Jicho la Mayanga limeweza kukusanya kundi zuri Stars

Muktasari:

Inakufanya kocha kuwa na uwanja mpana wa kumgundua mchezaji, uhodari wake na mapungufu aliyonayo pia anapotekeleza mambo mengi ndani ya uwanja.


HII ndio moja kati ya faida ya kuwa na kocha anayewajua kiundani wanasoka wa nchi hii. Kocha ambaye amekuwa akikutana na mikikimikiki ya wachezaji kwenye Ligi Kuu Bara na hata kwenye michezo ya kawaida wanayoshiriki wachezaji wa Tanzania.

Inakufanya kocha kuwa na uwanja mpana wa kumgundua mchezaji, uhodari wake na mapungufu aliyonayo pia anapotekeleza mambo mengi ndani ya uwanja.

Faida kubwa anayoipata kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Salum Mayanga, ni ile ya kuwajua kwa undani wachezaji wa Tanzania huku wengi wao akiwa amewafundisha kwa nyakati mbalimbali.

Kingine kinachomfaidisha Mayanga ni ile hali ya kucheza na kizazi cha wachezaji fulani hivi waliowahi kuwa pamoja miaka kama mitatu nyuma, kizazi cha wachezaji waliocheza kwenye kikosi cha Ngorongoro Heroes chini ya mkufunzi Kim Poulsen.

Kundi hilo linawakosa akina Ranadhani Singano, Juma Abdul, Salum Telela na wengineo wachache, lakini ndo hawa akina Shomari Kapombe, Said Ndemla, Jonas Mkude, Frank Domayo na Thomas Ulimwengu huku wakiongezewa nguvu na wadogo zao Ibrahim Ajib, Hassan Banda, Hassan Kessy, Mubaraka Yussuf na wengineo.

Hao wananogeshwa na uwepo wa wazoefu kiasi wa siku nyingi kama Deogratias Munishi, Erasto Nyoni na wengine wa umri wa akina Mkude waliokuwa wamesahaulika kama Simon Msuva na Salum Mbonde.

Kocha Mayanga amekuwa bingwa tayari kwa sababu jicho lake limegundua vipaji halisi vya wachezaji ambao watadumu kwenye kikosi hicho si chini ya miaka minne hadi mitano kama wataendelea kuwa kuwapo katika timu za Simba, Yanga na Azam.

Hakuna wasi kuwa hizi ndizo timu ambazo wachezaji wake wengi wanapata michezo mingi ya kirafiki na ya kimashindano ya kimataifa ndani na nje ya nchi. Licha ya nchi kuwa na uwakilishi wa vilabu viwili tu kwenye mashindano ya kimataifa, bado timu moja kati ya hizo inayokuwa imekosa uwakilishi ina uwezo wa kualika timu kutoka nje ya nchi na kucheza nayo au wao wenyewe kwenda nje ya nchi.

Hii ndiyo faida anayokwenda kupata kocha Mayanga kwa kuwachagua wachezaji hao tofauti na wale wanaokuwa kwenye timu kama Mtibwa, Prisons na nyinginezo za kariba hiyo, ingawa bado mchanganyiko wa aina hiyo haukwepeki.

Kwa hiyo Mayanga anapata faida kubwa kutokana na aina ya wachezaji alionao ambao wanaweza kubadilika kutokana na aina ya timu wanayokwenda kucheza nayo na kwa matakwa ya kocha.

Kiufundi kundi hili lilicheza vizuri kwenye mechi ya kwanza ya Taifa Stars chini ya kocha Mayanga, ilikuwa dhidi ya Botswana.

Wakitumia mfumo mama wa 4-4-2 ambao Watanzania wameuzoea sana kuanzia timu za mchangani, Stars iliandika ushindi wa mabao 2-0.

Pamoja na kwamba ulikuwa mfumo huo, lakini kwa jicho la ndani unaweza kuwaona wachezaji wawili Shiza Kichuya na Simon Msuva ambao ni mawinga waliofanya mfumo huo kuonekana kama 4-2-4 na hii ndiyo iliyowafanya viungo Himid Mao na Frank Domayo kupotea katikati kwa kuwa si rahisi Msuva au Kichuya kutekeleza majukumu ya viungo kwa asilimia kubwa.

Lakini kundi hili lilikuja kubadilika vizuri na kuucheza mfumo wa 4-2-3-1 kwa ufasaha zaidi kwani ngome ya Stars ililindwa na viungo Himid Mao na Mzamiru Yassin huku Msuva, Salum Abubakar na Farid Mussa wakicheza nyuma ya Ibrahim Ajib ambaye kidogo alishindwa kusimama juu kwa kuwa amezoea kucheza nyuma ya mshambuliaji wa juu.

Nafasi hiyo ya mshambuliaji wa mwisho bado ingeweza kuchezwa vyema na Mbaraka Yussuf aliyekuwa nje. Sasa hii ndio ya faida anayopata kocha Mayanga kwani kundi hili linaweza kubadilka kutoka kucheza mfumo mmoja hadi mwingine.

Kupitia wachezaji hawa, Mayanga anaweza kuibadili timu hata kutumia mifumo tunayoiona ikitumiwa sana Ulaya ya 4-3-3 au 3-4-3 na bado timu ikacheza kwa mpangilio na uwiano mzuri zaidi.

Nchi inaonekana kupungiwa mabeki huku ikiwa tajiri wa viungo. Moja ya umasikini tulionao Watanzania ni uvivu wa kuchagua maumbo ya wachezaji warefu wanaotakiwa kucheza eneo hilo.

Ndio maana tunamwona, Dickson Daudi, wa Mtibwa akiwa bado yupo uwanjani hadi leo nikwa sababu ya umbo lake zuri.

Bado hata kocha Mayanga anahusika kuangalia wachezaji wenye maumbo mazuri warefu watakaoweza kuwasaidia akina Mbonde na Banda.

Si vibaya kuwapa nafasi akina Salum Kimenya na wengineo wanaoweza kuziba na kucheza vizuri eneo hilo kwani, wanaweza kubadilika.