonga mwamuzi baadaye yakaisha. Hakuna mchezaji wao aliyemsukuma mwamuzi achilia mbali nahodha Ken Mkapa aliyejitenga na vurugu. Hawa ndio walikuwa manahodha halisi na wanaotakiwa.

Katika miaka ya karibuni Simba imekuwa ikitumia vigezo vya ajabu sana kuchagua manahodha wake. Inachagua manahodha kwa kigezo cha kuwa mchezaji wa zamani zaidi ndani ya kikosi cha sasa. Kwa kigezo hicho hicho waliwahi kumchagua Hassan Isihaka kuwa nahodha wa timu, miezi 15 tu baada ya kuingia kikosi cha kwanza akitokea Simba B. Na ndicho kigezo ambacho kimetumika kumchagua Mkude. Katika hali ya kawaida, nahodha ni mchezaji mwelewa, kiongozi, anayedhibiti jazba zake binafsi na za wenzake. Lakini pia anahitajika kuwa mchezaji mwenye uzoefu na aliyepitia kasheshe mbalimbali za soka.

Kwa mfano, Mkude anaweza kumuongoza vipi Method Mwanjali, staa wa kimataifa wa Zimbambwe ambaye amewahi kuwa nahodha wa Mamelodi Sundowns ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini. Hii ni moja kati ya timu tatu kubwa Afrika Kusini.

Mwanjali pia amewahi kuwa nahodha wa klabu kubwa ya Zimbabwe CAPS United. Lakini pia amewahi kukipiga Mphumalanga Aces. Kokote alikopita, Mkude hajawahi kukaribia kufika, anawezaje kuongozwa na Mkude?

Sitaki kumzungumzia Mwinyi Kazimoto, ambaye naye angeweza kufaa kutokana na uzoefu wake wa soka la ndani hadi lile la kulipwa alilocheza hivi karibuni Uarabuni, ukijumlisha na idadi ya mechi nyingi za timu ya taifa alizocheza kuliko Mkude.

Yanga sio wajinga kumfanya Vincent Bossou kuwa nahodha wao huku Kevin Yondani na kina Mbuyu Twite aliowakuta katika timu wakiwa humo humo uwanjani. Ni kwa sababu wameangalia uzoefu wake ndani na nje ya uwanja.

Ni kama ninavyoshangaa kuona baadhi ya wachezaji wa Azam, John Bocco, Salum Abuubakar au Himid Mao wakiwa manahodha wa timu mbele ya Paschal Serge Wawa aliyecheza mechi lukuki za kimataifa na kukumbana na kasheshe nzito katika soka.

Mechi ya juzi ilikuwa ya Simba. Baada ya ujinga wa mwamuzi, Mkude alipaswa kuchukua mpira na kuuweka kati huku akiwasihi wenzake watulie. Mpaka wakati Yanga wanafunga bao la Tambwe hawakuonekana kuwa tishio kabisa kwa Simba.

Simba wangeweza kutulia na kusawazisha bao hilo mapema. Ungeweza kuona hata baada ya kuondoka kwa Mkude bado Simba hawakuonekana kuwa na pengo lolote kubwa uwanjani huku wakiicheza mechi kama kawaida mpaka wakaja kufunga bao la kusawazisha jioni.

Nahodha anapaswa kuwa mchezaji anayefikiria kwa haraka sana nini kinaendelea katika mchezo. Mkude alipaswa kufikiria kwa haraka kwamba bao la Tambwe halikuwa mwisho wa maisha, hasa kwa kiwango cha Simba na Yanga iliyofungwa na Stand United siku chache zilizopita.

Kutafakari haya kwa haraka unahitaji sio lazima tu uwe nahodha, bali uwe mchezaji wa kulipwa unayejitambua. Mkude anaonekana kutokuwa na sifa yoyote kati ya hizi mbili. Tatizo letu kubwa ni kuendekeza ushabiki katika soka.

Mwisho wa mechi, Mkude alienda nje ya uwanja akiwa tumbo wazi katika eneo ambalo mashabiki wa Simba wanatokea. Alijua ambacho kingefuata. Kwa sababu mashabiki wa Simba walikuwa na furaha na bao la Shiza Kichuya waliamua kumbeba wakishangilia.

Unakwendaje katika mlango wa kutokea wa mashabiki lukuki wa kawaida?  Pengine ni kutaka sifa, lakini kwa lipi hasa? Kama timu ingefungwa, licha ya uzembe wa Saanya kutoona mkono wa Tambwe, bado Mkude angekuwa ameiangusha timu yake.

Simba inaingia lawamani kwa kutuletea manahodha wa mwendokasi. Tumetoka kwa nahodha Talib Hilal, kina Mussa Kihwelo (marehemu), halafu kina Hussein Marsha na sasa inatuletea manahodha wa mwendokasi katika vigezo ambavyo havieleweki.

Nahodha wa mwisho wa Simba ambaye nilikuwa namuelewa sana alikuwa Joseph Owino. Kichwa chake hakikuwa na moto na pia alikuwa ni mwanadamu anayejielewa ndani na nje ya uwanja. Jaribu kujenga taswira ni kitu gani ambacho Owino angefanya baada ya Saanya kuchemka juzi? Unafikiria angeweza kumsukuma mwamuzi? Simba ijitafakari.