Jinsi Kocha Simba alivyochezea kibarua chake dhidi ya Yanga

Tuesday February 28 2017

 

By FRANK SANGA

KOCHA wa Simba, Joseph Omog alijitafutia presha ya bure, lakini pia akakiweka kibarua chake rehani.

Haikuwa hivyo tu. Kocha huyo wa raia wa Cameroon alijitafutia matatizo kwa mashabiki na hata viongozi wake wa klabu hiyo ya Msimbazi, nina uhakika kama mambo yangekuwa tofauti wasingemuelewa.

Ni bahati nzuri kwake kwamba Simba ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, Jumamosi iliyopita pale Uwanja wa Taifa.

Kwenye mazungumzo ya vijiweni wiki nzima kabla ya mchezo huo, Simba ilikuwa inaongoza dhidi ya Yanga nje ya uwanja.

Mashabiki, viongozi na hata wachezaji wa Simba waliamini wanakwenda kushinda mchezo huo. Hawakuwa na sababu ya msingi ya kuweza kutetea hoja zao, labda pengine waliangalia jinsi walivyowafunga Yanga kwa penalti katika michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Pengine waliamini misukosuko anayoipata Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji ingechangia kufanya vibaya kwa timu hiyo ya Jangwani.

Binafsi sikuwa na mawazo hayo, niliona mechi ikiwa ngumu zaidi kwa Simba kuliko Yanga. Kwa sababu kwa kawaida watu wanapokuwa na matatizo huwa na umoja kuliko wakati wowote ule.

Hata ukiangalia kipindi cha kwanza cha mchezo, Yanga walionekana timu zaidi kuliko Simba ambao ungedhani wameokotana barabarani na kwenda kucheza mechi ya bonanza.

Huwa sipendi kuwalaumu makocha kwa sababu ninaamini kuwa, wamesomea kazi zao na sisi wengine hatupaswi kuingilia kazi zao kwa sababu wao wanakaa na wachezaji muda mrefu kuliko sisi.

Lakini nimeshindwa kujiuzuia kumlaumu Omog ambaye ninamuona alijitafutia matatizo yasiyo ya lazima katika mchezo huo wa watani hao wa Kariakoo.

Katika mechi ambayo unamkosa beki wako wa kati Method Mwanjali unatakiwa kuwa makini sana kupanga kikosi dhidi ya wapinzani wako, tena mabingwa watetezi na wakongwe.

Unapokuwa na mabeki wa kati Abdi Banda na Novaltus Lufunga, tayari ujue una matatizo katika eneo hilo na hasa kutokana na Yanga kuwa na washambuliaji wenye kasi kama Amissi Tambwe na Obrey Chirwa.

Kwa vyovyote vile, mabeki wa kati Abdi Banda na Novalt Lufunga walihitaji mtu wa kuwalinda mbele yao, ambaye hakuwa mwingine zaidi ya Jonas Mkude.

Mkude anaijua vizuri Yanga, ana uzoefu wa mechi kubwa, anafahamu presha ya mechi hizi, ni nahodha wa timu, amekaa muda mrefu, hawezi kukaa benchi katika mechi hiyo muhimu na kubwa.

Sina maana kuwa kiungo wa Ghana, James Kotei hakustahili kucheza, hapana, alicheza vizuri, lakini bado Mkude atabaki kuwa Mkude na hasa katika mechi kubwa kama ya Yanga.

Kosa la kwanza la Omog ilikuwa ni kumuweka benchi Mkude katika mechi kubwa kama hiyo, kwa sababu hata Mwanjali angekuwapo uwanjani, bado angehitaji ulinzi wa Mkude mbele yake.

Lufunga hakuwa fiti katika mchezo huo na ndio maana alisababisha penalti iliyofungwa na Simon Msuva wa Yanga. Kuanzia hapo Lufunga hakurudi tena kwenye mchezo ule, akawa anafanya makosa mengi. Katika hili huwezi kumlaumu Lufunga, kwamba ndiye mwenye makosa hapa ni Kocha Omog aliyempa mazingira magumu, Mkude angemsaidia zaidi kumpa ulinzi.

Safu ya mabeki wa Simba haikuwa nzuri, bado kocha akafanya kosa jingine la kumtoa Lufunga akaingia Shiza Kichuya, hivyo mabeki wa Simba wakawa pungufu na haikuwa ajabu kuona Janvier Bokungu akipewa kadi nyekundu kutokana na presha kubwa waliyoipata kutoka kwa washambuliaji wa Yanga.

Hii ina maana kuwa Simba ilibakia na mabeki wawili karibu kupindi chote cha pili; Mohammed Hussein na Abdi Banda.

Ni jambo hilo ambalo lilimlazimisha Omog kumuingiza Mkude ambaye alisaidiana vyema na Kotei kuituliza Yanga na kuwafanya Simba watawale kipindi cha pili.

Omog hawezi kukwepa lawama kwa yaliyotokea kuanzia penalti na kadi nyekundu, anapaswa kujua kuwa mechi kubwa kama hiyo zina wachezaji wake na huwezi kuwaweka benchi mtu kama Mkude na Kichuya.

Jambo jingine ambalo lilinishangaza kwa Omog ni alipoanza na washambuliaji watatu; Juma Liuzio, Ajib Ibrahim na Laudit Mavugo.

Nilijua Simba wangeshambulia sana, badala yake wakajilinda sana, nikabaki kushangaa kwa nini majina matatu ya washambuliaji yawe uwanjani, halafu timu inajilinda wakati kama lengo lilikuwa hilo wangeweza kuwa na viungo wengi zaidi. Simba ilishinda, lakini kocha aliwapa mashabiki presha isiyo ya lazima na yeye mwenyewe alijipa wakati mgumu na kibarua chake kilikuwa hatarini.

Bahati pekee katika mchezo huo ni kuwa Simba ilishinda, lakini kama ingefungwa makosa mengi ya Kocha Omog ingekuwa vigumu kuyatetea.a